Thursday, July 16, 2009

MBUNGE wa kuteuliwa na mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru ameushambulia waraka wa kichungaji uliotolewa na Kanisa Katoliki nchini, unaoelekeza namna ya kupata kiongozi anayefaa kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu ujao adai kuwa utaligawa Taifa.
Kingunge alitoa kauli hiyo alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ambayo iliwasilishwa na George Mkuchika bungeni mjini Dodoma jana.
Hata hivyo, Kanisa Katoliki kupitia Baraza lake la Maaskofu (TEC), limekuwa na utamaduni wa kutoa mwongozo kama huo wakati Taifa linapoelekea Uchaguzi Mkuu, huku kumbukumbu zikionyesha kuwa pia lilifanya hivyo mwaka 2005.
Katika kikao hicho cha jana kilichokuwa chini ya Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama aliyekuwa mwenyekiti, Kingunge alizungumza kwa msistizo huku akiwataka wabunge wamsikilize kwa makini na kutahadharisha kwamba asinukuliwe vibaya.
``Na sasa nimalize, nina jambo moja kubwa, naomba mnisikilize kwa makini, lakini msininukuu vibaya. Kanisa Katoliki, viongozi wake rafiki zangu, wale wa juu nawafahamu sana, Kanisa hilo limetoa mwongozo kuelekeza anayefaa kuchaguliwa katika uchaguzi ujao.
“Mimi nikautafuta na kuusoma. Sasa hili Kanisa Katoliki linatoa mwongozo wa kuchagua kiongozi wa kisiasa, kwa maana hiyo huu ni mwongozo wa Wakatoliki. Si utakuwa mwongozo wa Wakatoliki pekee?” alisema Kingunge akihoji.
Aliendelea kusema: “Kwa hiyo KKKT (Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania) nao watoe mwongozo kwa sababu wao hawaongozwi na Kanisa Katoliki, ni Wakristo ndiyo, lakini mantiki tu. KKKT wakitoa, Pentekoste watatoa wakwao na Anglikana bado, nao watatoa wakwao, Waislamu bado na wao watoe wa kwao.”
Kingunge ambaye ni mmoja wa wabunge wa muda mrefu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu enzi za Mwalimu Nyerere Rais wa Kwanza wa Tanzania aliongeza kuwa anazungumza hayo kwa kuzingatia mantiki ya mwongozo huo.
“Ni mantiki tu, nasema kwa heshima zote nawaomba viongozi wa Kanisa Katoliki, nawapenda sana, nawaomba warudishe ule mwongozo wao, sisi tunataka nchi moja na tuishi pamoja kwa kushikamana, hatutaki kugawanyika kama Lebanon,” alisema Kingunge bila kufafanua zaidi kuwa waurudishe wapi na kwa vipi.
Kauli hiyo ya Kingunge imetolewa wakati waraka huo wa Kanisa Katoliki umezua mjadala miongoni mwa watu wa kada mbalimbali, huku baadhi wakilishutumu kanisa hilo wakidai kuwa linaingilia masuala ya kisiasa.
Hata hivyo, juma lililopita Askofu Msaidizi wa Kanisa hilo Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodius Kilaini alisema mafisadi wanauhofia mwongozo huo.
Kwa mujibu wa Kilaini mwongozo huo unaweka vipaumbele vya nchi katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ndiyo maana wanaupinga.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya misa ya upadrisho iliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jimboni humo, Kilaini alisema mwongozo huo ulianza kutumika tangu uchaguzi wa mwaka 1995 na kusisitiza kuwa kwa mwaka huu watu wengi wameshtuka kutokana na kugusa masuala ya ufisadi.
Kanisa hilo lilitoa vitabu viwili vya mwongozi na vipaumbele vya nchi kabla ya kuuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2010, mwongozo ambao umekumbana na vipingamizi kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kwa madai kuwa dini inaingilia mambo ya siasa.
“Kwanza napenda watu waelewe kuwa mwongozo hauna lolote kuhusu dini kama watu wanavyodhani, kwa sasa jamii imeshituka kuhusu vitendo vya rushwa na ndiyo sababu baadhi ya wanasiasa wanapinga muongozo huo kwa kuwa unalenga kuwafungua watu macho na kukemea vitendo vya ufisadi,” alisema Kilaini na kuongeza.
“Ninachowataka wanasiasa wote washiriki kupiga vita ufisadi. Asiyetaka kupigana na ufisadi tusimchague na ndivyo mwongozo huo unavyosema,” alisema.
Alifafanua kuwa mwongozo huo unazungumzia juu ya serikali na msimamo wake na wala si kumchangua mtu fulani wala chama fulani kwa ajili ya kumpa uongozi.
“Watu wausome mwongozo huo kwa moyo mweupe na ninaamini wataufurahia, utakuza ufahamu juu ya masuala ya kidemokrasia,” alisema Kilaini.
Awali Mbunge wa Kigoma Kusini, Manju Msambya alishutumu mwongozo huo aliouita kuwa ni "Waraka wa Kiaskofu" wakati akichangia hotuba ya makadirio na matumizi ya Wizara ya Sheria na Katiba, akisema unawafundisha waumini wake kuhusu namna ya kuchagua viongozi kwa imani zao na kuonya kuwa nchi inaweza kuingia kwenye vurugu.
Msambya ambaye hakutaja moja kwa moja dhehebu la dini lililotoa waraka huo, alisema unapingana na kanuni inayosema watu wasichanganye dini na siasa.
Lakini Askofu Kilaini alisema mwongozo huo haukutungwa na maaskofu wala mapadri wa Kanisa hilo na kufafanua kuwa umetungwa na Chama cha Wataalam wa Kanisa Katoliki (CPT) na kwamba wao waliupa baraka zote baada ya kuusoma na kuona unafaa.

Source: Mwananchi

No comments: