Mbunge anaswa akifanya tambiko bungeni Dodoma
*Alisindikizwa na kigogo wa Bunge
*Spika akiri kupokea taarifa hizo
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE na Afisa mmoja Mwandamizi wa Bunge wamekutwa ndani ya Ukumbi wa Bunge wakifanya vitu vinavyodhaniwa kuwa ni vya kishirikina.
Taarifa zilizopatikana mwanzoni mwa wiki hii na kuthibitishwa na ofisi za Bunge, inadaiwa mbunge huyo alifanya tambiko hilo Jumatatu, kabla ya mkutano wa Bunge la Bajeti kuanza Jumanne wiki hii.
Shuhuda aliieleza Mwananchi kwamba, mbunge huyo aliingia kwenye ukumbi huo akiwa ameongozana na katibu mmoja wa bunge (jina tunalo) na kuanza kupita kila kiti cha mbunge na hatimaye aliishia kiti cha Spika.
Aliongeza kuwa, watu hao wakiwa wamefuatana walikuwa wakipita kila kiti huku mbunge huyo akinyunyiza vitu vinavyohisiwa kuwa dawa za kienyeji katika viti vya wabunge.
"Alipofika kwenye kiti cha Spika, alisimama muda mrefu akiwa ananyunyizia vitu fulani, lakini sikujua ni nini na wao waliamini kamera zote zilikuwa zimefungwa," alidai shuhuda huyo.
Shuhuda huyo alidai kuwa, mbunge huyo na mtumishi wa bunge walifanya shughuli yao bila kufahamu iwapo walikuwa wakionekana, bila kujua kuwa kulikuwa kuna watu wanafanya majaribio ya kunasa sauti na picha za ukumbini.
"Walianza kwa kusimama nje kwa muda mrefu wakiwa na wabunge wengine, baada ya wabunge kuondoka, mbunge huyo alibaki na katibu na kuingia ukumbini na kuanza kufanya kazi zao," alidai.
Alipoulizwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, iwapo ana taarifa hizo jana, alisema amezipata na kueleza kushangazwa kwake iwapo bado kuna watu wanaoamini mambo ya ushirikina.
"Taarifa ninazo ila siamini, isipokuwa inashangaza kuona kama bado kuna watu wanaamini mambo hayo kwenye dunia ya leo," alisema Sitta.
Sitta alisema baada ya kupata taarifa hizo, Katibu wa Bunge ameanzisha uchunguzi wa suala hilo. Hata hivyo alisema ushirikina hauwezi kusimama badala ya ukweli na haki.
Wakati huo huo, jana alasiri uvumi ulienea mjini hapa kuwa Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe alikuwa amefariki dunia.
Dk Mwakyembe ambaye juzi hali ilibadilika ghafla akiwa bungeni, alieleza Mwananchi kuwa afya yake ilikuwa imeimarika na kushangaa lengo la watu wanaoeneza uvumi huo.
Baada ya Dk Mwakyembe kukimbizwa kliniki juzi, baadhi ya wabunge walianza kuhusisha tukio hilo na 'tambiko' hilo lililofanyika Jumatatu, huku wengine wakiapa kutokubali hali hiyo kuendelea.
"Hawa watu na washindwe kwa Jina la Yesu. Wanataka kutuulia mtu bure na matambiko yao, Mungu yupo atasimama kati, ukweli utashinda," alisema mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Mbunge huyo ndiye aliyeoongoza Kamati ya Bunge ya Kuchunguza Mchakato waUshindi wa Zabuni ya Kuzalisha Umeme wa Dharura kwa Kampuni ya Richmond Development.
Watu mbalimbali nchini walikuwa wakipiga simu mjini Dodoma kuuliza ukweli wa taarifa hizo, lakini wote walikuwa wakijibiwa kwamba hakuna kitu cha aina hiyo.
Kaimu Katibu wa Bunge alikanusha kuhusiana na uvumi wa kifo cha mbunge huyo na akasema Dk Mwakyembe ana afya njema na kwamba jana alizungumza naye akiwa na pamoja Spika wa Bunge Samuel Sitta ambaye aliwaaga jana kwenda safarini Dar es Salaam.
Alisema kuwa ni kweli walipata taarifa za kuzidiwa kiafya hali iliyomfanya akimbizwe kituo cha afya cha karibu ambako alipumzishwa kwa muda kabla ya kuruhusiwa siku hiyo hiyo.
Alisema kuwa hivi sasa afya ya mbunge huyo ni njeama na haina mashaka ya aina yoyote yaliyosababisha watu kadhaa kupata hofu.
Source:Mwananchi.
Wapendwa,TOO MUCH!
hapa ndio tunaona umuhimu wa kuwa na wabunge na viongozi waliookoka.Pia tunaona umuhimu wa kuwaombea wanasiasa na viongozi kwa ujumla.
Tusimwachie shetani nchi, tushike zamu zetu.
Bwana awajaze nguvu.
Frank Lema
http://www.lema.or.tz/
No comments:
Post a Comment