Sunday, February 17, 2013

Watatu wanahojiwa Zanzibar: Padre/Father Mushi auawa kwa risasi

UPDATE/TARIFA MPYA (saa nane u nusu mchana) Taarifa ya Polisi:

Watu watatu wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Padre Mushi. Tafadhali bofya vipande vya picha zilizopachikwa hapo ili kuvikuza na kusoma taarifa ya Polisi inayoonekana hapo (shukurani kwa Francis Dande).
UPDATE/TAARIFA MPYA (saa saba mchana) Taarifa ya habari Radio One Stereo:
Taarifa ya habari ya Radio One Stereo iliyosomwa saa 7 mchana imeripoti kuwa Padre Mushi aliuawa na watu walipolisimamisha gari la Padre huyo alipokuwa akielekea katika kanisa la Mtakatifu Theresia lililoko eneo la Mtoni, na alipopunguza mwendo ili awasikilize, ndipo alipopigwa risasi kichwani na kusababisha gari alilokuwamo kukosa uelekeo na kuigonga nyumba iliyokuwa jirani. Watu walioshuhudia tukio hilo walimchukua Padre Mushi ili kumwahisha hospitalini katika jitihada za kuokoa uhai wake, lakini alifariki dunia. Waliomwua Padre Mushi bado hawajakamatwa.
                                                                                                      -----------------------

Taarifa kutoka Zanzibar zikiripotiwa na mwanahabari Donisia Thomas wakati kipindi cha Patapata cha WAPO radio FM kinaendelea, zinasema kuwa Padre Evaristus Mushi wa Kanisa la Parokia ya Minara Miwili huko Zanzibar amepigwa risasi majira ya saa moja asubuhi -na watu wasiofahamika- na kufariki dunia.

Taarifa za kufariki kwake zimethibitishwa na madaktari kutoka hospitalini alikopelekewa katika harakati za kuuokoa uhai wake.

Padre Mushi aliuawa akiwa anashuka kwenye gari lake tayari kuingia Kanisani kwa ajili ya kuendesha misa ya kawaida ya Jumapili katika kanida la Mtoni, mjini St. Joseph. Inaelezwa kuwa gari lisilofahamika lilifika na kufyatua risasi zilizomlenga Padre Mushi sehemu ya kichwani na hivyo kumsababisha majeraha yaliyokuwa yakivuja damu nyingi.

Mwanahabari anasema tukio hilo limezua taharuki kubwa miongoni mwa waumini ambao wamekataa kuahirisha ibada iliyokuwa iendeshwe na Padre huyo na kusema ikiwa kusudio ni kuwaangamiza Wakristo wote, basi na waangamizi wafike Kanisani wawaangamize wakiwa pamoja.

Jeshi la Polisi limeshafika katika eneo la tukio na kuanza uchunguzi.

Tukio kama hili liliwahi kutokea mwishoni mwa mwaka jana kwa Padre Ambrose kupigwa risasi.

Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/02/zanzibar-padrefather-mushi-emepigwa-risasi-na-kuuawa.html#ixzz2L9yw5E9H

No comments: