Tuesday, February 5, 2013

Polisi Dar kuchunguza maandamano ya Waislamu

Sheikh Ponda Issa Ponda 
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu azimio la maandamano hayo ya Waislamu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Suleiman Kova


POLISI Dar es Salaam wako kwenye mchakato wa kukusanya taarifa kuhusu maandamano ya waumini wa dini ya Kiislamu, yaliyopangwa kufanyika Februari 15, mwaka huu na kisha itatoa msimamo wake.

Juzi Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ilitangaza msimamo wake wa kufanya maandamano Februari 15, mwaka huu kwa lengo la kushinikiza Katibu wake, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake wawili walioko mahabusu waachiwe kwa dhamana.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Markaz, Chang’ombe Dar es Salaam, Amiri wa Umoja wa Wahadhiri wa Kiislamu aliwataka Waislamu wote kujumuika ili kufanikisha azma yao.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu azimio la maandamano hayo ya Waislamu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Suleiman Kova alisema kuwa wamesikia taarifa hizo na kwamba kwa sasa wanaendelea kukusanya taarifa zaidi na kisha watatoa msimamo.

“Nimezisikia taarifa za wao kutaka kufanya maandamano yenye lengo la kumtetea Shekh Ponda, bado tunaendelea kupokea habari hizi kutoka kwa watu mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari,” alisema Kova.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, baada ya taarifa hizo kukamilika ataitisha mkutano na waandishi wa habari ili umma ujue nini polisi wameamua juu ya maandamano hayo.
“Taarifa zikikamilika tutaitisha mkutano na waandishi habari ili umma ujue tulichokiamua,” alisema Kova.

Sheikh Ponda na Kiongozi wa Jumuiya hiyo,Sheikh Mukadamu Swalehe pamoja na wenzao 48 wanakabiliwa na kesi ya uporaji wa eneo la ardhi la Markaz Chang’ombe Temeke, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Ponda na wenzake kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kuingia na kujimilikisha eneo hilo lisilo mali yao, wizi wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya Sh50 milioni, huku Ponda na Mukadamu wakikabiliwa na kosa lingine la uchochezi.

Hata hivyo washtakiwa wengine katika kesi hiyo wako nje kwa dhamana isipokuwa Ponda na Mukadamu tu ambao dhamana yao imefungwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Source: mwananchi.co.tz

No comments: