Bwana Yesu asifiwe!
Ninamwamini Mungu kuwa ameendelea kukutendea wema mwingi kuliko unavyostahili katika maeneo mbalimbali ya maisha yako, na utukufu wote tunampa Yeye. Tumebakisha siku chache kabla ya kuumaliza mwaka 2010, basi na tusiache kumshukuru Mungu kwa mwaka mzima huu.
Tunamshukuru sana Mungu kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Tanzaniauliofanyika hapa tarehe 31 October 2010 kwa kuwa sote tulishuhudia kuwa ulikwenda kwa amani tofauti na hofu iliyokuwa imejengwa kwa watu wengi. Najua kulikuwa na kasoro kadhaa, lakini bado twapaswa sana kumshukuru Mungu. Kwa kuwa tulimwomba Mungu kwa ajili ya Uchaguzi, basi tuendelee kumtegemea Yeye, naamini hatatuacha tuangamie. Sasa tunakabiliwa na jukumu moja la "kulea mwana", yaani, kuwategemeza kwa maombi wale viongozi waliochaguliwa, pamoja na viti/nafasi zao za uongozi.
Karibu tujifunze sehemu hii ya somo letu, na ninaamini litakubariki tena.
Familia ya Kikristo (3): Huwajali Yatima, Wajane na Masikini
Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo, kwa Jina langu anikaribisha Mimi- Marko 9:37.
Bwana Yesu Asifiwe! Hii ni sehemu ya tatu ya somo hili kuhusu familia ya Kikristo, naamini litakuwa na manufaa kwako sasa au baadaye.
Leo, napenda tuangalie jambo moja ambalo linapaswa kuwa ni mojawapo tuu ya sifa/taratibu nyingi za familia ya Kikristo.
Wakati Familia ya Kikristo inamshukuru Mungu kwa kuwa inafurahia kuishi pamoja nyumbani, kupata muda wa kula pamoja, kwenda Kanisani pamoja, kuomba pamoja nyumbani na kadhalika, ni muhimu sana kukumbuka na kuwa kuna watu wengine wengi sana ambao hawapati kabisa nafasi hiyo pamoja na kuwa wanatamani sana, nao ni watu ambao Yesu Kristo alikufa msalabani kwa ajili yao pia kama Maandiko yasemavyo, "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele" Yohana 3:16.
Tangu wakati wa Agano la Kale, Mungu ameonesha kujali sana maisha ya watu walio katika mazingira magumu kama vile yatima, wajane na masikini. Wakati huo, aliweka sheria kuwa wana wa Israel wakienda kuvuna mazao yao shambani, wasivune na kukusanya yote, bali waache kidogo kwa ajili ya masikini ili waje kuokota baadaye. (Soma Walawi 19:8-10).
Pia Mungu ameonesha upendo wake kwa yatima na wajane sehemu nyingi katika Biblia,akitutaka tusiwatendee mabaya, bali tuwatendee mema.(Soma Kumbukumbu 14:27,Kutoka 22:22 :"Usimdhulumu mjane wala yatima")
Kwa kuwa sisi na familia zetu za Kikristo ni wana wa Mungu, basi hatuna budi kuyafanya kwa vitendo yale ambayo Mungu amekuwa akituagiza katika Neno lake kuhusu kundi hili la Yatima, Wajane na Masikini, na ndiyo msisitizo wa somo la leo. Kila familia ya Kikristo ni vyema sana kuweka maazimio maalumu ya kuwajali watu waliopo kwenye makundi hayo. Hiyo ni Huduma ya kuoonesha upendo wa Yesu kwa wengine, na jambo hilo laleta baraka sana. Hebu tazama Mungu alichosema kuhusu Huduma hizi,"Heri mtu yule anayemjali masikini, BWANA atamwokoa wakati wa shida" Zab 41:1, "Yeye amhurumiaye masikini humkopesha BWANA, naye atamtuza kwa aliyotenda"Mithali 19:20.
Umegundua baraka tele zinazoambatana na huduma hiyo? Kuwajali watu walio katika makundi hayo, kwa mfano watoto yatima kunajumuisha mambo kama vile kuwaombea na kisha kuwatembelea mahali walipo na kuwasaidia katika mambo mbalimbali yanayowahusu na kisha kuwaambia habari njema za upendo wa Yesu kwao. Kwa mfano unaweza kuwatembelea yatima kwenye vituo vinavyowalea, ukaenda na mahitaji yao kiasi chochote kama bidhaa za chakula, ukafika pale ukawasadia kufua nguo zao, ukaongea nao mambo mbalimbali, ukawaombea na kisha ukaondoka. Maandiko yasema kuwa ukifanya hivyo ni sawa na kumkopesha Mungu, atakulipa maradufu.
Tuombe..
Mungu Baba, ninakuja mbele zako kwa Damu ya Yesu. Ninakushukuru kwa ujumbe huu wa Neno lako ambao umenifundisha kuyatenda mapenzi yako. Ninaomba unisamehe kwa kila namna ambayo nimewadharau wajane, yatima na masikini. Ninaomba uniumbie moyo mpya wa kuwapenda na kuwaonesha upendo wako, wapate kujua ya kuwa unawapenda na kuwathamini sana na kuwa wewe Mungu huna upendeleo. Nimeomba haya na kuamini, kwa Jina la Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, Amen"
Ubarikiwe na Bwana Yesu utakapoyatenda maneno ya ujumbe huu.
*Mistari ya Biblia niliyotumia katika somo hili nimeinakili kutoka katika tafsiri ya Biblia inayoitwa "NENO BIBLIA"
Ili Kristo ajulikane sana,
Frank Lema,
savedlema2 at yahoo.com
www.lema.or.tz
Arusha Tanzania,
November 22, 2010.
No comments:
Post a Comment