MSANII aliyejipatia umaarufu kupitia nyimbo za asili za Kihaya, Saida Karoli anadaiwa kusakwa kwa udi na mvumba na Kanisa la Assemblies of God lililopo Boko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Risasi Jumamosi limetonywa.
Mtoa habari wetu ambaye ni muumini wa kanisa hilo aliyeomba hifadhi ya jina lake alidai kwamba, kusakwa kwa Saida kunakuja kufuatia uamuzi wake wa kwenda kufanyiwa maombi lakini baada ya zoezi hilo akaingia mitini.
Muumini huyo alidai kuwa, awali msanii huyo alifika kanisani hapo kwa lengo la kutubu dhambi zake na kumrejea Mungu, lakini baada ya kuombewa na mambo yake kumnyookea alianza kuwa mwenye mahudhurio mazuri kiasi cha waumini wengine kuhisi angekuja kuwa mfano kwa wengine.
“Alifika hapa na kufanyiwa maombi, akawa mhudhuriaji mzuri lakini ghafla alikata mguu bila kujulikana sababu.
“Tunamshangaa sana kwani pamoja na kutubu dhambi zake na kuokolewa, hajatulia kwenye imani yake. Kwa kweli tunamsaka ili arudi amtumikie Yesu, aachane na mambo ya ulimwengu,” alisema muumini huyo.
Baada ya kupata taarifa hiyo, gazeti hili lilimtafuta mchungaji wa kanisa hilo aliyefahamika kwa jina moja la Semtomvu, alipopatikana alikiri ‘kumpaka upako’ Saida lakini akaonesha kushangaa jinsi msanii huyo ‘alivyomtoka’.
“Ni kweli nilimbatiza Saida, alikuja hapa akaniambia anaumwa na anahitaji uokovu ili amtumikie Bwana Yesu, lakini nashangaa baada ya kumbatiza na kulitumikia kanisa kwa muda sijamuona tena,” alisema Mchungaji huyo.
Aliongeza kwamba bado wanamsaka msanii huyo ili aendelee kuwa mtumishi na popote alipo ajue Bwana Yesu anamhitaji, achane na mambo ya dunia.
Alipotafutwa Saida kuzungumzia suala la kusakwa na kanisa hilo alisema kwamba kwasasa yeye yuko Mwanza hivyo ni vigumu kwenda kuabudu kanisani ila kama kanisa hilo lina tawi lake huko atakwenda, kama hakuna wasimtafute
Source: Globalpublisherstz.info
No comments:
Post a Comment