Friday, July 30, 2010

House girl' amnyonga mtoto, ajinyonga

MTUMISHI nyumbani kwa mkazi wa Uwanja wa Ndege, Kihonda mkoani Morogoro amemnyonga mtoto wa 'tajiri yake' mwenye umri wa miaka miwili na nusu.
Binti huyo mwenye umri wa miaka 16 alimnyonga mtoto huyo, Seth Steven, jana saa 2.45 usiku na yeye akajinyonga.
Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro,Thobias Andengenye, amesema, mtoto huyo amenyongwa nyumbani kwa, Steven Kapombe, alipokuwa akifanya kazi binti huyo. Kwa mujibu wa Kamanda huyo, msichana aliyemyonga mtoto huyo anaitwa Zaina, na kwamba alikuwa anafanya kazi nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo.
Kwa mujibu wa Andengenye, alitumia kipande cha kanga kumyonga mtoto huyo na alitumia nguo ya aina hiyo kujinyonga. Alisema, chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana na kwamba, polisi wanaendelea kuchunguza.
Wakati huo huo, mkazi wa uwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, Farida Athumani (34), anashikiliwa na polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kutaka kujiua. Msichana huyo alikunywa sumu ya panya jana saa 5 asubuhi, na kwamba, mkazi wa eneo hilo, Ahmed Omary (63), alitoa taarifa Polisi.
Andengenye alisema, polisi wanaendelea kuchunguza tukio hilo na kwamba, msichana huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.

Source: Habari Leo

No comments: