Monday, August 30, 2010

MCHUNGAJI WA EAGT AFUNGWA JELA MIEZI 6

Mchungaji wa Kanisa la EAGT lillilopo mtaa wa Ichenjezya mjini Vwawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya Simon Kitwike (48) jana alijikuta akihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani, baada ya kudharau mahakama kwa kukataa kuapa ili atoe ushahidi kutokana na imani ya Dini.

Mchungaji huyo aliyevunjiwa nyumba yake mwishoni mwa mwaka jana na kuibiwa mali kadhaa za nyumbani kwake alifika katika mahakama ya wilaya ya Mbozi ili kutoa ushahidi wake, lakini alikataa kuapa kabla ya kutoa ushahidi wake akidai ni dhambi.

Hakimu wa mahakama ya wilaya Kajanja Nyasige alimwamuru asome kifungu katika Biblia kinachomtaka asiape mahakamani, ndipo mchungaji huyo alifungua Biblia na kusoma kitabu cha Mathayo 5: 35 kuwa ndicho kinachompa msimamo huo.

Baada ya kusoma kifungu hicho Hakimu Nyasige alimuuliza tena mshitakiwa (shahidi) kama atakuwa tayari kuapa ili aweze kuendelea na kutoa ushahidi wake mahakamani, hata hivyo mshitakiwa huyo aliendelea kubaki na msimamo wake wa kukataa kuapa.

Ndipo Hakimu huyo alimsomea kifungu cha sheria na 198 (1) kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 kinachokataza mtu kudharau Mahakama na kuwa kuendelea kukataa kuapa ni kuvunja sheria na hivyo anatenda kosa la jinai.

Hata hivyo hakimu Nyasige aliendelea kumvumilia mchungaji huyo ili aweze kubadili msimamo wake kwa kumwamuru asome Biblia hiyo tena Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 13:1- 5, shahidi huyo alisoma kifungu hicho mbele ya mahakama, lakini alipoulizwa kama amebadili msimamo wake alijibu kuwa hawezi kubadili msimamo wake, kwa aya hiyo ya waraka na akasisitiza kuwa msimamo upo pale pale.

Hakimu Nyasige alilazimika kumsomea hukumu na kumtia hatiani kutokana na kosa la kuidharau mahakama, hivyo anamhukumu kwenda jera miezi sita na kuwa atatakiwa kuja kutoa ushahidi wake kwa kesi ya msingi Marchi 2, mwaka huu.

Mwandishi wa habari hizi alimhoji Mchungaji mwandamizi wa Kanisa hilo aliyejitaja kwa jina moja la Mwakasaka ambaye alisema amesikitishwa na hukumu hiyo na akadai kuwa mchungaji wake alielewa vibaya vifungu vya biblia vinavyozungumzia viapo.

Naye Mchungaji Erasto Makalla wa kanisa la Pentekoste alieleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo ya mchungaji kupingana na mamlaka ya serikali na akasema kuna haja ya kuwafanyia semina wachungaji ili waelewe taratibu za serikali.

Matukio ya upinzani yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara wilayani hapa ambapo mwaka juzi waumini wa madhehebu ya Mashahidi wa Jehova walikuwa kwenye mgogoro na serikali baada ya kukataza wanafunzi wasiimbe wimbo wa taifa na kuheshimu bendera.

No comments: