Thursday, January 10, 2013

WAFAHAMU AMISH

WAFAHAMU AMISH
HISTORIA YAO
Kikundi cha Amish kiliundwa huko ulaya na Jacob Amman mnamo miaka ya 1644-1720 kikiwa ni sehemu ya kanisa la Mennonite lililogawanyika. Dhamira ya kikundi hiki ilikuwa ni kujaribu kurudisha tamaduni, mila na desturi za mwanzo za kanisa la Mennonite ambazo zilionekana kutaka kupotea.  Mpaka sasa hakuna mwafaka uliofikiwa kuhusu kikundi hiki na kwamba kipo katika mrengo upi katika imani ya wakristo.  Baadhi ya watu wanawachukulia kama waprotestant wa kihafidhina (wasiopenda mabadiliko).  Wengine wanawafananisha na baadhi ya makanisa huru ya ulaya yanayofanana na kanisa la Mennonite.
Mila, desturi na tamaduni za kikundi hiki ziliandikwa na mwanzilishi wake Menno Simons (1496-1561) na kufikia mwaka 1632 imani ya Amish ilikuwa imeshaandikwa.  Amish wengi waliogawanyika kutoka kanisa la Mennonite waliishi kusini mwa jimbo la Rhine huko Switzerland. Katika karne ya 17 kundi hili liligawanyika tena kutokana na kile kinachoaminiwa ni kukosekana kwa nidhamu miongoni mwao.
Jinsi Amish wanavyotumia magari ya kukokotwa na farasi katika kusafiri
Kutokana na kugawanyika huko baadhi yao walihamia nchini Marekani katika jimbo la Pennsylvania, New York, Illinois, Indiana, Iowa, Missouri Ohio, pamoja na majimbo mengine mwanzoni mwa Karne ya kumi na nane (18). Kundi hili lilijaribu sana kutunza chembechembe za imani iliyokuwepo nchi za ulaya katika karne ya kumi na saba (17).  Walijaribu kuzuia maendeleo ya kisasa yaliyokuwa yameanza kujitokeza kwa kuanzisha mila, tamaduni na desturi zilizojitenga na zile za Marekani zilizokuwa zinakua kwa kasi.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo kama James Hoorman wanasema, Nchini marekani Amish wana litrujia moja kubwa lakini kadri miaka inavyozaidi kwenda mbele litrujia hiyo inazidi kubadilika miongoni mwao.  Kwasasa Amish wamegawanyika katika makundi makubwa manne, ambayo ni; Swartzengruber, Old Order, Andy Weaver, na New Order Amish. Makundi haya yote yanafanya kazi tofauti huku yakitofautiana kwa namana wanavyoishi kulingana na imani yao.  The Swartzengruber Amish ni wahafidhina (Wasiopenda mabadiliko) wakubwa katika imani hiyo huku wakifuatiwa na Old Order Amish ambalo ndilo kundi maarufu. The Andy Weaver wameendela kwa namna fulani lakini New Order Amish ndiyo waliondelea zaidi kupita wote.
IMANI YAO

Amish ni kikundi cha watu wanaofuata mafundisho ya Jacob Ammann (Mwanzilishi wa kikundi hiki), raia wa Switzerland aliyeishi katika karne ya kumi na saba (17).  Ni moja kati ya madhehebu ya wakristo wa kiprotestant likifanana sana na kanisa na Mennonite.   KWwasasa wengi wao wanaishi nchini Marekani wakifuata tamaduni za kawaida zinazojumuisha kukataa kula kiapo mahakamani ama sehemu nyingine ile itakayokulazimu kula kiapo, kutokupiga kura ama kufanya shughuli za kijeshi.  Hawakubaliani kabisa na technolojia mpya na ya kisasa zinazotumika katika maisha ya kila siku ya mwanaadamu.  Usafiri unaotumiwa na watu hawa ni magari ya kukokotwa na farasi.
Mavazi ya mwanamke wa Amesh. Hayaruhusiwi kuwa na urembo ni lazima yawe plain

Moja kati mstari wa maandiko unaoaminiwa sana na Amish katika imani yao ni kitabu cha Yakobo 1:27 (
Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa).  Kwa tafsiri yao kujilinda na dunia pasipo mawaa ni kukaa mbali kabisa na vitu ambavyo ulimwengu unafanya  kwa mfano  kuendesha magari, kuangalia runinga, kwenda kwenye majumba ya sinema, kujipamba kwa kuvaa hereni na mapambo yafananayo na hayo. Mbali na hayo watu hawa hawakai katika nyumba za umeme na wala hawatumii simu.  Mambo haya yote na mengineyo yafananayo na hayo kwa tafsiri yao ni mambo ya kidunia yanayokatazwa katika andiko hilo la kitabu cha Yakobo.
Ili kupata nguvu ya kuendesha vifaa mbalimbali vinavyohitaji nguvu ya ziada ili viweze kufanya kazi watu hawa hutumia majenerator pamoja na magari ya farasi kama mbadala wa matreka kwa kazi za mashambani.   Upo utaratibu wa namna ya kuvaa kwa wanawake na wanaume, mavazi yao wanatengeneza wenyewe na wanaume hawanyoi nywele wala ndevu.  Askofu ndiye kiongozi wa kanisa lililogawanyika katika makundi yanayoitwa district, utaratibu wa namna ya kufanya ibada huwekwa na kiongozi huyo.  Ibada hufanywa kila jumapili kama makanisa mengine, lakini wao hawana makanisa kwa maana ya jengo bali ibada hizo hufanyika katika nyumba zao.
Namna ya farasi wanavyotumika katika shughuli za kilimo na Amish
Yapo baadhi ya matatizo katika kundi hili kama yalivyo madhehebu mengine ya dini lakini mara zote matatizo hutatuliwa ndani ya kundi pasipo kuruhusu kutoka nje. Kwa Marekani watoto wa kundi hili wanaruhusiwa kwenda shule za kawaida mpaka pale wanapotimiza umri wa miaka kumi na mitano tu. Vijana wanapokuwa wadogo wanapewa fursa ya kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine ili waamue kama wataambatana na imani hii ama la. Kutokana na hilo vijana wengi wa Amish wamejikuta wakijihusisha na utumiaji wa madawa  ya kulevya, matumizi ya pombe, mahusiano ya kingono na mambo mengine mengi yanayofanywa na vijana katika umri huu huku wakiruhusiwa kuendesha magari, baadae wengi wao huamua kuachana na maisha hayo ya kidunia na kujiunga na kanisa.
Ukitazama katika maisha yao ya kiroho, Amish ni sawa kabisa na Wayahudi wa asili ambao mpaka leo wanafuata mafundisho ya sheria za agano la kale.  Katika hili wana listi ndefu ya mambo wanayoruhusiwa kuyafanya na yale wasioruhusiwa kuyafanya.  Kwa ujumla endapo utashindwa kufuata sheria na taratibu hizo basi utakuwa katika hatari ya kuadhibiwa na kanisa kwa namna ya kutengwa kanisani.
Namna Amish wanavyotumia magari yanayokokotwa na farasi kwa shughuli za kilimo
Amish wanaami kwamba YESU KRISTO ni mwana wa Mungu, ambaye alikufa kwa dhambi zetu, na YEYE ndiye njia ya wokovu. Kila wanachokifanya katika maisha yao ni lazima kiwe na uhusiano na Mungu. Wanaiona kazi yao kuwa ni njema na ni upendeleo wa pekee kutoka kwa BWANA.  Ikiwa kazi yao njema itaweza kufunika na kutowesha mambo mabaya basi wanaamini kwamba BWANA atawapa uzima wa milele mbinguni.  Kwa ajumla watu hawa ni wazuri, wachapa kazi wanaohakikisha wanasimama katika njia sawa ya Mungu ili baadae wapate taji la uzima wa milele.  Wanaamini kwamba Amish ni namana ya kuishi na sio dini. Wamechagua kuishi maisha ya kawaida ili watumie muda mwingi nyumbani na familia zao, badala ya kwenda kwenye mambo yaliyoendea na yanayotumia technolojia ya kisasa.
Hivi ndivyo wanaume wanavyovaa na hawaruhusiwi kunyoa nywele wala kukata ndevu
Kama kundi watu hawa hawaamini katika ulinzi wa wokovu, wanaamini mtu anaweza  kupoteza wokovu wake ikiwa mtu huyo atajitenga na Mungu kwa kufanya mambo yaliyo kinyume NAYE.  Hawaamini katika ubatizo wa watoto wadogo lakini pia hawaamini ubatizo wa maji mengi.  Baadhi yao wanaamini kwamba YESU KRISTO alilipa deni la dhambi zetu  na hivyo wamepokea neema ya wokovu.  Lakini wengine wanaamini kwamba wokovu wao unatokana na matendo yao kwa kujiweka pembeni na mambo ya ulimwengu. 
Ukitazama kwa undani maisha wanayoishi watu hawa ni namna wanavyojaribu kujitenga kabisa na ulimwengu huu. Lakini ni vyema tukafahamu kwamba hatuwezi kujitenga na watu wengine kwakuwa maandiko matakatifu yanatuagiza kwenda kuhubiri injili ulimwenguni; ‘’ Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari’’ (Matayo 28:19-20). Hatuwezi kujitenga na ulimwengu kwasababu tumeitwa kuhubiri neno ulimwenguni.  Ni vyema tukatambua na kuamini kwamba tumeokolewa kwa neema na si kwa matendo yetu; ‘’Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu’’ (Tito 3:4-5)Haya ni baadhi tu ya mambo machache sana niliyoweza kuyaeleza kwa leo juu ya imani hii. Yapo mengi sana ambayo nitayaeleza siku za mbeleni kwa lengo la kukuza ufahamu wetu zaidi.

No comments: