Monday, August 30, 2010

Fujo Kanisani

Timbwili la kufa mtu limezuka katika Kanisa la Kiroho la Christ International (CIC) kufuatia baadhi ya waumini na viongozi wa Kamati Kuu wa Kanisa hilo kumkataa kiongozi wao Mkuu (Mchungaji) aliyefahamika kwa jina la John Meena kufuatia kitendo chake cha kutia makufuli milango ya kanisa hilo na tuhuma nyingine.

Kimbembe hicho kilichodumu kwa takriban dakika thelathini, kilichukua nafasi Jumamosi Agosti 28, 2010 katika kanisa hilo lililopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia songombingo hiyo ambayo kwa akili zisizokwenda kawaida ingetoa tafsiri kama ni filamu mahiri ya waigizaji maarufu wa Kiamerika.

Awali ilidaiwa kwamba, Mchungaji Meena alilifunga kanisa hilo kwa makufuli yake binafsi na uongozi ulipobaini hivyo uliyavunjilia kwa mbali na waumini wa kanisa kuendelea na shughuli zao za kila Jumamosi mpaka Mchungaji Meena aliporudi na kukuta makufuli yake yakigalagala chini.

Aidha, licha ya mwenye makufuli hayo kufika, viongozi hao na baadhi ya waumini walimtadhaharisha asikanyage ndani ya kanisa hilo huku wakimchimba mkwara kuwa, kufanya hivyo kungeweza kumfanya akione ‘cha moto’.

Hata hivyo, habari zinadai kuwa, wapo waumini waliotaka kutuliza hali ya hewa, ndipo sintofahamu kubwa ilipoibuka na kufanya mahali hapo kuwa kama uwanja wa ‘mapambano’.

Baada ya kuona hivyo, ndipo Mchungaji Meena alipoamua kukimbilia Kituo cha Polisi Mabatini ambapo dakika chache mbele, Polisi walifika ingawa nao walishindwa kuweka mambo sawa kwani viongozi wa kanisa hilo walisisitiza kuwa, hawamtaki Mtumishi huyo wa Mungu.

Hata hivyo, mwisho wa yote, polisi hao waliamua kuondoka na Mchungaji ‘wao’ hadi kituoni kwa lengo la kumwokoa asishambuliwe na viongozi wenzake walioonekana kukamatwa sawasawa na jazba.

Kuhusu tuhuma nyingine ilidaiwa kuwa, Mchungaji Meena amekuwa hasikilizani na viongozi wenzake na amekuwa akijiamulia mambo mengi peke yake wakati katiba ya kanisa hilo inamtaka kuandaa Kamati ya Baraza la Kanisa katika kila maamuzi.

“Kila Kamati ikitaka kukaa ili kuweka mambo sawa Meena (Mchungaji) amekuwa hasikilizi, amekuwa akijinadi kuwa, yeye ni kiongozi na atakayemsikiliza ni Roho Mtakatifu tu siyo watu wa kamati, matokeo yake ni kama haya,” alisema Mchungaji wa kawaida wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina la Asijile Moses.

Mchungaji Asijile aliongea kwa niaba ya wenzake na kuendelea kudai kuwa, kutokana na tabia hiyo kanisa hilo ambalo awali lilikuwa na waumini zaidi ya 130, sasa limepukutika kwa wengi kukimbia na kubaki 35 tu.

Kanisa hilo wakati linaanzishwa lilikuwa chini ya Mchungaji Mnigeria Samuel Oluseyi Olufemi ambaye alitimuliwa nchini na Idara ya Uhamiaji kwa kosa la kutotosheleza vigezo vya sheria vinayomruhusu kuishi Tanzania.

Source: GlobalPublishers.info

No comments: