Majambazi waliovamia katika Kanisa la Maombezi Utashinda, linaloongozwa na Mchungaji Anthony Lusekelo ‘ Mzee wa Upako’ na kufanikiwa kupora zaidi ya shilingi milioni 20 za sadaka, wamejisalimisha kwa kiongozi huyo wa kiroho, mmoja akiwa katika hali mbaya.
Habari za uhakika zilizodakwa na gazeti hili kutoka katika kanisa hilo zinadai kuwa, baada ya uvamizi huo kufanyika, Mzee wa Upako pamoja na waumini wake walifanya maombi rasmi ya siku saba ambayo yalisababisha watu wawili kujisalimisha kanisani hapo kama kiongozi huyo alivyohubiri, na mmoja kuuawa mjini Morogoro.
Imedaiwa kuwa wiki iliyopita bwana mmoja alifika kanisani hapo huku akilia akiwa mtupu akiomba msamaha kwa Mzee wa Upako, na kueleza jinsi walivyoingia kanisani na kupora kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 20.
Chanzo chetu makini kanisani hapo kilisema kuwa, mtu huyo (jina tunalihifadhi kwa sababu za kiusalama) alifika kanisani hapo akiwa na ndugu zake, akionekana kama alirukwa na akili, japokuwa alikuwa na uwezo wa kusema, hatarudia tena kutenda alichotenda.
“Alikuwa akiomba msamaha na kusema hatarudia tena kuiba, alikuwa akisema hayo huku akiwa mtupu, ndugu na jamaa zake aliofuatana nao walimuomba sana Mzee wa Upako amsamehe,” alisema mtoa habari wetu.
Habari zinasema kuwa, Mzee wa Upako alimuambia kijana huyo pamoja na ujumbe wake kuwa, amemsamehe kwa sababu hata maandiko yanasema msamehe aliyetubu na baadaye watu hao waliondoka kanisani hapo.
Mtoa habari wetu alizidi kuanika kuwa, watu hao na huyo anayetuhumiwa kuiba walikwenda moja kwa moja katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo mgonjwa wao alipokelewa na kulazwa katika wodi ya watu wenye matatizo ya akili.
Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye wodi hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuuliza mtu mwenye jina alilopata kanisani kwa Mzee wa Upako, akathibitishiwa kuwa yupo na amelazwa hapo kutokana na kuonekana ana matatizo ya akili.
“Ni kweli mtu huyo yupo amelazwa hapa, lakini kwa kawaida huwa haturuhusiwi kueleza matatizo ya mgonjwa, huwa tunafanya hivyo kwa ridhaa yake tu, sasa kwa kuwa ni mgonjwa, huwezi hata kumuona kwa mahojiano,” alisema afisa mmoja hospitalini hapo ambaye hakupenda kutaja jina lake.
Aidha, kuna habari kuwa mtu mwingine ambaye naye anadaiwa kuhusika katika wizi huo alifariki mjini Morogoro kwa kupigwa risasi na polisi katika tukio la ujambazi.
Uwazi liliweza kumpata kiongozi wa juu wa kanisa hilo la Maombezi Utashinda ambaye alizungumza na Mwandishi Wetu kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini na kukiri kutokea kwa tukio hilo.
“Tulifanya maombi maalum madhabahuni ambayo ni sehemu takatifu, ibada inapofanywa sehemu kama hiyo huwa ni lazima matokea yatapatika na ndiyo haya yametokea ya watu wawili kuja kuomba msamaha hapa,” alisema kiongozi huyo.
Aliongeza kuwa, fedha zilizoibiwa siyo za Mzee wa Upako bali zilikuwa ni sadaka ya Mungu, hivyo walioiba walifanya makosa makubwa ambayo baada ya maombi yameitikiwa na Mungu mwenyewe kwa kuwaonesha wakosaji walichokifanya.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema mara baada ya kuvamiwa na majambazi walipata ushirikiano mzuri kutoka kwa polisi chini ya uongozi wa Kamanda wa Kanda Maalum, Suleiman Kova na akawasifu kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kushughulikia tukio hilo.
Hivi karibuni Mzee wa Upako alivamiwa kanisani kwake na majambazi ambao walimnyang’anya mlinzi wake bunduki na kumpora (Lusekelo) shilingi zaidi ya milioni 20 ambazo ni fedha za sadaka za kanisa na gazeti hili kuandika tukio hilo kwa urefu.
Source: Globalpublisherstz.info
1 comment:
http://www.youtube.com/watch?v=wIYUqWteA50&NR=1
Post a Comment