Sunday, August 10, 2008

Angela Lubala ajivua taji la ubalozi wa Redds kwa imani ya dini

Na Mwandishi Wetu
BALOZI wa Redds Angela Lubala ametangaza rasmi kujivua taji lake kutokana na shinikizo la imani ya dini.
Angela mapema wiki iliyopita alifanyiwa sherehe ya kukabidhiwa rasmi mikoba ya ubalozi wa Redd's na balozi aliyepita Victoria Martin kwenye hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam.
Katika sherehe hiyo Mwananchi ilihoji juu ya imani yake ya dini na kuwa balozi wa bia ya Redd's mrembo huyo aliyekuwa amefuatana na mama yake mzazi, mdogo wake alisema: " Kwa sasa hata nikizungumza watu hawatanielewa, lakini mimi ni mtu mzima mwenye zaidi ya miaka 18 nina maamuzi yangu, nashukuru wazazi wangu wananisapoti," hiyo ilikuwa kauli ya balozi wa Redds siku nne zilizopita alipofanya mahojiano na Mwananchi.
Hata hivyo pamoja na wazazi hao kuudhuria shughuli hiyo ya mtoto wao kukabidhiwa mikoba ya kuitangaza pombe ya Redd's jana wamepasua hadharani kuwa shinikizo kutoka kwa viongozi wa kanisa na baadhi ya waumini wa kanisa la Kilokole la Word Alive lililopo Sinza Mori ndio lililowafanya wakaamua kumvua taji binti yao.
Inadaiwa baba yake ambaye anafahamika kwa jina halisi la Askofu Deo Lubala aliwekwa kitimoto na uongozi wa juu wa kanisa hilo na kumshinikiza kumuondoa binti yake kwenye shughuli hiyo inayohusisha pombe.
Naye meneja wa Redd's George Kavishe alisema, "Sijui lolote wao siku tunamkabidhi rasmi bendera ya ubalozi wa Redd's pale New Afrika wazazi wake wote walikuwepo, leo wanaenda kumvua taji binti yao hata kutujulisha."


Source: Mwananchi Newspaper.

No comments: