Thursday, February 28, 2008

Je! Ni Sahihi kwa Mkristo Kujihusiha na Mazoezi ya Viungo au Kushiriki Michezo?

Shalom watu wa Mungu!

Kwa sababu ni fani yangu, nimeonelea leo niwashirikishe umuhimu wa mazoezi ya viungo kwa mwili wa binadamu. Naandika haya kwa makusudi kamili nikijua kwamba wengi hasa wa jamii ya waaminio wa ki-Tanzania huona ni kama kupoa kiroho kwa mpendwa kushiriki katika mazoezi ya viungo, kucheza mpira, riadha, kuogelea, na michezo mingineyo inayohusisha mjongeo wa viungo vya mwili (body movements). Biblia inaeleza katika kitabu cha 1Timotheo 4:8 "... Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote..." Huo mstari unaweka bayana kwamba mazoezi yanafaa japo ni kwa kiwango fulani-HAUKATAZI mazoezi ya mwili.Kwa kuonesha kwamba mazoezi ni muhimu na hata wakati fulani kushiriki kwenye mashindano ya michezo, Paul anasisitiza kwa kutolea mfano 1 Wakorintho 9:24-27 "... Je! Hamjui ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja?..." Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote ........" Paul anajiringanisha kama mwanariadha mahali hapo." Anaonesha pia kwamba katika michezo zipo sheria zake na kanuni za kufuata ili kuweza kufikia lengo (2 Timothy 2:5). Kana kwamba haitoshi, Paul anaonesha pia hata michezo ya kukabiliana ana kwa ana (combat sports) kwamba nae yupo katika kupiga ngumi na si kama apigaye hewa (2 Timothy 4:7).


Kwa vielelezo hivyo ni dhahiri kabisa hakuna dhambi ndani yake kwa mtu wa Mungu kushiriki kwenye michezo au mazoezi ya mwili cha msingi ni kuwa na dhamiri na nia njema ya kwa nini unafanya hivyo. Ni agizo la Mungu kwamba hekalu lake litunzwe hii sio kiroho tu hata katika utu wa nje ni muhimu pia (1 Corinthians 6:19-20). Efeso 5:29 - yazungumzia juu ya matunzo ya mwili, pia Biblia inakataza ulafi naam hata inafikia hatua ya kusema ujitie kisu kooni kama wewe ni mlafi Mithali 23:2, kuwa makini hapa!!! Kwa ujumla twaweza sema biblia inakazia juu ya suala la mtu kuitunza afya ya mwili wake.


Kwa mtazamo huo hapo juu, nikirejea kwenye umuhimu wa michezo au mazoezi ya mwili, ziko faida lukuki ndani yake. Tafiti nyingi zimefanyika na karibu zote zinaonesha mtazamo chanya juu ya umuhimu wa michezo na mazoezi kwa mwili wa mwanadamu. Michezo au mazoezi ya mwili yana faida zifuatazo:


1. Hupunguza uwezekano wa kupatwa na magonja ya moyo na kifo kutokana na magonja hayo.

2. Hupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu

3. Hupunguza mafuta yaliyo hatari kwa mwili wako katika damu (blood cholesterol and triglycerides) na kuachilia yale yaliyo salama tu (HDL - or good cholesterol).

4. Hupunguza uwezekano wa kupatwa na mgandamizo mkubwa wa damu (HBP) na kushusha kwa wale walio nao tayari (hypertension)

5. Hupunguza uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa kisukari (Diabetes mellitus type 2DM)

6. Inapunguza uwezekano wa kupata kansa ya utumbo mpana

7. Husaidia katika kufikia na kutunza kiwango cha uzito maridhawa wa mwili.

8. Hupunguza hisia za mtindio wa mawazo na tashwishwi

9. Huimarisha hali njema ya kisaikolojia na kupunguza hisia za msongo

10. Hujenga na kuimarisha mifupa, viungo na misuli za mwili

11. Hupunguza na ama kuondoa tatizo la unene (Obesity)

12. Kwa wazee huwafanya kuwa imara na uwezo wa kudhibiti miili yao kutokana na kuanguka au kuchoka kwa haraka.


Kwa faida hizo na nyingine nyingi ambazo sijazitaja upo uwezekano kabisa wa mtu wa Mungu kuongeza siku zako za kuishi hapa duniani ambayo kwa hakika ni ahadi ya Mungu, na hakuwa mjinga anaposema "...siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na bwana Mungu wako..." (Kutoka 20:12). Wengi wetu kwa kutokushiriki katika mazoezi japo kidogo tumeiharibu miili yetu na kuwa na vitambi visivyokuwa na sababu na miili ambayo ni goigoi ambayo hata imekua kizingiti kwa kazi ya Mungu. Ni kweli yapo magonjwa lakini si yote ni shetani, mengine ni uzembe wetu tu wenyewe (Hosea 4:6).


Kanisa ambalo kimsingi ni eneo la kuwajenga watu kiimani na kuwasogeza kwa Mungu limesahau na kuiweka nyuma habari ya mafundisho ya mazoezi ya miili kwa washirika wake. Eneo hili likitumika vema, laweza hata kuwa ni eneo la injili ya kuwaleta watu kwa Yesu! Fikiria umeanzisha timu ya mpira iko daraja la kwanza, na slogan au moto wenu unakuwa Yesu Ni Mwokozi kila muingiapo uwanjani, unafikiri ni watu wangapi watakuwa wamefikiwa na ujumbe huu kwa msimu mmoja tu wa ligi? au kanisa likiwa na ukumbi wa kufanyia mazoezi Gymn au likianzisha aerobic fitness centre ni watu wangapi watakuwa wakihudumiwa hapo kwa mazoezi hayo na pia kuipata injili kwani hazitapigwa nyimbo za duniani bali ni nyimbo za kumtukuza Yesu na hata ikibidi kabla na baada ya mazoezi mwaweza weka utaratibu wa kuwa na maombi. Yote haya ni katika kuujenga mwili na ufalme wa Mungu! Yatosha kwa leo!!!!!


Mbarikiwe na Yesu!

Chalukulu John Bilinzozi, Norwegian School Of Sport Science And Physical Education - Oslo, Norway. E-mail: chalu.john@gmail.com

2 comments:

Anonymous said...

Mungu akubariki sana,mazoezi ni kitu muhimu sana ktk maisha,nimeipenda sana ths blog na uifanikishe zaidi ya hapa

Anonymous said...

Tatizo wapendwa wengi huwa tunadania kuwa mazoezi ni dhambi.jamani watumishi hebu tuanze mazoezi.tufuate ushauri wa kaka Chalukulu.
asante kaka chalu, nimeipenda hii blog kwa kweli