Tuesday, October 12, 2010

Suala la mzee wa upako lachukua sura ingine

TUKIO la hivi karibuni la kuvamiwa kwa Mchungaji wa Kanisa la Maombezi Utashinda, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako (pichani) na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi limechukuwa sura mpya baada ya watumishi wawili wa Mungu kuhojiwa.

Waliohojiwa katika tuhuma hizo nzito za kuvamiwa kwa Mzee wa Upako na kuibiwa mamilioni ya shilingi ni Askofu David Mwasota na Mchungaji Frank Chacha ambao wanatoa huduma kwenye kanisa la Naioth Gospel Assembly lililopo Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam.

Vyanzo vyetu vya habari vilidai kwamba Mchungaji David Mwasota alikamatwa na polisi na kuhojiwa kwa zaidi ya saa 6 katika Kituo cha Mbezi jijini Dar es Salaam kuhusiana na tukio hilo na kutakiwa kumfikisha katika kituo hicho Mchungaji wake Frank Chacha.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, inadaiwa kuwa mara baada ya Askofu Mwasota kumfikisha kituoni hapo, Mchungaji Chacha alihojiwa kwa siku mbili mfululizo bila kupata dhamana kwa madai kwamba kama angeachiwa haraka angevuruga upelelezi wa polisi.

“Baada ya Askofu Mwasota kumfikisha Chacha kituoni hapo, Mchungaji huyo alishikiliwa kwa muda wa siku mbili akihojiwa,” kimoja cha chanzo chetu ambacho tunakihifadhi jina lake kilisema.

Iliendelea kudaiwa kwamba Mzee wa Upako alihisi kuwa Mchungaji Chacha alihusika na tukio hilo kutokana na ujumbe mfupi wa maneno (SMS) aliomtumia, hivyo akaamua kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

Inadaiwa kwamba ujumbe uliotumwa kwenda kwa Mzee wa Upako ulikuwa ni wa kumpa pole kuhusiana na tukio la kuvamiwa na majambazi kisha kuporwa mamilioni ya pesa usiku wa kuamkia Septemba 27, mwaka huu.

Hata hivyo, vyanzo hivyo vilisema kwamba ujumbe aliotumiwa Lusekelo haukuwa na nia mbaya ila aliutilia mashaka kwa kuwa ulimuuliza kama alimkosea Mungu kutokana na kukumbwa na balaa hilo.

“Hilo la kuambiwa kwamba amemkosea Mungu ndilo lililomfanya mtumishi huyo kuona kama vile alikuwa akifanyiwa dhihaka katika tukio hilo la kuibiwa pesa,” kilidai chanzo chetu.

Inadaiwa kuwa Mzee wa Upako alishindwa kuelewa maana ya ujumbe huo na kuhisi kufanyiwa dhihaka na mtumishi mwenzake Chacha ambaye hakuwa na lengo baya.

Aidha, chanzo hicho kilisema kwamba hii ni mara ya pili kwa Mzee wa Upako kumtuhumu Mchungaji Chacha ambaye zamani alikuwa anatoa huduma katika kanisa lake kabla ya kutokea hali ya kutoelewana ambapo alihamia kwa mlezi wake Askofu Mwasota.

“Inawezekana ana bifu na Mchungaji Chacha kutokana na kuondoka katika huduma yake ndiyo maana ameamua kufanya hivyo, ni jambo la kusikitisha watumishi kupelekana polisi na haya siyo maadili ya kitumishi kabisa,” kiliendelea kusema chanzo hicho.

Kwa upande wa Askofu Mwasota alisema kwamba baada ya kutoka kituoni kesho yake (Jumanne) alimfuata Mchungaji Chacha na kumpeleka Kituo cha Polisi Mbezi ambapo alikaa kwa muda wa siku mbili ndipo alimtoa kwa dhamana.

“Mzee wa Upako ni mwanangu na sijagombana naye na sina matatizo naye, ila sijui kwa yeye na Mchungaji Chacha wana matatizo gani kwa sababu walikuwa watu wa karibu, nitaongea naye vizuri nijue tofauti zao,” alisema Askofu Mwasota.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Elias Kalinga alipopigiwa simu siku ya Jumapili kuzungumzia sakata hilo alisema bado analifuatilia na tulipomtafuta kabla ya gazeti hili kuingia mitamboni simu zake zote hazikupatikana.

No comments: