Monday, July 5, 2010

Masheikh wasusia ripoti mahakama ya kadhi

RIPOTI ya kwanza kuhusu mapendekezo ya sekretarieti ya pamoja kati ya wataalamu wa serikali na wa kiislaam, juu ya mfumo na uendeshaji wa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara, imekwaa 'kisiki'.Hatua hiyo imekuja baada ya jopo la masheikh 25, likiongozwa na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Issa bin Shaaban Simba, kuikataa kwa maelezo kuwa ina mapungufu.Hivi karibuni Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mufti Simba kwa nyakati tofauti, waliwaambia waandishi wa habari kuwa Mahakama ya Kadhi, iko jikoni na kwamba muda si mrefu, itaiva.
Viongozi hao waliwasihi Waislaam kote nchini, wasiwe na wasi wasi.Hata hivyo juzi Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislaam (T) na Shura ya Maimamu, yalisema kupitia katika tamko yao kwamba hawataikubali mahakama itakayoundwa, ikiwa haitatambuliwa kikatiba na kutengewa bajeti na serikali.Kufuatia kauli hizo na ile ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoweka bayana kwamba haitaiingiza tena hoja ya Mahakama ya Kadhi katika ilani yake ya uchaguzi wa mwaka 2010/15, jopo la masheikh lilitisha kikao cha siku mbili chini ya Mufti Simba, kujadili ripoti ya kwanza ya mapendekezo ya mfumo na uendeshaji wa mahakama hiyo.Kikao hicho kilichoanza Julai 3 na kumalizika Julai 4 mwaka huu, kilijadili kipengele kwa kipengele ripoti hiyo na kugundua kuwa ilikuwa na mapungufu makubwa kuhusu mambo muhimu ya mahakama hiyo inayoliliwa na Waislaam kwa miaka 20 sasa.Akizungumza na waandishi wa habari Katika Makao Makuu ya Bakwata jijini Dar es Salaam jana, mufti Simba, alisema jopo limebaini kuwa, kuna mambo muhimu yanayohitaji kujadiliwa tena kati ya serikali na Waislamu."Jopo limekaa na kujadili kipengele kwa kipengele na kuona kwamba bodo kuna mambo muhimu ambayo yanahitaji kukaa tena na serikali ili kufikia mwafaka," alisema mufti Simba.Mufti Simba alisema mambo hayo yanahusu mfumo wa uendeshwaji wa mahakama na kwamba , jopo halikukubaliana na mfumo uliopendekezwa katika ripoti hiyo."Kwanza ni vipi mahakama ya kadhi itakuwa na uwezo wa kisheria na kikatiba wa kutoa maamuzi yake, pili ni vipi mahakama itaingizwa katika mfumo wa mahakama uliopo nchini na namna ya kugharamia uendeshwaji wake,"alisema mufti Simba.Hata hivyo Mufti Simba ambaye ni msemaji wa jopo hilo la kufuatilia mchakato wa urejeshwaji wa Mahakama ya Kadhi Tanzania bara, aliwataka Waislaam na watu wa madhehebu mengine nchini,kuwa watulivu."Tunaomba Waislaam na wananchi wote kwa jumla kuwa, watulivu kwa kuwa jambo hili ni zito na linahitaji umakini wa hali ya juu katika kufikia mwafaka," alisema.Alisema jopo limepokea mapendekezo yaliyofikiwa kati ya Sekretarieti ya Serikali na Waislaam, kuhusu namna ya kuunda na kuendesha mahakama hiyo. .Alisema kikao hicho kimepata mahudhurio mazuri kwa kuhudhuriwa na wajumbe wote 25 kutoka taasisi na madhehebu mbalimbali ya kiislaam pamoja na wanasheria (mawakili).Aliwataja wajumbe kuwa ni, masheikh Issa bin Shaaban Simba (Mwenyekiti), Salum Hassan Fereji (Bakwata), Ally Muhidini Mkoyogore (Bakwata), Ismail Makusanya (Bakwata), Shaban Rashid (Bakwata), Abdillahi Mnyasi (Bakwata) na Abubakar Zubeir (Salafia).Wengine ni masheikh Hamid Jongo (Bakwata), Alhad Mussa Salum (Bakwata), Muhammed Jalal Sharif (Daawatil Islaamiyya), Ramadhan Lakha (Sunni), Mussa Kundecha (Baraza Kuu), Suleiman Kilemile (Masjid Thaqafa), Muharrami Dogga (Alharamain) na Twaha Selemani Bane (Alharamain).Masheikh wengine ni, Juma Omar Porri (Answar Sunna), Abdallah Bawazir (Qiblatain), Twalib Ahmad Abdallah (Masjid Maamur), Abdallah Ndauga (I.I.R.O), Said el-Maamriy (wakili), Issa Maige (wakili), Yahya Njama (wakili), Mohammed Khamis Said (Bakwata), Abdallah Matumla (Mwanasheria Bakwata) na Suleiman Lolila (Bakwata).Hata hivyo Mufti Simba alisema hana uhakika kama serikali itaendelea kulitekeleza la mahakama ya kadhi baada ya uchaguzi iwapo halikumalizika kwa sasa.
Source: Mwananchi.co.tz

No comments: