Thursday, December 23, 2010

Kuna ujumbe gani ndani ya Christmas?

Salamu za Christmas kutoka kwa Frank Lema
"Kwa Mungu hakuna lisilowezekana"

Bwana Yesu Asifiwe!
Ninamshukuru na kumsifu Mungu
"Kwa kuwa ni mwema, na kwa maana fadhili zake zadumu hata milele-Zaburi 106:1" kwa kutupa mimi na wewe zawadi hii ya kufika wakati huu wa mwaka na pia, kwa zawadi hii ya kufika wakati huu wa Christmas. Babu yangu mkubwa alifariki juzi tarehe 20 December,yaani siku 5 kabla ya Christmas, akiwa na miaka 96. Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya kuwa naye kwa miaka yote hiyo, lakini pia inatukumbusha wote kuwa ile tuu kwamba tunapata nafasi ya kuifikia Christmas, ni neema hiyo, kwa maana tumeona kuwa si wote waliopata nafasi hiyo.

Tunaposheherekea sikukuu za Christmas, napenda sana tusheherekee huku tukijifunza jambo ambalo Roho Mtakatifu ametupa kulifahamu wakati huu wa kukumbuka kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Hivyo, karibu tujifunze kwa ufupi mambo muhimu yaliyoambatana na Christmas;

"Tunamhitaji Roho Mtakatifu kwa ajili ya mafanikio yetu"

Tutatafakari story ya Christmas kama ilivyoandikwa katika Luka 1:26-38.(click hapa kusoma) Katika maandiko hayo, tunasoma namna Malaika Gabriel alivyopeleka ujumbe wa kuzaliwa Yesu kwa bikira Mariamu, na kumweleza "Sikiliza, utapata mimba, nawe utazaa mtoto wa kiume; na utamwita jina lake Yesu. Mtoto huyo atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Aliye Juu. Na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Mfalme Daudi, baba yake. Atatawala juu ya nyumba ya Yakobo daima; na ufalme wake hautakuwa na mwisho!'' Kama maneno hayo yalivyo wazi, huo ndio uliokuwa ujumbe wa Mungu kwa bikira Mariamu. Huu ulikuwa ni ujumbe mwema na wa kupendeza. Lakini Mariamu akauliza "Lakini, nitapataje mimba, na mimi ni bikira?" Na ninataka tujifunze kitu hapo. Ni kwanini bikira Mariamu aliuliza swali hilo? Ni kwasababu kwa kawaida yetu sisi wanadamu, tuna taratibu ambazo tumezikuta hapa duniani na tunaamini ni lazima hizo zifuatwe ili tupate jambo fulani jema, kama vile ambavyo Mariamu alijua kuwa haiwezekani kupata mtoto kama anavyoambiwa wakati bado hajaolewa ili akutane kimwili na mume wake, na kisha apate mtoto. Kwa maneno mengine, Marimu alitegemea kuwa angeambiwa maneno hayo ya kumzaa mtoto baada ya yeye kuolewa na Yusufu, hapo asingekuwa na haja ya kuuliza swali hilo. Kwa hiyo kilichosababisha lile swali la Marimu na taratibu ambazo tumezikuta katika ulimwengu huu, na ambazo tunadhani kuwa ni lazima zifuatwe ili Mungu aweze kutubariki. Sasa hebu tulitazame jibu la Malaika Gabrieli kwa Mariamu, Malaika alimjibu,Malaika akamjibu, ``Roho Mtakatifu atakujilia na nguvu za Mungu zitakufunika kama kivuli, na kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu" Umeona maneno hayo? Malaika alimjibu na kumwambia Mariamu kuwa, kinachotakiwa ili maneno hayo yatimie siyo mwanaume, bali ni "Roho Mtakatifu kumjilia na nguvu za Mungu kumfunika kama kivuli" Umeyaelewa maneno hayo? Mungu akikwambia kuwa atakupeleka nchi fulani kusoma au kufanya kazi, hahitaji uwe na ndugu yako katika nchi hiyo ili akupokee na kukusaidia, unamhitaji Roho Mtakatifu na Nguvu za Mungu ili kukufanikisha katika hilo. Mungu akikwambia atakupa kazi katika shirika fulani la kimataifa, huhitaji kumfahamu bosi fulani ili jambo hilo litimie, unamhitaji Roho Mtakatifu na Nguvu za Mungu, Yeye ndiye atajua akusaidie vipi. Mungu akikwambia utafaulu masomo yako vizuri, unamhitaji Roho Mtakatifu na Nguvu za Mungu ili uweze kusoma kwa bidii na ufaulu....

Wakati huu wa Christmas, Neno hili likae moyoni mwako kwamba, unachokihitaji ili ahadi za Mungu zitimie kwako siyo taratibu za dunia hii, unamhitaji Roho Mtakatifu na Nguvu za Mungu kukufanikisha, hivyo, mwombe Mungu akujaze Roho wake na Nguvu zake.

"Baraka na Laana katika ulimi wako"

Watu wengi waliookoka ni wagumu sana kukiri mambo mema hata kwa ajili yao wenyewe. Mkute mtu amepata ajira na ameanza kufaya kazi, mwambie "hongera kwa kupata kazi, muda si mrefu utajenga nyumba" utamsikia anakujibu "Ahh, wapi bwana, kazi yenyewe ya kubangaiza tuu" Katika Christmas hii, napenda ufahamu kuwa maneno unayoongea yanaweza yakawa kama vile manukato au mavi. Maana yake, kila maneno unayozungumza, kuna roho zinafuatia hayo maneno. Ukizungumza maneno ya baraka kwako, Malaika wa Mungu wanayafuatia maneno hayo mema ili kuyafanya kwako. Unapotamka maneno ya kukudidimiza, maneno yasiyofaa, mapepo yanafuata maneno hayo na kukuzuilia mafanikio yako kama ulivyokiri, yaani, ni kama vile ambavyo inzi huwa wanafuata mavi mahali yalipo, ndivyo mapepo yafanyavyo.

Hebu tujifunze kwa Mariamu, yeye alisemaje Malaika alivyomwambia namna atakavyompata mtoto? Angalia " Mariamu akasema, ``Mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema." Kisha malaika akaondoka. Umeona namna Mariamu alivyoipokea hiyo baraka upesi? Jifunze hapo, mtu akikwambia neno jema/la kukubariki, hata kama hajaokoka, wewe sema "Amen, namshukuru Mungu kwa kuwa itakuwa hivyo" sema hata kwa sauti ya kunong'oneza kama unaona aibu! kuliko kukaa kimya au kukataa baraka hiyo. Sawa?

Fanya mambo makubwa na wewe!

Katika wakati wa Christmas, kuna baadhi ya nyimbo ambazo hupendwa duniani mwote na zimejipatia umaarufu mkubwa. Wimbo mmojawapo ni "Joy to the World" na mwingine ni "Silent Night" na nyimbo hizi ni nzuri sana. Hebu fikiria, wimbo wa Joy to the World ulitungwa na ndugu mmoja aliyeitwa Isack Watts mwaka 1719, kwa hiyo leo wimbo huu una miaka 281,na bado unapendwa sana dunia nzima, (na pengine hata wewe unaupenda!), Silent Night ulitungwa na Father Joseph Mohr mwaka 1816 na uliimbwa mara ya kwanza December 24, 1818 kwa hiyo leo una miaka 192 na bado tunaupenda sana. Tazama namna watu hawa walivyoweza kwa nguvu za Mungu kutunga nyimbo hizi za Christmas ambazo zinapendwa hadi leo dunia nzima, na wewe dhamiria kwa msaada wa Mungu kufanya jambo ambalo litabaki likimtukuza Mungu hata baada ya wewe kuondoka katika ulimwengu huu. Kumbuka maneno ya Malaika "Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilo wezekana.''Luka 1:37.

Roho Mtakatifu ajuaye kuyafafanua maneno ya Mungu kwa ufasaha wote akufundishe zaidi.

Unaposherehekea Christmas, maneno haya yawe moyoni mwako na uyazingatie kuyafanya, wafundishe na wengine pia. Christmas ni wakati wa kuwa karibu na pamoja kwa familia zote, jitahidi uwe karibu na familia yako.

Tuombe...

"Baba katika Jina la Yesu, Asante sana kwa kunipa mimi neema ya kufikia kipindi hiki ninapoadhimisha kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Asante kwa maneno haya ambayo umenifundisha ili niyazingatie wakati huu ninaposheherekea Christmas. Ninaomba uendelee kunifundisha niione Christmas kama unavyoiona Wewe. Ninaomba unipe Roho wako Mtakatifu na nguvu zako, na unifundishe mimi kukiri maneno ya baraka katika maisha yangu. Ninaomba wakati huu wa Christmas uwe ni wakati wa uzima kwangu, kwa rafiki zangu na kwa watumishi wako wote. Nimeomba haya nikiamini, kwa Jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, Amen"

Hizi ndizo salamu zangu za Christmas kwako, na, ndiyo kusema;

Merry Christmas and a Jubilee New 2011 Year!

Frank Lema,
The Kingdom News,
www.thekingdomnews.org,
savedlema2 at yahoo dot com,
December 23,2010.

No comments: