Friday, October 8, 2010

"Kufunga na kuomba"

"Kufunga na kuomba"
Mathayo 17:21 "Jinsi hii haitoki, isipokuwa kwa kufunga na kuomba"

Bwana Yesu asifiwe!

Ninaamini kuwa wewe unaendelea vyema sana na Mungu ameendelea kuwa mpaji,mponyaji,mlinzi na mtetezi wako, nawe unaweza kusema kuwa "Mtetezi wangu yu hai"(Ayubu 19:25)

Kuna ndugu mmoja,mshirika mwenzetu katika Huduma hii,aliniandikia email siku kadhaa zilizopita akanieleza kuwa anataka kufanya maombi ya kufunga, na akaomba nimwelekeze aombaje hayo maombi. Katika kumjibu, nikaona itakuwa baraka zaidi nikikutumia na wewe pia somo hili, nikiamini kuwa linaweza kuwa baraka kwako pia. Kama ni hivyo, karibu.

Kufunga na kuomba.

Sisi tunaomwamini Kristo, maombi ya kufunga ni maombi ambayo tunayafanya kwa muda tutakaoongozwa na Roho Mtakatifu, huku tukijinyima baadhi ya vitu ambavyo tunavipenda hii ikiwa ni ishara ya kuonesha kuwa tunakitaka kile tunachokiomba zaidi sana kuliko vile vitu tuvipendavyo, ndiyo maana tumeamua kuviacha ili tumwombe Mungu kile ambacho tunamwomba. Kwa lugha nyingine, hunenwa kuwa ni kuutesa au kuusulubisha mwili wetu ili uitii roho yetu kufanya kile ambacho kimeamriwa na Mungu, kwa maana, mara nyingi miili yetu hupingana sana na makusudi ya Mungu katika maisha yetu, ndiyo kama Bwana Yesu alivyosema, "roho i radhi, ila mwili ni dhaifu".

Kufunga kunaweza kufanywa kwa kukifanya kitendo chochote ambacho unajua kitautesa/kuusulubisha mwili wako ili kuutiisha katika mapenzi ya Mungu, huku wewe ukiomba. Angalia nabii Danieli alichofanya, anasema "Sikula mkate mzuri, wala nyama, wala sikunya divai, wala sikujipakaa mafuta, hata wiki tatu zilipopita" (Daniel 10:3, tafsiri yangu kutoka KJV Bible), kwake Daniel, hayo ndiyo mambo ambayo aliona akiyafanya, yatautesa mwili wake mbele za Bwana. Wakati wa Agano la Kale na wakati Yesu akiwa hapa duniani, watu wengi wakiwamo wafalme na hata viongozi wa dini walikuwa wakifunga huku wakiwa wamejichafua miilii yao kwa kujipaka majivu na mavumbi.

Sasa hebu yatafakari maneno haya ya Bwana Yesu kwa wanafunzi wake, alipowaambia, "Jinsi hii haitoki, isipokuwa kwa kufunga na kuomba"(Mathayo 17:21). Bwana Yesu aliongea maneno haya kwa wanafunzi wake baada ya wanafunzi wake kushindwa kumkemea pepo hadi atoke. Waliposhindwa kumkemea pepo, Yesu alikuja,akamkemea yule pepo na pepo akatoka mara moja. Wanafunzi wake walipoyaona hayo, walifanya vyema, kwani walimfuata Yesu faragha, wakamuuliza "ni kwanini tulishindwa kumtoa pepo?" Ndipo Yesu akawajibu na kuwaambia; "Yesu akawajibu, "Kwa sababu ya imani yenu haba. Nawaambieni kweli, kama tu mkiwa na imani, hata iwe ndogo kama mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu: `Toka hapa uende pale,` nao utakwenda. Hakuna chochote ambacho hakingewezekana kwenu, ila jinsi hii haitoki ila kwa kufunga na kuomba". Unaweza ukaona ni namna gani Bwana Yesu alisisitiza sana kufunga na kuomba.

Katika kipindi chetu, tumezoea kufanya maombi ya kufunga kwa kuunyima mwili wetu chakula kabisa kwa kipindi tutakachoamua huku tukiomba. Hiyo ni ishara kuwa, tunakithamini zaidi kile tunachokiomba kuliko chakula cha kuulisha mwili.Maombi ya kufunga yanaonesha "priorities" zetu, kwamba tunampenda Mungu zaidi kuliko tunavyopenda chakula au vitu vingine tuvipendavyo.

Hebu tuangalie maelekezo aliyoyatoa Bwana Yesu kuhusu kufunga na kuomba.Yatafakari maneno haya yake Bwana Yesu:"Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni hakika, hao wamekwisha pata tuzo lao. Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako, ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika atakutuza.(Mathayo 6:16-18).Na hayo basi ndiyo maelekezo ya Bwana wetu kuhusu kufunga na kuomba, utakapofanya maombi ya kufunga, usijioneshe kwa watu kuwa umefunga, wala usiwatangazie watu kuwa umefunga ili wakusifu, Baba yetu, yaani Mungu huyaona yaliyo sirini, hivyo anajua kuwa umefunga na umefunga kwa sababu gani.

Watu kadhaa katika Biblia walifanya maombi ya kufunga, kama vile Musa aliyefunga siku arobaini na zaidi sana, Bwana Yesu aliyefunga siku arobaini(Mathayo 4:2), Esta na Wayahudi siku tatu (Esta 4:3,16),Daniel na kadhalika.

Unaweza kufunga kwa kuamua kuacha kula kwa kipindi utakachoongozwa na Roho Mtakatifu ndani ya moyo wako. Kwa mfano, unaweza kuamua kuwa utafunga kuanzia asubuhi hadi saa 12 jioni (yaani hutakunywa kifungua kinywa, wala chakula mchana,wala chakula chochote hadi saa 12 jioni) au unaweza kufunga kwa kipindi kirefu zaidi ya hapo. Utamwambia Mungu kwamba "Leo ninafanya maombi ya kufunga, sitakula chakula chochote hadi itakapofika saa 12 jioni, kwa ajili ya kukuomba kuhusu jambo hili...." Hilo linakuwa ni patano lako na Mungu.

Namna ya kuomba:

Ninakuomba uangalie mfano mmoja wa namna wana wa Israeli walivyofunga na kumwomba Mungu. Wao walikuwa wanaomba toba kwa Mungu. Soma katika Biblia, Nehemia sura ya 9 na utaona namna walivyoigawanya siku yao. Walitumia robo ya siku kulisoma Neno la Mungu (Neh9:3),na kisha wakaanza kuomba toba kwa kuzitubu dhambi zao kwa Mungu kwa uwazi sana.

Ninachotaka kusisitiza, mara nyingi watu huamua kufanya maombi ya kufunga, na wakaamua kutokula chochote kwa kipindi fulani, lakini mambo mbalimbali ya dunia hii yakawasonga na wakajikuta wamejinyima kula lakini hawakupata muda wa kuomba wala kulisoma Neno la Mungu. Hivyo basi, utakapoamua kufanya maombi ya namna hii, hakikisha kuwa unatenga muda wa kutosha wa kulisoma Neno la Mungu sana na pia muda wa kutosha kumwomba Mungu kwa uhuru kama walivyofanya wana wa Israeli, kumbuka siyo kufunga tuu, bali ni kufunga na kuomba, both of them. Na, usisahau yale maelekezo ya Bwana Yesu kwenye Mathayo 6:16-18 kuhusu maombi ya kufunga na kuomba.

Roho Mtakatifu ajuaye kuyafafanua maneno ya Mungu kwa ufasaha wote akufundishe zaidi na zaidi.

Tuombe....

"Ee Bwana Yesu, asante kwa kunipenda sana hata kufa na kufufuka kwa ajili yangu. Asante kwa kunifundisha somo hili kuhusu kufunga na kuomba. Ninakuomba unipe Roho wako Mtakatifu, na Yeye Roho Mtakatifu anifundishe zaidi na zaidi kuhusu somo hili. Ninaomba unisaidie ili na mimi niweze kuomba na kufunga. Jitukuze sana katika Huduma hii ili wengi wakujue na kuja kwako. Asante Bwana Yesu, Amen"

Amani ikae Israel,
Frank Lema,
www.lema.or.tz
savedlema2 at Yahoo dot com
October 6th, 2010,
Arusha, Tanzania.

2 comments:

Anonymous said...

Asante sana kwa somo hili, nina imani kwa yoyote aliyelisoma na kulielewa basi Mungu atakwenda kutenda kazi sawasawa na mapenzi yake. Jina la Bwana lihimidiwe!

Anonymous said...

Asante sana kwa somo hili kwani nilitoka kumpigia mchungaji akanijibu ila pia nikakutana nalo humu kwa uweza wa mungu, ubarikiwe sana na mungu akuzidishie. Amen.