Monday, July 5, 2010

Mwizi arejesha simu kanisani kwa kuhofia adhabu

MTU mmoja aliyesadikiwa kuiba simu mbili katika Kanisa la Waadventista Wasabato la Magomeni, jijini Dar es Salaam, juzi alilazimika kujisalimisha kwa uongozi wa kanisa hilo kwa kuzirejesha simu hizo akiogopa adhabu kali kutoka kwa Mungu.Mwizi huyo ambaye hata hivyo jina lake halikuweza kufahamika mara moja, alifanya hivyo baada ya kiongozi mmoja wa kanisa hilo, John Odera, kumtaka arejeshe simu hizo kabla ya kukutana na mkono wa Mungu.Mzee Odera alitoa tangazo la kupotea kwa simu hizo na kumtaka aliyezichukua kuzirejesha."Kuna mwenzetu mmoja amekuja kusali akijua kuwa wote wanaokuja hapa, wanakuja kwa lengo la kusali na wote ni watakatifu. Hivyo akaacha simu zake mbili hapo akaenda chooni lakini alipotoka hakuzikuta, anajaribu kuzipiga hazipatikani yaani zimezimwa," alisema mzee Odera.Mzee huyo wa kanisa la alimuomba mtu aliyechukua simu hizo azirejeshe katika ofisi ya wazee wa kanisa hilo au amkabidhi shemasi yeyote na kwamba kama ataamua kuondoka nazo, basi atakutana na mkono wa Mungu.Baada ya kumaliza tangazo hilo, mzee Odera aliondoka na kupisha taratibu nyingine kuendelea.Hata hivyo muda mfupi kabla ya mhubiri kusimama, wakati akitoa utambulisho wa waliokuwa wametoa huduma na ambao walikuwa wanatarajia kuendelea kutoa huduma katika ibada hiyo, mwenyekiti wa program hizo aliwatangazia waumini kuwa simu hizo zimepatikana."Habari njema, habari njema ni kwamba zile simu zilizotangazwa hapa kuibwa tayari zimepatika," alisema mwenyekiti huyo na kusabisha waumini kushangilia kwa furaha.Hata hivyo Mwananchi lilipoutafuta uongozi wa kanisa ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusu tukio hilo haukuweza kutoa maelezo.

Source: Mwananchi

No comments: