Sunday, July 4, 2010

Mahakama ya kadhi yageuka kaa la moto!

Siku kiduchuu baada ya Waziri wa Sheria na Katiba, Bw. Mathias Chikawe, kutangaza msimamo wa Serikali kutounda Mahakama ya Kadhi, Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) limepinga tamko hilo na kumtaka waziri huyo kufuta kauli yake fastaaa.Akichonga mbele ya wanoko wa minews,Shekhe Mkuu wa Tanzania Mufti Issa bin Shaaban Simba, alimtaka Bw. Chikawe arudi kukusanya maoni kwa watalaamu wa dini hiyo wa nchi mbalimbali ndipo afikie maamuzi."Tumechoka kupotoshwa katika mambo yetu huwezi kumakabidhi Joseph (mtu ambaye si muislam) asimamie Sheria za Kiislam kwani yeye hajui hata maana ya uislam" alisema Mufti Simba huku akiungwa mkono na jopo la Mashekhe kwa kuitikia 'Takbir !'Alisema tamko hilo la Serikali halijawatendea haki waislam na imeonesha wazi kuwa nchi hii ina wenyewe na waislam ni tabaka la pili.Mufti alisema, Serikali isitishike na kauli ya vitisho ya makanisa kuwa haitapigiwa kura katika uchaguzi mkuu wa mwakani kwani nchi hii ni ya wakristo, waislamu na wapagani.Alisema waislam wamevumilia kukandamizwa kwa muda mrefu kwani Mahakama hiyo ilikuwepo na Serikali ndiyo iliyoitoa hivyo isione uzito kuirudisha kwani ziko Mahakama nyingi kama ya Kazi,Bishara Ardhi na Nyumba.Aliendelea kusema Rais Jakaya Kikwete aliwahidi waislam kuwa Bunge litashughulikia suala hilo na kutoa maamuzi yatakayo waridhisha hivyo, Bw. Chikawe asiwachonganishe na Rais."Rais anania njema na waislam lakini Bw. Chikawe na jopo alilosaidiana nalo kufanya maamuzi hayo ndiyo wamepingana na nia ya Rais," alisema Mufti Simba.Alifafanua kuwa mfano aliouchukulia, Bw. Chikawe kufananisha uamuzi wake na utaratibu wa Afrika ya Kusini haufai kwani nchi hiyo ina waislam wachache ukilinganisha na Tanzania.Alishangaa kusikia, Bw.Chikawe alishauriana na wataalamu ambao BAKWATA haiwafahamu wala hawajui utaratibu na sheria za kiislam.Alimtaka waziri huyo na jopo lake kuiga mfano wa nchi za Kenya, Uganda na Zanzibar ambazo tayari zimeishaunda Mahakama hiyo na kwamba Tanzania ina waislam wengi kuliko nchi hizo. Alisema mambo ya kupakana mafuta kwa mgogo wa chupa yamewachosha waislam hivyo amewataka mashekhe wote wa mikoa na wilaya kuunga makono tamko lake.Mmoja wa Shekhe liyehudhuria mkutano huo na kuonekana kuguswa na tamko hilo ni shekhe Issa Ausi ambaye ni Katibu wa Baraza Hilo Wilaya ya Ilala na kueleza kuwa Baraza hilo sasa limeanza kurudi katika mstari na kuwataka waislam wasirudi nyuma kudai haki yao.Alisema waislam wakati wakidai uhuru wakristo walikuwa nyuma wakiwa wamevaa soksi ndefu, hivyo anashangaa kuona sasa ndiyo wanoongoza nchi na wasilam wakiwa nyuma."Serikali ituambie nchi hii inaongozwa na wakristo pekee ambao hawakuwepo wakati tunadai uhuru mwaka ule tumehangaika sana sisi, leo hii wao ndiyo wasemaji wa serikali" alisema kwa hamaki Shekhe Ausi.Mashekhe hao wameunda tume ya watu watatu ambao ni Shekhe Issa Ausi, Mohamed Mhenga na Haji Magubika itakayokwenda leo Dodoma kuonana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ili kufikisha tamko hilo.

Source: darhotwire.com

No comments: