Monday, February 11, 2013

UKWELI KUHUSU UZUSHI WA “DA VINCI CODE”

Baada ya kukisoma kwa makini kitabu hiki kilichoandikwa na mwandishi na mtaalmu wa elimu ya dini Dan Brown,aliyejipatia umaarufu mkubwa kwa kueneza uzushi mkubwa duniani kuhusu imani ya kikristo na YESU KRISTO mwenyewe,nimeonelea ni vyema nikauanika uongo huu hadharani ili kila mmoja wetu apate kuutambua uzushi huu.
Uwongo huu unaojizolea umaarufu siku hadi siku sio kitu cha kupuuzwa hata kidogo na ni lazima sisi kama kanisa tusimame na kuupinga kwa kweli zilizopo (facts) bila kuuonea aibu wala kuugopa maadam ukweli upo wazi.Kitabu cha mwandishi Dan Brown kimeuza zaidi ya nakala milioni 40 duniani kote tangu kitoke kwa mara ya kwanza mwaka 2003.Pia f
ilamu iliyotengenezwa huko Hollywood Marekani kutokana na kitabu hicho imeshaonyeshwa karibu duniani kote ikiwemo hapa kwetu Tanzania ambapo hata nakala zake zimeshaanza kusambaa.Unaweza kushangaa kwa nini uwongo huu umepata umaarufu mkubwa kiasi hicho,hii inawezekana kwa sababu wapinzani wa ukristo wapo wengi na ile roho ya mpinga kristo ipo na inafanya kazi,2Wathesolanike 2:1-10;
Nafahamu zipo njia nyingi za kupingana na uwongo huu,ikiwemo njia ya maombi,kuwafundisha wakristo Neno la Mungu kwa usahii na hata kupuuzia huu uwongo ili upotee wenyewe.Lakini hatuwezi kukataa ukweli kuwa lipo kundi la watu ambalo hata mtume Paulo analiita “wenye masikio ya utafiti” ambalo litaendea kuzitafuta filamu hizi na vitabu hivi ili kutaka kujua kilichomo ndani. Nchi nyingi za magharibi watu wengi wamachukuliwa na uwongo huu na hata wengine wametokea kuuamini bila kujua ukweli halisi wa uzushi huu.Mfano msomaji mmoja wa kitabu hiki alikaliliwa akisema kuwa “kuanzia sasa sitaenda tena kanisani ..Sikujua kama ukristo ni hadithi za kutunga….”.
Sasa matokeo kama haya si mambo ya kupu
uzia hata kidogo,kwani history ya kanisa inaonyesha kuwa imani potofu mbalimbali zilizowahi kuibuka duniani zilianza na mawazo ya vikundi vidogo au mtu mmoja na zilipata nguvu kadri siku zilivyoendelea.Na ndio matokeo ya imani nyingi za uwongo tunazoziona leo hapa duniani na waumini wa imani hizo wapo tayari kuzitetea kwa hali na mali kwa kuwa hawakufahamu msingi halisi wa imani zao.Hii imesababisha hata kupishana kwa mafundisho baina ya madhehebu mbalimbali ya kikristo.Yapo madhehebu ya kikristo yasiyoamini kuhusu ROHO mtakatifu,Uungu wa YESU na mambo kadhaa.Kwa hiyo kanisa haliwezi kupuuzia hata kidogo uwongo huu.
Labda kwanza tungeanza kujiuliza hoja alizoanzisha mwandishi Dan Brown kama zinaukweli wowote,

  • Je, YESU alikuwa na ndoa ya siri na Mariam Magdalena?
  • Ni kweli Uungu wa YESU ulianzishwa na kutungwa na mtawala wa kirumi Constantino na Kanisa?
  • Ni kweli Constantino alitumia umaarufu na ushawishi wa YESU kutunga Uungu wa YESU?
  • Je vitabu vya agano la kale tunavyotumia siku za leo vilichaguliwa na Constantino?
  • Je kumbukumbu za kwanza kuhusu maisha ya YESU ziliteketezwa ili kuuficha ukweli?
  • Je, maandiko ya kale yaliyogunduliwa hivi karibu pamoja na injili za wagnostika (Gnostic gospel) yanatueleza ukweli kuhusu YESU?
Hayo ni madai makuu ya msingi yaliyomo kwenye kitabu cha Da Vinci Code.
Labda tungeanza na kuelewa kwanza nini maana ya neon “Da Vinci Code”.Hili ni jina la mwanahistoria,mwanasayansi,mwanafilosofia na mchoraji mashuhuri aliyekuwa akiitwa Leornando Da Vinci(1452 – 1519 A.D).Dan Brwon anadai kuwa huyu jamaa alikuwa ni mwanachama wa kikundi cha siri kilichokuwa kikidai kujua mambo ya siri ya wakati huo kilichojulikana kwa jina la “Priory of Sion”.Leornado Da Vinci ndio msingi mkubwa wa mwandis
  • hi Dan Brown kuhusu madai yake kuwa YESU KRISTO alikuwa na ndoa ya siri na Mariam Magdalena.Hii inatokana na mchoro aliochora Leornado Da Vinci ukielezea kalamu ya mwisho ya YESU na wanafunzi wake.Katika mchoro huu unaoitwa Da Vinci Code,inadaiwa kuwa Leornado amemchora Mariam Magdalena akiwa pembeni mwa YESU.Japo baadaye wakristo wengi waliamini huyo ni Yohana mwanafunzi wa YESU yule ambaye YESU alimpenda sana.Da Vinci hakuwa na lengo la kumchora Yohana kama kanisa lilivyokuwa likiamini bali alimchoro Mariam Magdalena, na ndiyo maana inaitwa “Da Vinci Code” yaani siri ya Da Vinci. Da Vinci anadai kwamba kwa kuwa YESU alikuwa na ndoa ya siri na Mariam Magdalena ndio sababu Mariam Magdalena ilibidi awepo kwenye kalamu hiyo ya mwisho.Angalia mchoro hapo chini.












Kutoka kulia kwenda kushoto ni Bartholomeo, Yakobo mdogo, Andrea, Yuda, Petro, Yohana(au Mariam Magdalena kulingana na Da Vinci Code), YESU KRISTO, Thomaso, Filipo, Mathayo, Thadeo na Simon.



Kwa hiyo Brown anaelezea uwongo wake kwenyer kitabu chake hicho kwa kumtumia profesa wa uingereza wa mambo ya kale yanayohusu elimu ya dini anayeitwa Sir Leigh Teabing.
Teabing anadai kwamba katika baraza la maaskofu zaidi ya 300 lililokutana Nikea mwaka 325 A.D, ”mambo mengi yanayohusu ukristo yalipigiwa kura na kutolewa maamuzi baada ya kujadiliana na kubishana kwa kirefu” likiwemo la Uungu wa YESU.
Teabing anasema kuwa kabla ya baraza la Nikea mwaka 325 A.D,YESU alikuwa anatambulika na wanafuasi wake kama mmojawapo wa manabii waliowahi kuwepo,na kwamba ni mwanadamu aliyekuwa na uwezo wa ajabu tu ila siyo Mungu kama inavyodaiwa.Kwa hiyo Teabing anadai kwamba YESU alifanywa kuwa mwana wa Mungu na pia alifanywa kuwa Mungu rasmi na baraza hilo la Nikea kwa kupigia kura uamuzi huo chini ya Mtawala wa Rumi wa wakati huo aliyejulikana kama Constantino.Tena anadai kuwa baada ya makubaliano hayo ya Maaskofu hao wapatao 300 ndipo nyaraka zote za muhimu zilizomuhusu YESU ziliteketezwa na kupotezwa kabisa.Kwa maneno yake Teabing anadai kuwa msingi mzima wa ukristo umejengwa juu ya uwongo.
Da Vinci Code haiwezi kujisimamia yenyewe bila kutumia matukio jalisi ya kilichofanywa katika baraza la Nikea, watu waliowahi kuishi kama Constantino na Arius na nyaraka zilizowahi kuandikwa kama injili za wagnostika.
Kwa hiyo kama tunataka kutengenisha kweli na uzushi huu, kazi yetu kubwa itakuwa ni kubainisha ukweli halisi wa hayo mambo ambayo bwana Dan Brown anayategemea kusambaza uongo wake.
UKRISTO NA CONSTANTINO
Kabla ya Constantino kuanza kutawala Rumi,wakristo walikuwa wakiteswa sana.Lakini baada ya Constantino kuwa mkristo(kuokoka) kwenye miaka ya 300 AD,akaigeuza Rumi na kuwa utawala wa kwanza wa kikristo na hivyo kanisa na serikali vikaunganishwa na kuwa kitu kimoja.Kutokana na hilo mateso kwa wakristo katika utawala wa Rumi hayakuwepo tena wakati wote wa utawala wa Constantino.
Kwa hiyo Constantino akaazimia kuunganisha utawala wake wa mashariki na magharibi ambao ulikuwa umegawanyika vibaya kutokana na kuibuka kwa imani mbalimbali za uongo,madhehebu mbalimbali,migawanyiko iliyotokana na tofauti za kiimani na mengineyo mengi ambayo yalitokana na mabishano kuhusu uhalisia wa YESU.
JE, KWELI CONSTANTINO NDIYE ALIYEANZISHA UUNGU WA YESU?
Kuweza kujibu madai ya Dan Brown ni lazima kwanza tujue ni kipi wakristo walikuwa wanaamini kabla ya Constantino na baraza la Nikea hawajakaa mwaka 325 A.D.
Wakristo walikuwa wakimwabudu YESU kama MUNGU tangu karne ya kwanza.Lakini katika karne ya nne,Kiongozi wa kanisa lililopo upande wa mashariki wa utawala wa Constantino aliyekuwa akiitwa Arius alianzisha kampeni akidai kuwa YESU aliumbwa kipekee zaidi ya malaika lakini hakuwa Mungu.Athanasius na viongozi wengine wengi wa kanisa kwa upande wao waliamini kuwa YESU alikuwa ni MUNGU katika mwili.
Kwa hiyo Constantino akataka kuumaliza mgongano huo ili alete amani katika utawala wake wa mashariki na magharibi.Kwa hiyo mwaka 325 A.D akawaalika zaidi ya maaskofu 300 kutoka kila sehemu ya ulimwengu wa kikristo wa wakati huo kwenda Nikea (ambayo kwa hivi sasa ni sehemu za Uturuki)
Swala kubwa hapa ni, Je kanisa la kwanza lilimchukulia YESU kama muumbaji au ni kiumbe tu – mwana wa Mungu au mwana wa fundi seremala? Je mitume walifundisha nini kuhusu YESU?Kutoka katika maelezo yao ya awali kabisa kwenye nyaraka zao walimwona YESU kama Mungu.Baada ya miaka 30 tangu kufa na kufufuka kwa YESU,Paulo mtume anawaandikia wafilipi kuwa YESU ni MUNGU katika mwili (Wafilipi 2:6-7).
Pia Yohana,mwanafunzi aliyekuwa karibu zaidi na YESU na kuishi naye kwa zaidi ya miaka 3 anathibitisha Uungu wa YESU katika maneno haya (Yohana 1:1-4,14) ”Hapo mwanzo alikuwepo Neno,naye Neno alikuwepo kwa Mungu,naye Neno alikuwa Mungu,………………………………………….naye Neno akafanyika mwili na kukaa kwetu.Nasi tukauona utukufu wake……………….”
Aya hii kutoka injili ya Yohana iligundulika kwa kutumia kipimo cha carbon-14 kuwa iliandikwa kwenye mwaka 175 A.D.
Kwa hiyo YESU alikuwa akitajwa kama Mungu zaidi ya miaka 100 kabla ya Constantino hajaitisha baraza la Nikea.Kwa hiyo tunaona kuwa madai ya uzushi ya Da Vinci Code kuwa Uungu wa YESU ni matokea ya mkutano wa Nikea karne ya 4 ni uongo mtupu.
Kwenye kitabu chake Dan Brown anadai kupitia Teabing kwamba maaskofu wengi kule Nikea walikubaliana na mafundisho ya Arius kuwa YESU ni nabii wa kawaida tu na kuwa eti mafundisho ya sasa kuhusu Uungu wa YESU yalikubaliwa kwa kura chache sana.
Ukweli ni kwamba ,kati ya kura 318 za maaskofu wote waliopiga kura ni wawili tu ndio waliokubaliana na mafundiho ya Arius ,lakini wengine wote waliamua kubaki na mafundisho ya mitume wa kwanza walioishi na YESU KRISTO kuwa YESU ni Mungu na ni zaidi ya nabii wa kawaida.
Baraza likaamua na kukubali kuwa YESU na Mungu Baba ni wamoja,Pia Mungu Baba,Mwana na Roho Mtakatifu ni utatu mtakatifu,(coexistent,coeternal Persons but one God).Mafundisho haya ya utatu mtakatifu ndiyo msingi mkuu wa imani ya kikristo.Japokuwa Arius alikuwa ni mtu aliyekuwa na ushawishi mkubwa,lakini baada ya majadiliano marefu na kutafuta ukweli na ushahidi wa kutosha baraza la Nikea likamtangaza rasmi Arius kuwa ni mzushi dhidi ya imani ya kikristo (heretic) kwa sababu mafundisho yake yanapingana na yale waliofundisha mitume kuhusu Uungu wa YESU
Historia inaonyesha bila mashaka yoyote kuwa YESU akikubali waziwazi kabisa kuabudiwa na wanafunzi wake.Paulo na wanafunzi wengine wanafundisha kwa uwazi kabisa kuwa YESU ni Mungu na anastahili kuabudiwa.Na hawa mitume walifundisha hivi na hata kumwabudu YESU tangu karne ya kwanza.Sasa iweje tena Teabing adai kuwa Constantino ndiyo aliyeanzisha Uungu wa YESU wakati kanisa lilikuwa likimwabudu YESU kama Mungu miaka zaidi ya 200 kabla ya Constantino.Huu ni uwongo wa wazi kabisa na wala hauhitaji mtu kuwa na PhD kuugundua.
JE, NI KWELI HISTORIA YA KWANZA YA YESU ILIHARIBIWA NA CONSTANTINO?
Da Vinci Code inadai kwamba Constantino aliharibu ushahidi wa historia ya kwanza kabisa ya YESU na kuamuru iandikwe upya kwa kutumia injili tulizonazo hivi sasa kwenye agano jipya na kuziharibu injili nyingine zaidi ya 80.
Hapa kuna mambo mawili ya kumjibu Dan Brown.Kwanza ni kujua iwapo kuna ukweli wowote katika madai kwamba Constantino alibadilisha na kulazimisha uchaguzi wa vitabu vya Agano Jipya.Pili ni kujua iwapo aliteketeza nyaraka za awali ambazo zingetumika kuandika Biblia.
Tukianza kujibu hoja ya kwanza, maandiko na nyaraka mbalimbali zilizoandikwa na viongozi wa kanisa karne ya pili na wazushi na wapinzani mbalimbali zinathibitisha matumizi makubwa ya vitabu tunavyotumia leo hii vya agano jipya.
Karibu miaka 200 kabla ya Constantino hajaitisha baraza la Nikea, mpinzani na mzushi Marcion alivikubali vitabu 11 kati ya 27 vya Agano Jipya kama maandiko ya mitume wa kwanza.
Na kwa wakati huohuo mzushi mwingine na mpinzani Valentinus alitumia sehemu kubwa ya maandiko yaliyopo katina Agano Jipya.Kwa hiyo tunaona kuwa hawa wazushi wakubwa wawili waliokuwa ni wapinzani wakubwa wa viongozi wa kanisa la kwanza walitumia maandiko hayahaya tunayotumia leo hii kwenye Agano Jipya, haingekuwa rahisi kwao kuandika yale ambayo maaskofu wa Nikea waliyataka, Hii inaonyesha wazi kuwa kanisa la kwanza walitumia sana vitabu vya agano jipya tunavyotumia leo kabla ya Constantino.
Hivyo basi hakuna ukweli wowote kuwa Constantino alishinikiza na kuanzisha matumizi ya vitabu hivi vya Agano Jipya wakati ambapo vilishakuwa vinatumiwa na mamilioni ya waamini kama maneno ya Mungu karibu miaka 200 kabla yake.
Na kujibu hoja ya pili kuwa nyaraka hizi za kale za injili ya wagnostika ziliteketezwa na kutoweshwa zisiwemo kwenye agano jipya ili kupotosha ushahidi.Teabing anadai kwamba injili za wagnostika ziliondolewa kutoka kwenye Biblia 50 za mwanzo ambazo Constantino aliagiza ziandikwe.
Injili hizi za wagnostika zinatokana na kikundi cha watu wanaojulikana kama wagnostika, Jina hili linatokana na neon la kiyunani (kigiriki) gnosis, likiwa na maana ya “maarifa”.Watu hawa walikuwa wakifikiri kuwa wao wanafahamu mambo fulani fulani ya siri ambayo watu wengine hawakuwa wakiyajua.
Kadri ukristo ulivyokuwa ukienea sehemu mbalimbali, wagnostika waliyachanganya mafundisho yao na baadhi ya mafundisho ya ukristo na wakaanzisha imani iliyokuwa na mchanganyijko wa kignostika na ukristo.
Katika historia ya ukristo iliyoandikwa na Oxford, John Manners anaandika jinsi wagnostika walivyochanganya ukristo na hadithi zao za kale, dini za miungu yao ya asili na mizimu na mambo yao ya kiuaguzi.
Tofauti na Brown anavyodai,si kweli Constantino ndiye aliyesababisha kuichukulia imani ya wagnostika kama imani potofu bali ni mitume wenyewe wa kanisa la kwanza ndio waliosema kwa uwazi kabisa kuwa imani ya wagnostika ni potofu.
Mfano Mtume Yohana alivyoandika kati ya mwaka 95-99A.D. Katika 1Yohana 2:22Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Masiha. Mtu wa namna hiyo ni adui wa Kristo--anamkana Baba na Mwana.”
Kwa kufuata mafundisho ya mitume,viongozi wa kanisa la kwanza walitangaza waziwazi kuwa ugnostika ni imani potofu.Mmoja kati ya mababa wa kanisa, Irenaeus,aliandika miaka 140 kabla ya baraza la Nikea kuwa ugnostika ulichukuliwa na kanisa kama imani potofu.Pia alizikataa “injili” zao na akiunga mkono injili nne zilizopo kwenye agano jipya alisema “haiwezekani vitabu vya injili vilivyopo vipunguzwe au viongezwe
Mwanatheolojia mmoja aliyejulikana kama Origen aliandika hivi katika karne ya 3 ,zaidi ya miaka 100 kabla ya Nikea.
Najua kuna injili fulani inayoitwa ,”Injili ya Thomaso”,and “Injili ya Mathias”, na nyinginezo nyingi—Hebu na mtu asituone sisi ni wajinga kwa sababu ya hao wanaojifikiria wao wenyewe kuwa wanaoufahamu fulani[gnostics].Hata hivyo zaidi ya yote haya,sisi tumeshathibitisha bila mashaka yoyote ni injili zipi kanisa linazitambua,ni zile injili nne tu ndizo zinazokubalika
Kwa hiyo hapa tunaona kauli na mapendekezo ya viongozi wa mwanzo wa kanisa waliokuwa wakiheshimika sana kwa wakati huo.Wagnostika hawakutambuliwa kama wakristo na walijulikana kama imani potofu kabla ya hata baraza la Nikea
KUHUSU WAANDISHI WA INJILI ZA WAGNOSTIKA.
Swali la kujiuliza hapa ni,Je, kwa nini basi injili zote hizi za wagnostika zinadaiwa kuandikwa na wahusika waliopo kwenye agano jipya la Biblia tunayoitumia leo hii? Mfano,Injili ya Filipo,Injili ya Petro,Injili ya Mariam(Magdalena),Injili ya Yuda, na kadhalika.Je ni kweli ziliandikwa na wahusika wenyewe kama inavyodaiwa na wagnostika?
Injili hizi zote za wagnostika zimeandikwa kati ya mwaka 110 hadi 300 A.D.Na hakuna hata mwanazuoni yeyote anayeamini kuwa zimeandikwa na wahusika wenye majina ya hizo injili kwa kuwa hazina ushahidi wa kutosha.
Moja kati ya maelezo yanayopatikana katika maktaba ya Nag Hammadi huko Misri(sehemu ambayo injili ya wagnostika ya filipo iligundulika mwaka 1945) yanaeleza kwamba “injili za wagnostika ziliandikwa na waandishi wasiojulikana na wahusika wanaodaiwa kuandika injili hizo siyo wale waliopo kwenye agano jipya [tunalotumia leo]
Mmoja kati ya wanazuoni wa agano jipya Norman Geisler akizielezea injili mbili za wagnostika,injili ya Petro na matendo ya Yohana(hizi siyo vitabu vya agano jipya tunavyovifahamu) anasema,”maandiko ya wagnostika hayakuandikwa na mitume ila na watu wengine katika karne ya 2 na kuendelea,wakijifanya kupewa ruhusa na mitume ili wafikishe mafundisho yao kwa wakristo.Katika siku za leo tunauita huu ni udanganyifu na utapeli
JE, KWELI YESU ALIKUWA NA NDOA YA SIRI NA MARIAM MAGDALENA?
Hoja hii ndiyo ambayo imeonekana kuleta utata zaidi ulimwenguni na hata kusababisha kitabu hicho cha uzushi cha Dan Brown kuuzwa na kununuliwa sana.
Da Vinci Code inadai kuwa YESU na Mariam Magdalena walikuwa na ndoa ya siri iliyosabisha kuwa na uzao.Dan Brown anadai kwamba kikundi cha siri cha kikatoliki kinachojulikana kama “Priory of Sion” ndicho kinachotunza siri kuwa tumbo la Mariam Magdalena lilobeba uzao wa YESU ndio linaloitwa kikombe kitakatifu “Holy Grail”. Brown anadai kuwa baadhi ya wanachama wa kikundi hiki cha Priory of Sion ni pamoja na Sir Isaac Newton, Botticelli, Victor Hugo na mzushi maarufu Leornado Da Vinci.
Je madai haya ni ya kweli? Hebu tuangalie wanazuoni wengine wanasemaje kuhusu uzushi huu.
Katika makala moja iliyotochapishwa na gazeti la Newsweek inamnukuu mwanazuoni mmoja akisema kuwa “Madai kwamba YESU na Mariam Magdalena walioana kwa siri hayana ushahidi wowote wa kihistoria,Hoja zinazotolewa na Da Vinci Code zinasimamia kwenye mstari mmoja wa injili ya wagnostika ya Filipo inayoonyesha kuwa Mariam Magdalena alikuwa na ukaribu na YESU”
Pia kuna mstari mmoja tu katika Injili hiyo ya wagnostika ya Filipo kuwa YESU alimbusu Mariam Magdalena.Lakini kumsamia mtu kwa kumbusu kilikuwa ni kitu cha kawaida katika karne ya kwanza katika eneo hilo la mashariki ya kati,na hilo siyo jambo la ajabu”.
Siyo hivyo tu ila tunaona kwamba injili ya Filipo ya Wagnostika ni ulaghai ulioandikwa kati ya mwaka 150-220 A.D na mwandishi asiyejulikana.Kwa hiyo madai yote yaliyomo humo hatuwezi kuyaamini hata kidogo.
Pia kuhusu kikombe kitakatifu (Holy Grail) na pamoja na Priory of Sion,Brown hana ushahidi wowote kuhusu hilo kwa sababu kikombe kitakatifu ni kile kikombe alichotumia YESU wakati wa kalamu ya mwisho na wala hakina uhusiano wowote na Mariam Magdalena.
Kuhusu Priory of Sion ni uongo wa wazi kabisa ambao Dan Brown anauzusha bila kuona aibu hata chembe.Leornado Da Vinci hajawahi kuwa mwanachama wa kundi hilo kwa sababu kundi hilo liliundwa rasmi mwaka 1956, miaka 437 baada ya kifo chake. Leornado Da Vinci aliishi kati ya mwaka 1452 hadi mwaka 1519.
JE NI KWELI KUNA NYARAKA ZA SIRI ZILIZOFICHWA?
Teabing anadai kwamba kuna maelfu ya nyaraka za siri zinazothibitisha kwamba ukristo ni hadithi za uongo za kutunga na kufikirika.Je, madai haya ni kweli?
Kama kungekuwa na nyaraka hizo kama anavyodai Teabing,basi wanazuoni wapinzani wa ukristo wangekuwa tayari wameshazisambaza tangu kipindi hicho.Nyaraka za uzushi zilizokataliwa na kanisa la kwanza wala siyo siri tena na zimekuwa wazi kwa karne nyingi sasa.Wala hakuna la ajabu hapo,kwani hazikuhusishwa kama sehemu ya maandiko yaliyokubaliwa na mitume.
JE, LERONADO DA VINCI ALIKUWA SHOGA?
Baadhi ya wanazuoni wanaamini kwamba Leornado Da Vinci alikuwa shoga au alipenda kujihusisha na mambo ya kishoga.Wanatoa madai haya kutokana na ukweli kwamba Leornado Da Vinci hakuwahi kuwa na mke.Lakini hili sio jambo hasa la kumfanya mtu kudhaniwa kuwa ni shoga ila tatizo hapa ni ile tabia yake ya kupenda kuchora picha za vijana wa kiume wazuri wakiwa uchi wa mnyama. Mara nyingine alichora vijana hao wazuri wakiume wakionekana kuingiliana kimwili wao kwa wao.Pia mwaka 1476,Leornado Da Vinci alifikishwa mahakani kwa mashtaka ya vitendo vya kishoga.Japokuwa alifungwa kwa miezi miwili lakini mashtaka hayo yalifutwa kwa kukosekana ushahidi wa kutosha.
UKWELI UPO WAZI KABISA.
Tumeona kwa uwazi kabisa ukweli usiopingika kuhusu maisha matakatifu ya YESU KRISTO mwana wa MUNGU na ni MUNGU halisi kama Biblia takatifu inavyosema katika Injili ya Yohana 1:1-4; 14
Tofauti kabisa na injili za wagnostika, ambazo waandishi wake hawajulikani (hazijulikani ziliandikwa na nani), Agano Jipya tunalotumia leo hii limepitia majaribio mengi likithibitishwa kwa karne nyingi sasa.
Mwanazuoni mmoja aliwahi kusema kwamba, kama unataka kusoma uzushi na hadithi za uongo kuhusu YESY KRISTO wa Nazareth, basi kitabu cha Da Vinci Code chaweza kuwa chaguo lako zuri, lakini kama unataka kuujua ukweli wa maisha ya YESU kutoka kwa watu waliomwona kwa macho na kuishi naye basi Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo, Mtakatifu Marko, Mtakatifu Luka na Mtakatifu Yohana ndiyo chaguo lako bora kabisa la wakati wote la kujua njia sahihi kabisa ya kuweza kumwona Mungu.

No comments: