BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA) limesema Chama Cha Mapinduzi(CCM) na serikali yake havipaswi kulaumiwa juu ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, kwa kuwa vimekwisha toa ridhaa na tayari mchakato wa uundwaji Mahakama hiyo umeanza.
Tamko hili linakuja siku chache baada ya waumini wa waislam nchini kuijia juu CCM kwa madai kuwa imewasaliti kwa kukiuka ahadi yake kupitia Ilani ya Uchaguzi mwaka 2005, kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Shekhe Mkuu wa BAKWATA, Mufti Shaban bin Simba, alisema kimsingi suala la uanzishwaji Mahakama ya Kadhi halina mgogoro tena kwa kuwa tayari serikali imekwisha likubali na uanzishwaji wake uko mbioni kutekelezwa.
Mufti Simba, alisema hatua iliyofikiwa kati ya BAKWATA na Serikali juu ya Mahakama ya Kadhi ni yakuridhisha hivyo kuwataka wananchi pamoja na waislamu wote nchini kuwa na subira na kutawala jazba zao ili kuruhusu kamati iliyoundwa kushughulikia suala hilo, kufanya kazi yake.
"Tayari kamati ya uundwaji wa Mahakama ya Kazi imekwishaanza kufanya kazi, kwa sasa mazungumzo kati ya wanasheria wa serikali na wanasharia wa Kiislamu pamoja Kamati ya Mashekhe kutoka BAKWATA yanaendelea, hoja si kuomba ruhusa ya kuanzisha Mahakama, hoja yao ni namna gani ianzishwe mahakama hiyo," alisema Mufti Simba.
Alisema serikali ya CCM haipaswi kulaumiwa kwa kuwa ilikwisha likubali suala la kuwepo Mahakama ya Kadhi, hivyo hoja kuwa serikali imewasaliti si za kweli, na kuwa maneno hayo yanasemwa na watu ambao hawajaielewa vizuri hoja hiyo kama ilivyofafanuliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Bw. Pius Msekwa.
Aidha, Mufti Simba alisema kutoingizwa kwa suala la Mahakama ya Kadhi katika Ilani ya CCM 2010 - 2015 si tafsiri ya kuwa CCM imelipuuza jambo hilo, bali ni utaratibu wa kuruhusu chama kushughulikia mambo mengine baada ya kumaliza hilo.
"Ninachokijua mimi, CCM haikuwa na haja ya kurudisha suala la Mahakama ya Kadhi katika ilani yake wakati wa uchaguzi ujao, yako mambo mengi yanayopaswa kushughulikiwa na serikali si hili tu, kwa kuwa imekwishalimaliza na kuruhusu tuendelee hakuna haja ya kuliweka katika ilani yake tena," alisema.
Alisema tayari ripoti ya awali ya mchakato wa uanzishwaji Mahakama hiyo imekwishafikishwa mezani kwake na kuwa ameandaa mkutano wa mapitio ya yale yaliyopendekezwa na kuyafanyia marekebisho kitakachofanyika Julai,3 na 4 mwaka huu na kutoa taarifa ya maendeleo ya suala hilo.
Tayari CCM imekwisha tanganza kulipatia ufumbuzi suala hilo baada ya kupokea ushauri kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria, uliotaka suala hilo kuachwa mikononi mwa waumini wa dini ya kiislamu waanzishe kwa misingi ya dini hiyo na si katika mfumo wa mahakama za kawaida.
Source:majira.co.tz
No comments:
Post a Comment