SIKU chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza kuliondoa suala la Mahakama ya Kadhi katika ilani yake, wabunge wamehoji uhalali wa serikali kushindwa kulimaliza suala hilo kama ilivyoahidi.Hatua hiyo, inakuja kutokana na CCM kuliweka suala hilo, kwenye ilani yake ya uchaguzi mwaka 2005, ikiahidi kulipatia ufumbuzi na mwaka jana Bunge liliambiwa kuwa serikali imeamua kutoanzisha mahakama hiyo na badala yake itaangalia misingi ya dini ya Kiislamu na kuiingiza kwenye sheria za nchi.Uamuzi huo, uliitingisha nchi baada ya viongozi na wanaharakati wa dini hiyo, kucharuka wakipinga uamuzi huo, lakini Waziri Mkuu Mizengo Pindi alikutana na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu na kulituliza kwa kukubaliana kuunda tume ya kufuatilia suala hilo.Lakini jana Bungeni katika maswali ya papo kwa papo, Mbunge wa Mkanyageni (CUF) Habibu Mnyaa alilifufua suala hilo na kumtaka Waziri Mkuu Pinda aeleze kwa nini serikali imeshindwa kulimaliza suala hilo.Kufuatia swali hilo, Pinda alirudia kauli yake na kusema serikali haijakata tamaa katika kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kwamba ipo katika mchakato wa mwisho wa makubaliano ya jinsi ya kuunda mfumo utakaokubalika kwa pande zote mbili katika kuiendesha mahakama hiyo.“Hakuna jambo lisilokuwa na mwisho wake, na kila jambo ni lazima lizingatie mazingira na ndio maana serikali bado haijakata tamaa na italimaliza pasipo kusababisha malalamiko kutoka katika madhehebu mengine ya dini,” alisema Pinda.Pinda alifafanua serikali haitaki kujihusisha moja kwa moja katika suala hilo kutokana na kuwa ni sehemu ya ibada ya dini ya Kiislamu, na kwamba serikali inaheshimu imani ya kila mtu.Mnyaa alimtaka Pinda alieleze Bunge kama CCM italiweka suala hilo au la katika ilani yake ya 2010/15.“Sasa katika hili mimi sijui nikueleze nini, maana wewe ni mpinzani, lakini lililokubwa ni kuheshimu imani ya kila dhehebu,” alisema PindaWakati hayo yakitokea Bungeni jana, juzi Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilisitisha maandamano yaliyotakiwa kufanyika leo yaliondaliwa na Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (Bahakita) kuwahamamsisha waislamu kutoipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu mwaka huuWaislamu wanadai CCM iliwadanganya mwaka 2005 katika suala la kuanzishi mahakama hiyo.Sheikh Mkuu Issa Shaaban Simba, ambaye ni Mwenyekiti wa jopo la masheikh 25 wanaowawakilisha Waislaam katika mazungumzo na kamati maalum ya serikali kuhusu kuanzishwa kwa mahakama hiyo , amewataka waumini wa dini hiyo, kuondoa hofu na kwamba jambo hilo litamalizwa karibuni.Mufti Simba alilazimika kutoa kauli hiyo, baada ya CCM kuamua kuondoa suala la Mahakama ya Kadhi kwenye ilani yake ya mwaka 2010 kwa maelezo kuwa ahadi yake ya mwaka 2005 kuhusu kulitafutia ufumbuzi, imeshatekelezwa.Ahadi hiyo ilitekelezwa baada ya serikali kuamua kufanya utafiti wa misingi ya dini hiyo ili iingizwe kwenye sheria za nchi badala ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi ndani ya mfumo wa mahakama."Hakuna haja ya Waislaam kupapatika, jambo la Mahakama ya Kadhi limeiva na halina tatizo lolote."Jambo hili la kadhi lipo katika mchakato na linaendelea kuzungumzwa kati ya kamati ya masheikh na kamati ya serikali pamoja na wanasheria wa kiislaam na wale wa serikali."Lakini napenda kukipongeza na kukishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuiweka hoja ya Mahakama ya Kadhi katika ilani yake ya uchaguzi ya 2005/10 bila ya kuombwa na baadaye kuiamuru serikali yake kuitekeleza," alisema Mufti huyo.
Source:mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment