Thursday, January 10, 2013

Tuombe kwa Jina la Yesu

Tuombe kwa Jina la Yesu (6)
Sadaka yako na Maombi yako.
"Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu." (Mdo 10:4)
Bwana Yesu Asifiwe!

Ninaamini kuwa ujumbe huu umekukuta hujambo kabisa na unauona na kuufurahia ukuu wa Mungu katika maisha yako wewe na ya wale wanaokuzunguka, kwa maana maandiko yasema kuwa "Furaha ya Bwana ndiyo nguvu zetu". Mimi binafsi ninapenda kumshukuru Mungu kwa kuwa mwema sana kwangu na kunitendea mambo kwa fadhili kuu mno.

Kwa majuma kadhaa sasa tumekuwa tukijifunza somo hili lenye kichwa "Tuombe kwa Jina la Yesu", lengo la somo hili lilikuwa na kujenga msingi imara wa maombi kwa watu wote wanaotamani kujenga zaidi maisha yao ya maombi mbele za Mungu wetu mwema. Kwa wale mliojiunga na Huduma  hii hivi karibuni, tazama mwisho kabisa wa email hii utaona sehemu ya  kusoma masomo ya siku za nyuma. Pia tembelea www.thekingdomnews.org kwa maelezo zaidi. Leo tunaendelea na sehemu ya tano ya somo hili, Roho Mtakatifu wa Mungu akufundishe upata kulifahamu Neno la Mungu.

Sadaka yako na Maombi yako.
Leo tutajifunza uhusiano kati ya maombi yetu kwa Mungu na sadaka zetu kwa Mungu Baba. Kwa ajili ya kujifunza vyema somo hili, hebu ifikirie mistari hii ya Biblia; "Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.  Akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, Mimi ni BWANA, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi."(Mwanzo 15:4-7).

Katika maandiko ya mistari hiyo, tunaona Mungu akimpa Ibrahimu (baba yetu wa imani) ahadi kubwa sana katika maisha yake. Alimwahidi kuwa watoto wake watakuwa kama nyota za mbinguni. Na ahadi hii imetimia hata sasa yaonekana. Nami nataka tutazame Ibarahimu alifanya nini baada ya kusikia ahadi hii kwa Mungu? Kitendo cha Ibrahimu kupewa ahadi hiyo na Mungu, ni sawa kabisa na wewe kusoma Biblia na Roho Mtakatifu wa Mungu kukuonesha Neno ambalo lina ahadi fulani kwa ajili yako.

Ibrahimu aliposikia Mungu akimpa ahadi hiyo, alitaka uthibitisho kutoka kwa Mungu kuonesha kwamba kweli ahadi hiyo Mungu aliyoisema itatokea kwake. Tunaona katika mstari wa nane Ibrahimu akimwambia Mungu: "Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? " (Mwanzo 15:8), kwa swali hilo, Ibarahimu alimtaka Mungu athibitishe kama anachokisema ni kweli kitatokea kwa Ibrahimu ambaye alikuwa hana hata mtoto mmoja kwa wakati huo. Naye Mungu akamjibu na kumwambia "Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. (Mwanzo 15:9). Katika mistari hiyo, tunaona kuwa Ibrahimu alitaka uthibitisho juu ya Neno la Mungu kutukia katika maisha yake, na Mungu akamwambia amtolee sadaka (mstari wa 9), na katika mistari inayofuata ya sura hii ya Mwanzo 15, tunaona kuwa Ibrahimu alimtolea Mungu sadaka zake na Mungu alizikubali sadaka hizo, na kweli kile Mungu alichomwahidi Ibrahimu kimetokea, kwa sababu hata wewe kama umeokoka basi wewe ni wa uzao wa Ibrahimu kwa imani.

Mfano mwingine wa mtu aliyeunganisha maombi yake na sadaka zake ni askari aliyeitwa Kornelio, ambaye tunasoma habari zake katika Matendo 10:3-4 "Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu." Na ukisoma zaidi utaona kuwa Mungu alimpelekea msaada yeye na familia yake yote.

Habari hiyo tuliyoisoma inatufundisha kwa uwazi kabisa kuwa kuna nafasi/sehemu ya sadaka katika maombi yetu tunayoyapeleka kwa Mungu. Kwamba unapopata Neno katika Biblia au Mungu amekwambia Neno fulani kwa njia yoyote, ikiwa unatamani Neno hilo litimie katika maisha yako, basi fanya kama alivyofanya Ibrahimu. Chukua sadaka yako, nenda nayo kwa Mungu na uzungumze naye ukimweleza kuwa kama Ibrahimu alivyomtolea sadaka katika Mwanzo 15, na wewe pia unamtolea Mungu sadaka yako ili hili jambo ambalo unaamini amekuahidi lipate kutimia. Lakini ni muhiimu kujua kuwa sadaka/pesa hainunui majibu ya maombi yako kwa Mungu.

Hivyo basi, ni vyema ukapanga mkakati wako wa maombi, kwa mfano unaweza ukapanga kuwa na maombi fulani kwa muda wa wiki nzima. Andika maombi yako kwenye karatasi na weka ndani ya bahasha. Humo mwenye bahasha pia weka sadaka yako ambayo unapenda moyoni mwako kuambatanisha pamoja na mahitaji yako. Kisha, kila siku unapomwomba Mungu unakuwa umeshika ile bahasha yenye maombi na sadaka yako, huku ukiomba kwa bidii na kumwambia Mungu kuwa pia unaambatanisha maombi yako hayo na sadaka yako kwake.

Namwomba Roho Mtakatifu aendelee kulipanua hili somo moyoni mwako kwa utukufu wa Mungu Baba. Na kama somo hili limekusaidia ninaamini uta-forward kwa rafiki zako pia ili nao wabarikiwe, na usisite kuwakaribisha kwenye Kanisa la Mtandaoni.

Tuombe....

"Mungu Baba, ninakuja kwako kwa Damu ya Yesu Kristo. Ninaomba unisamehe kila nilipokukosea, na unipe Roho wako Mtakatifu anisaidie nibadilike. Baba, asante kwa Neno lako litialo uzima, asante kwa kunifundisha namna ya kuambatanisha maombi yangu na sadaka yangu kwako. Ninaomba unisaidie niweze kuliweka somo hili katika matendo. Asante kwa ajili ya mtumishi wako na Huduma hii, ninaomba mapenzi yako yaendelee kufanyika zaidi. Nimeomba haya kwa Jina la Yesu Kristo, Amen"


Tuzidi kuombeana ili kazi hii ya Injili isonge mbele na Mungu atukuzwe kwa ajili ya hiyo.

Mungu karibu ufanye makao yako Tanzania;
Frank Lema,
Kanisa la Mtandaoni,
The Kingdom News,
www.thekingdomnews.org
thekingdomnews@yahoo.com
August 22, 2012
Arusha, Tanzania.

No comments: