Sunday, August 10, 2008

Wito Kumwombea na kumtia moyo dada Angela

Shalom na Bwana Yesu asifiwe sana!
Ninawaandikia post hii baada ya taarifa tulizozipata za dada Angela Lubalanza ambaye amejivua taji la ubalozi wa bia ya Redds.
Kila mtu anajua namna wapendwa na watu wengine wengi walivyokazana kulipinga suala la dada huyu kujiingiza kwenye mashindano ya urembo na hata kuwa balozi wa bia. Kama kuna waliomwombea basi Mungu awabariki sana, inawezekana Mungu amejibu maombi yao.
Wale ambao wamekaa makanisani kwa muda mrefu nadhani wameshawahi kuona pale mtumishi wa Mungu anapofanya kosa na kupoa kiimani. Wakristo wengi huungana na wamataifa kuanza kumsema vibaya, kumnyooshea vidole na mambo mengine kama hayo. Wapendwa, kitendo hicho humzuia sana yule mtu aliyerudi nyuma, pale anapoamua kuanza upya na Bwana. Unakuta mtu ameamua kurudi tena kwa Yesu kumtumikia, lakini watu bado wanaendelea kumsema vibaya, mara utasikia "Tulimwambia akajifanya mjuaji, ona sasa" na maneno mengine. Tena unakuta wanaomsema hivyo ni wakristo wenzake, tena na waliookoka wamo humo. Hiki ni kitu kibaya na Bwana Yesu hakipendi. Mtu anapoamua kurudi kwake tunatakiwa kumsaidia na kumtia moyo huku tukimpa mifano kama ya Mfalme Daudi na wengineo.
Kwa hivyo basi, Sisi wana Sayuni tunachukua nafasi hii kuwasihi wakristo wote kumpokea Dada Angela tena kwa Yesu, tumkaribishe vizuri, tumwombee na kumtia moyo ili asimame katika nafasi yake. Tafadhali msimcheke wala kumdharau. Kumbukeni kuwa Yesu Kristo alikufa kwa ajili yake pale msalabani, msiiharibu kazi ya Bwana Yesu.
Nawasihi zaidi wale waumini wa kanisa la Baba yake kumpokea kwa ukaribu zaidi, wawe naye k aribu sana, wamsaidie kwa kila namna. Na wana-blog wote pia sasa tuungane kumtia moyo na kumwombea kwa bidii.
Ninaamini kuwa Mungu atambariki kila mtu atakayelifanya hili kwa vitendo.

Mbarikiwe sana, Karibu Sayuni.

1 comment:

Anonymous said...

Usiwe kama unampoza huyo Angela swala linakuja kwamba angela kwa upande mmoja au mwingine si binti mdogo na wala sio mkubwa ingawa kwa sheria za nchi yetu ni ameshafikia kuitwa mtu mzima, sasa swala ni kwamba kwani Angela akati anashirikia hayo mashindano baba yake hakuwepo au watu wakubwa wa karibu yake hawakuwepo? hapo inaonyesha jinsi gani baadhi ya wanandini wanashindwa kusimamia mambo yanayohusu na kuzunguka jamii zao. Lawama kwa upande mmoja au mwingine atupiwe pia baba au mama yake.