Friday, October 29, 2010

Tuepuke kuhamasisha udini katika kipindi hiki cha uchaguzi

WAKATI zikiwa zimebaki takribani siku chache ili kufikia siku maalumu kwa Watanzania ya kupiga kura Oktoba 31, mwaka huu, joto la kampeni linazidi kupanda huku yakitokea matukio na malumbano kadhaa ambayo kwa kweli hayapendezi.

Malumbano hayo ambayo mengi yanatokana na ushabiki wa wahusika kutoka kwa mgombea mmoja kwenda mwingine sasa yanaanza kubadili upepo na kugusa eneo nyeti la dini ambalo iwapo yataachiwa yazidi kuendelea yanaweza kuharibu kabisa desturi ya Watanzania iliyodumu kwa miaka mingi.

Hivi karibuni yamekuwapo malalamiko ya baadhi ya viongozi wa dini kudaiwa kutumia majukwaa ya nyumba zao za dini kuzungumzia siasa lakini baya zaidi kumwaga sera na kuwaombea kura wagombea wanayemtaka hali ambayo ni kinyume kabisa na kazi za viongozi hao.

Malalamiko hayo ambayo sasa yanaanza kuwa malumbano yamewekewa msingi na tamko la mashehe na maimamu la jana ambalo lilitoa karipio la wazi na kuwatuhumu baadhi ya viongozi wa dini ya kikristo kuwa wamekuwa wakitumia majukwaa kuhamasisha kiongozi wanayemtaka ndiye achaguliwe katika uchaguzi wa mwaka huu.

Ukweli ni kwamba sitaki kuegemea upande wowote wala kuhoji nani mkweli na nani muongo jambo la msingi hapa ni kwa hawa viongozi wetu wa dini kuanza kuingiza siasa kwenye dini, hali ambayo inaweza kuwagawa Watanzania.

Kazi kubwa ya viongozi wetu wa dini sote tunaifahamu pamoja na kutufundisha na kutuelekeza kutumia njia ya Mwenyezi Mungu na kuepuka kutenda dhambi lakini pia wana wajibu wa kuhakikisha kuwa jamii wanayoiongoza kwa misingi ya dini inafuata maadili lakini pia kuitahadharisha na viongozi wasio waadilifu bila kuegemea upande wowote.

Hivyo basi katika wakati huu muhimu wa uchaguzi kila Mtanzania ana wakati mgumu wa kusikiliza sera, kutafakari na hatimaye kuchagua kiongozi ambaye anaona anafaa, hivyo iwapo vyombo vya dini vitatumika kumpigia debe mgombea yeyote ni wazi kuwa ni rahisi kumshawishi mtu kumchagua kiongozi huyo kutokana na imani ya dini.

Kutokana na ukweli huo, ni vyema na muhimu kwa viongozi wa dini kuacha kutumia nyumba za dini kama majukwaa ya siasa na kutupiana lawama katika kipindi hiki, na badala yake kila mmoja kwa wakati wake na wajibu alionao atumie fursa hiyo kutoa elimu ya uraia na ya uchaguzi kwa waumini wake kutokana na ukweli kuwa kwa sasa bado Watanzania wengi hawana elimu hiyo.

Huu si wakati wa kutumia dini kama kigezo cha kumpigia debe mtu au sehemu ya kuanzisha migogoro ambayo hapo baadaye inaweza kuleta mpasuko, tushirikiane kwa pamoja kama watanzania katika kipindi hiki ili kuhakikisha kuwa baada ya uchaguzi, kunakuwa na viongozi wenye sifa, waadilifu ambao wataleta mabadiliko katika nchi hii.

Hivyo basi viongozi wa dini katika muda uliobaki wana wajibu wa kutumia nafasi waliyonayo kuwaelimisha waumini wao umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na kupiga kura na namna ya kumtambua kiongozi bora kwa vigezo vya sifa na uwezo bila kuegemea chama au mgombea.

Source:http://www.habarileo.co.tz/uchambuzi/?n=10714

No comments: