POLISI Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam jana ulizuia kufanyika kwa ibada kwenye kanisa la Moravian Jimbo la Misheni ya Mashariki Tabata ili kuepusha uvunjifu wa amani.
Kikosi cha polisi kiliongozwa na maofisa wa polisi akiwamo Mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo, Duwani Nyanda.
Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kuwapo kwa
mgogoro ambao kwa siku ya jana ungesababisha vurugu kutokana na upande
mmoja wa uongozi wa kanisa hilo kutaka kusimikwa kwa nguvu huku upande
mwingine ukikataa.
Wakati huohuo Umoja wa Kanisa la Moravian duniani
umeukana uongozi mpya uliotangazwa na Mchungaji Clement Fumbo
aliyesimamishwa kuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Misheni Mashariki kwa madai
kuwa umekiuka sheria na katiba za kanisa hilo.
Awali Mchungaji Fumbo alikuwa akipita katika
makanisa akitangaza kuwa Umoja wa Kanisa Duniani (Unity Board)
unamtambua na kwamba umemruhusu yeye aendelee na uongozi ikiwa ni pamoja
na kuchagua halmashauri mpya jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati
akitoa maelekezo kwa wachungaji, Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Jimbo
la Kusini, Clement Mwaitebele alisema amepokea barua kutoka kwa
Mchungaji Dk Jorgen Boytler ikikataa kitendo cha Mchungaji Fumbo
kujitwalia madaraka kinyume na katiba.
“Baada ya Mchungaji Fumbo kujichagulia halmashauri
yake niliamua kuutaarifu uongozi wa ngazi za juu za kanisa duniani ili
kuomba ushauri, ambao nao ulimkana kwa madai kuwa kanisa hilo
linaendeshwa kwa kanuni na katiba,” alisema Mchungaji Mwaitebele.
Aliongeza kuwa sehemu ya barua hiyo kutoka kwa
Boytler ilisema “Nimepata taarifa kuwa ndugu zetu wa Dar es Salaam
wamechagua uongozi mpya wakieleza kuwa ndiyo Halmashauri Kuu mpya ya
Jimbo la Misheni Mashariki, uamuzi huu ni wazi kuwa umekiuka katiba na
miongozo yote ya majimbo yetu,” ilisema.
Naye Katibu Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania,
Conrad Nguvumali alikemea vikali hatua hiyo ya Mchungaji Fumbo akisema
kuwa ni uasi na usaliti wa hali ya juu na kwamba lazima wachungaji
waheshimu uamuzi wa Sinodi.
Source:Mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment