Friday, October 22, 2010

SIKU YA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 31, 2010 TUMUUNGE MKONO ASKOFU KAKOBE

Ndugu Mhariri,
Kauli ya askofu Zachary Kakobe ya kuyataka makanisa yote ya FGBF nchini kutokuwa na ibada siku ya uchaguzi mkuu, jumapili ya oktoba 31,2010 na badala yake ibada hiyo kufanyika jumamosi ya oktoba 30,2010 ni ya kuungwa mkono na kupigiwa mfano na wadau wote wanaoutakia mema uchaguzi mkuu, mwaka huu.
Madhali jitihada za maaskofu kuishawishi serikali kufikiria upya kuhusu siku ya uchaguzi mkuu kubadilishwa zimegonga ukuta mwaka huu, basi ni vyema kwa maaskofu hao, kuwa na utaratibu mbadala kwa mwaka huu wa kuwaruhusu wapiga kura kutoka makanisa yao ili wawe huru kuchagua viongozi wao siku hiyo ya jumapili na badala yake ibada zifanyike siku ya jumamosi, nadhani hili litakuwa jema na mbadala wa ombi lililowasilishwa serikalini.
Zipo faida kadhaa kwa maaskofu kuwaruhusu watanzania wenye sifa kwenda kupiga kura siku hiyo ya jumapili na kutokuwa na shughuli nyingine za ibada siku hiyo;
Mosi,Ni haki ya kikatiba kwa mtanzania aliyetimiza sifa husika kuchagua kiongozi wake au hata kuchaguliwa kuwa kiongozi.
Pili,Wagombea walio halali, waadilifu na wacha Mungu watachaguliwa kutokana na kura halali za watanzania walioamua kuacha kwenda kusali na kufanya utumishi huo wa kupiga kura!
Tatu,Kwa kuwa mafisadi hawawezi kuondolewa na mafisadi, basi ni vema na haki watanzania wema na wacha Mungu, wakawakatae mafisadi kwa nguvu ya sanduku la kura!Siku hiyo ya jumapili na si vinginevyo.
Vilevile kwa kuwa sauti ya wengi ni sauti ya Mungu,wengi watakaojitokeza kumchagua mgombea yeyote atakayepita, basi hapo litakuwa ni chaguo la Mungu kwelikweli.Hakuna mantiki ya mtu ambae hakupiga kura halafu eti analalama kuwa "mbunge wetu huyu hatufai, tangu achaguliwe hatujamuona jimboni".Hicho ni sawa na kilio cha samaki, machozi kubebwa na maji!Ni muhimu basi kupiga kura ili tuwe na hakika wa yule tunayempenda kuwa mbunge, raisi au diwani wetu.Hivyo natoa wito watanzania, jumapili tuitoe kama sadaka kwa Mungu kwa kwenda vituoni asubuhi na mapema, tupige kura ili tulete mabadiliko katika nchi yetu iliyobarikiwa.
Ndugu maaskofu, tukiamua kufanya ibada siku ya jumamosi, siku moja kabla ya uchaguzi mkuu, itatupa fursa pia ya kuuombea uchaguzi mkuu kwa pamoja kama watanzania, tukimsihi Mungu atupe vingozi walio bora na aliowakusudia yeye mwenyewe. lakini kwa kuwa Mungu hatokuja kupiga kura mwenyewe na malaika wake, anawataka watakatifu wote walio bora hapa duniani, wakatumie hekima yake (Mungu) kuwachagua viongozi walio bora vilevile.
Hizo ni baadhi ya faida chache nilizoziona kwa watanzania kuamua kufanya ibada siku ya jumamosi badala ya siku ya jumapili ya uchaguzi mkuu, oktoba31, 2010.Hivyo basi natoa wito kwa maaskofu wetu kuunga mkono uamuzi wa askofu Kakobe wa kuhamishia ibada siku ya jumamosi badala ya jumapili.
Nikimalizia hoja hii, kuchagua viongozi katika jamii yetu ya kitanzania ni utumishi mkubwa kwa Mungu vilevile.Tukiomba Mungu atupatie viongozi bora lakini sisi wenyewe waombaji hatupigi kura,tutakuwa tukisaliti majibu ya maombi yetu kila mara uchaguzi unapowadia.Haya shime watanzania tuamke,tukapige kura siku hiyo ya jumapili ya Uchaguzi Mkuu.Bwana Mungu na atubariki sote.
Modercai JP Siulapwa,(Sauti ya Nyika)
Po Box 15864,
Dar Es Salaam.
Phone:0719 654416/0754216761

No comments: