Wednesday, December 8, 2010

Mufti Simba adai Serikali imekubali kurejesha Mahakama ya Kadhi


SHEIKH mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba.


SHEIKH mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba amedai kuwa serikali imekubali kuirejesha Mahakama ya Kadhi nchini na kwamba mchakato wake ulisimama kupisha uchaguzi mkuu.

Mufti Simba alisema hayo jana alipokuwa akitoa salamu za mwaka mpya wa Kiislaamu wa 1432AH na akaweka bayana kuwa kipaumbele kikubwa kwa Waislamu katika mwaka huo ni kuona Mahakama ya Kadhi inaanza kazi na serikali kuitambua siku ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu kwa kuifanya iwe ya mapumziko.

Mchakato wa Mahakama ya Kadhi unaendelea na umefikia mahala pazuri kwa sababu serikali imeshakubali kuirejesha," alisema Mufti Simba.

Kauli hiyo ya Mufti Simba imetolewa baada ya makamu wa rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kueleza Novemba 17 wakati akijibu salamu za Baraza Kuu la Waislamu kuwa Waislamu nchini wataona matunda mazuri ya kilio chao hivi karibuni.
“Kuhusu Mahakama ya Kadhi, insha-Allah Mungu tutawafikisha kuona matunda mazuri muda si mrefu,” alisema Dk Bilal.
Kilio cha Waislamu kudai Mahakama ya Kadhi kiliongezeka katika miaka miwili iliyopita wakati walipoanza kuishambulia serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi ya chama tawala ya kuwaanzishia chombo hiyo kwa madai ni sehemu ya ilani yake ya uchaguzi wa mwaka 2005.

Baada ya mvutano wa muda mrefu na viongozi wa dini ya Kiislamu, serikali ilitoa taarifa kuwa Mahakama ya Kadhi itaundwa nje ya mfumo wa sheria za nchi na kuunda kamati ya kushughulikia utekelezaji wa maazimio hayo.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mufti Simba aliwatoa wasiwasi Waislaamu wote nchini kuhusu Mahakama ya Kadhi akieleza kuwa mchakato wake ulisimama kupisha uchaguzi.
“Mchakato wa Mahakama ya Kadhi ulisimama kwa sababu baadhi ya watu ambao tulikuwa nao katika mazungumzo walikuwa wanagombea,” alisema Mufti Simba.

“Kilichobaki ni kuweka mfumo mzuri ambao utaendesha mahakama hiyo. Kwa hiyo siku chache zijazo majopo yote mawili yatarudi mezani kumalizia mchakato na hatimaye mahakama ianze kufanya kazi.”
Hata hivyo, mufti Simba alisema kuwa Waislaamu hudai mambo yao kistaarabu na kwamba hakuna haja ya kuweka shinikizo kwa maandamano, migomo na mabango.

Kuhusu mapumziko siku ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislaamu, Mufti Simba alisema tayari wameshaiandikia serikali kuomba jambo hilo kama ilivyo kwa sherehe za maadhimisho ya miaka mingine.
Aliwataka Waislaamu kuijali siku hiyo na kufanya maadhimisho mbalimbali katika ngazi ya taifa, kanda, mkoa, wilaya, kata na hata msikiti, ikiiwa ni pamoja na kupamba nyumba zao na sehemu zao za kazi kuashiria sherehe hizo
.

“Ili serikali iweze kutusikia na kutufikiria, lazima sisi wenyewe tuonekane tunaihitaji hiyo siku. Ombi tayari tumelifikisha serikalini na tunaamini serikali italishughulikia,” alisema Mufti Simba.
Mufti alisema mapumziko katika sikukuu ya mwaka mpya wa Kiislaam yangekuwapo, lakini kulikuwa na makosa mwanzoni.
“Miaka ya nyuma; wazee wetu kabla sisi hatujaja, waliulizwa wataje sikukuu za Waislaam, wakasema ni Idd Kubwa na Idd ndogo pamoja na siku ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W). Wakaisahau siku ya mwaka mpya wa kiislaamu,” alibainisha Mufti Simba.

Mufti aliwata Waislaamu kuingia katika mwaka mpya wa 1432 ambao ulianza jana kwa kuwajibika katika kujitafutia maendeleo na sio kutegemea wafadhili katika kila jambo.
Aliwataka Waislaam kuhama kutoka katika maovu na kuhamia katika kufanya mema na kushiriki katika kazi za ujenzi wa taifa.

Aliwaombea dua viongozi wa nchi, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Makamu wake na baraza lote la mawaziri na kuwataka kuihamisha Tanzania kutoka katika hali iliyopo sasa ya kiuchumi na kuipeleka kwenye maendeleo mazuri.

Source: mwananchi.co.tz


No comments: