Saturday, June 7, 2008

KAMA HIZI HABARI NI KWELI, BASI NDANI YA WALOKOLE KUNA MBWA MWITU WAKALI SANA!

Mchungaji na wanakwaya kortini!
MCHUNGAJI na wanakwaya wanane wa Kanisa la Assemblies of God la Kimara, Dar es Salaam, wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha kwa mashtaka ya kula njama za kuiibia Benki ya Barclays tawi la hapa Sh milioni 120.
Wakisomewa mashitaka na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Shami Dunia mbele ya Hakimu Mkazi Mary Mrio wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, ilidaiwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Februari mosi mwaka huu.
Alidai washtakiwa hao wakiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Bukombe Development Association ya Dar es Salaam na mkazi mmoja wa Arusha, Februari mosi mwaka huu waliidanganya Barclays tawi la Sopa Arusha na kujipatia Sh milioni 120.
Mwendesha mashtaka huyo alimtaja Mchungaji huyo kuwa ni Wiliamson Nsekela (45) mkazi wa Kimara Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kampuni ya Bukombe Development Association, Manyala John (33), mkazi wa Dar es Salaam.
Aliwataja wanakwaya hao kuwa ni Lupakisyo Mkumbwa (39), Hawa Chifoto (30), Rehema Mwaifunda (35) na Mariamu Mbunda (34), wote wakazi wa Kimara, Dar es Salaam.
Wengine ni Dennis Mwangomo (24) mkazi wa Mabibo Dar es Salaam, Martin Mwakipesile (30) wa Mwananyamala na mkewe aitwaye Mariam Mwakipesile. Aliwataja wengine kuwa ni Michael Mura (26) mkazi wa Tabata Dar es Salaam na Rashid Hamis (26) ambaye ni mkazi wa Ngarenaro Arusha.
Mwendesha mashtaka alidai Mchungaji Nsekela kwa kushirikiana na Manyala walikula njama kwa kuwaahidi wanakwaya hao kuwapatia kazi katika machimbo ya madini ya tanzanite, Mererani Manyara.
Alidai waliwatengenezea vitambulisho vya kampuni hiyo na kuwataka watoe vitambulisho vya kupigia kura kwa ajili ya kufunguliwa akaunti katika Benki ya Barclays kwamba watakuwa wakichukua mishahara katika benki hiyo.
Dunia alidai Manyala na Nsekela baada ya kupata vitambulisho hivyo kutoka kwa wakwaya na kutengeneza vingine vya kampuni hiyo walikwenda Arusha na kufungua akaunti na kutokana na Benki ya Barclays kutoa mikopo kwa wafanyakazi wa Taasisi za Serikali na nyinginezo, watuhumiwa waliomba mikopo kila mtuhumiwa akiomba Sh milioni 10.
Alidai kwa vile benki hiyo haikuwa na hakika ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa kampuni iliyodai inafanya kazi za huduma ndani ya migodi ipo Dar es Salaam na akaunti zimefunguliwa Arusha.
Hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha, Mary Mrio aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 26 itakapotajwa tena na watuhumiwa walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kila mtuhumiwa kutoa Sh milioni mbili na mdhamini mmoja.
Polisi pia inamshikilia Meneja Mauzo wa Benki hiyo wa tawi la TFA, Jackline Sandawe na Prosper Kasenega wa Makao Makuu ya benki hiyo, kwa tuhuma za kushirikiana na watuhumiwa kufungua akaunti na kutofuata taratibu.

Source: HabariLeo, J'mosi, June 7, 2008.

3 comments:

Anonymous said...

VIPI KUHUSU ASKOFU NA BINTI YAKE MISS CHANG'OMBE?

Anonymous said...

aisee hii mbona aibu jamani.

Anonymous said...

WATUMISHI WA MUNGU TUNAONESHA MFANO GANI KWA WALE WASIOMJUA MUNGU?
KWELI MWAITEGE ALIKUA HALALI KUSEMA MTANITAMBUAJE......
TUBADILIKE ILI TUWEZE KUIBADILISHS DUNIA