Saturday, March 8, 2008

Viongozi wa kanisa muda umefika amkeni!

Lengo na dhumuni la nakala hii ni kusupport mawazo ya ndugu Lema ambaye ameandika nakala ya iliyotangulia;

Unajua kwa nini viongozi wetu wa dini wako kimya? Wako kimya kwa sababu hawatoki tena mbinguni.Wanatoka duniani.Wanaitegemea serikali badala ya serikali kuwategemea wao ,''tumepewa mamlaka'' inaishia madhabahuni

Nimefundishwa kanisani na nimeelewa uhusiano uliopo kati ya Kristo na Kanisa, achilia mbali kufundishwa kwenye mafundisho ya ndoa kwa undani zaidi, lakini kila mchungaji padri,maaskofu makadinali wanayajua haya, kuwa kanisa ni mfano halisi wa mwanamke!
Linatakiwa liwe na sifa zote za mwanamke, ambazo ni pamoja na utii,upendo,kujali,kukusanya kulinda n.k

Pamoja na kuwa tunaweza kuringa tuna roho mtakatifu hata na kuwa na nguvu za kuhamisha milima,kufufua wafu,katu bila upendo unaoendana na matendo halisi ya wakati na mahali husika karama zetu na kazi zetu ni bure,bila kuwa na moyo,hari na uwezo wa kutetea haki hatufai utumishi wetu tutaulizwa,wapentekoste wangapi wanalea yatima?,maskini?,wajane? n.k, ni aibu ya kuwa pengine wamataifa wametuzidi kwa mbali sana.

Kwa sababu tunajiona tumefika mbinguni,upako tulionano pengine umetupofusha? Nitakataa kumbe penye upako au nguvu za Mungu kuna haki kuna ukweli,kuna ujasiri kama wa Stefano akifa bila kumkana Yesu, Kama tunasema Mungu habadiliki ni yule jana leo na hata Milele,tunaambiwa pia Eliya alikuwa mtu wa kawaida sawa na sisi aliamuru Mvua isinyeshe na ikawa,naam zaidi tunaishi pia katika kipindi ambacho Roho mtakatifu ni dhahiri kwa watu walioamini, wakati zamani nguvu hizo zilikuwa kwa wachache na ndio tunaowasoma hata leo. Wako wapi akina Daniel,Shadrack, Meshack na Abedinego,nimesikia kuna manabii wengi zama hizi , wako wapi akina Yohana mbatizaji ambaye alieleza uovu wa kiongozi serikalini!??????

Watu wanaishi kwa taabu nchi hii, maisha Magumu, rushwa kila mahali,ubadhirifu wa fedha za umma uko dhahiri, haki kupindishwa, uonevu mahali mahali, wakati kuwa Kuna baadhi ya viongozi wa dini wanadai waliomba wakajibiwa na kuwa ni majibu ya Mungu kuwa na viongozi tulionao sasa! Nikaamini zama za viongozi kupakwa mafuta kumbe hata sasa zipo japo si za moja kwa moja ‘indirectly’ .Nikaamini basi watatokea akina Samweli na Nathani enzi za mfalme Sauli na Daudi ambao watakosoa utendaji kazi mbovu, baadhi ya mambo yasioyosahihi ya serikali,vyama,taasisi hata zisizo za kiserikali.Mmekaa kimya kama vile sio viongozi wa kanisa.Yesu ni Mfalme wa wafalme, yuko juu ya serikali na mamlaka zote, Yesu huyo mnae tena kila siku mnawaita watu waje kuombewa magonjwa mbalimbali yakiwemo ukimwi ambao nimeona kwa macho yangu watu wanapona hata kama serikali haitaki tuseme,

Kanisa likae kimya juu ya ununuzi wa rada, ndege ya raisi,matumizi mabaya ye serikali,kunyima haki watu, maisha ya taabu na dhiki wanayoishi watanzania,EPA,RICHMOND,? Kama tunaambiwa tuheshimu mamlaka ni pamoja na kuiambia ukweli, si mamlaka zote zinaheshimiwa kwani sidhani kama Mungu anaweza kuweka mamlaka kama za akina madikteta tunaowajua kama hatukutaka wenyewe!

Kanisa ni dhaifu kwa sababu tuna viongozi wa makanisa dhaifu katika kutambua na kuelewa wajibu wao katika jamii si kiroho tu bali hata kimwili.Yale yaliyo katika uwezo wetu kuyafanya mnatakiwa mfanye kwani ninyi ni miungu(Zaburi 82:6, Yohana 10:34) .

Waumini wenu au washirika wenu, wamesalitiwa vyama vinavyojiita vya upinzani vimewasaliti maana havina mpango wa kuungana pamoja kilammoja anataka chake,baadhi ya wasomi wakiwemo maprofesa wamewasaliti, wengine mmewaona juzi wakitoa maamuzi ya kisiasa wakati wao wasomi, Siasa imeingia kwenye elimu ambayo ni dira ya taifa,kodi wanazotoa waumini wenu na nyie maaskofu zinaharibiwa. Yesu alikasirika siku moja alipoingia hekaluni na kukuta minada inaendelea badala ya neno la Mungu,hekalu la sasa ni mtu.Tumaini la watanzania liwe viongozi wao wa kanisani.

Hawa wasomi, viongozi wa serikalini mafisadi ni waumini wenu na mnachukua sadaka zao! Mambo wanayopitia kizazi cha sasa ndio kinaelezea aina ya viongozi ambao tutakuwa nao baadae, aina ya wachungaji ambao tutakuwa nao baadae, hali ya maisha ya sasa inelezea jinsi ambavyo ni vigumu kwa viongozi wa kanisa kukataza rushwa hapo baadae,mmeona jinsi ambavyo mkuu wa mkoa wa DSM akipiga vita wasichana kujiuza mwili, wameacha au wamebadilisha maeneo?, jamani manabii,mitume,walimu,wainjilisti,wachungaji mko wapi? Au kwa sababu zaka na sadaka vinaletwa tu? Lakini hao waumini wenu watafika mbinguni??? hizo sadaka na zaka zinapatikana kihalali?(Fikiria wewe ni mchungaji wa Lowassa mpaka anapata aibu ile si ni aibu ya kanisa!! wewe mchungaji ulikuwa haujui kuwa ana tatizo, la hata inawezekana kweli ulikuwa haujui kwa jinsi ya kibinadamu, je Roho hakukuambia?? kama hakukuambia basi hauombi! na kama hauombi basi haufai kuwa mchungaji!!! na kama ulijua ukaka kimya dhambi hiyo pia ni yako.Timotheo aliambiwa ONYA, KARIPIA maana mchungaji wa kweli aliyejazwa Roho , hekima na mamlaka viongozi wa serikali wanatetemeka maana sio wewe unayeishi bali ni kristo) kuna mtu atasema mchungaji yule wa Lowassa hajaokoka , je ni wachungaji wangapi waliookoka wangeweza kuzuia kama yasimtokee Lowassa kamaLowassa angekuwa muumini wa kanisa lake??

Amkeni maaskofu kondoo wenu wanararuliwa kwani nyie ni viongozi wa mshahara?, Yesu alisema kiongozi mwema yuko tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengine.Mna Mungu anayetisha, anayeweza,wa haki muwazi mkweli,hashindwi,haogopi!.Jamani hata sasa tunahitaji kuwaona mashujaa wa Imani za kiroho na kimwili,hata kama hawataandikwa kwenye biblia mbinguni wataandikwa!

Ukiwa na viongozi wa kidini vipofu,wasiosema kitu wala kukaripia serikali kama akina Gamanywa,Kulola n.k ambao kwa nafasi zao walitakiwa wawe wakali na hakika Taifa lingewaogopa na kuwaheshimu si siri na si bure viongozi wa kilokole Tanzania hawaheshimiwi huwezi kufananisha heshima ya Pengo serikalini na Kulola?? Hiyo nguvu isiishie kuombea watu Yohana alimbatiza mpaka Yesu bado akaenda gerezani kwa kusema kuwa mkuu serikali ni mzinzi, je ni ngumu sana kwa mtu kama Gamanywa kukemea uovu nay eye ni mwenyekiti wa makanisa ya kipentecost!! Kalagabaho watu wanafanya biashara zao na wako tayari ku-compromise GOD’s standard by using money!! Sio kwamba simpendi nazungumza kwa nafasi yake na vita ya maisha bora tunayoyalilia.

Urafiki huu na uoga huu tutaletewa sheria ambazo watapitisha waumini wenu ili hali nyie mmekaa kimya.Wabunge wa Afrika kusini waliopitisha sheria ya kutambua ndoa za jinsia moja, hivi hawa hamna wakristo?, si wana viongozi wao wa kanisa.Basi tunaweza kusema ndiyo wanayofundishwa kanisani? La! sasa wanatoa wapi.Kuchekea na kudharau mambo madogo huzaa makubwa,Kanisa lingekuwa na nguvu hata hiyo hoja ya mahakama ya kadhi wangejiuliza mara mbili kama waizue au wakae kimya , kutokana na udhaifu wa Kanisa linajadiliwa mpaka kuundiwa tume inayolipwa na kodi za waumini wa kanisa! Wameona sisi ni dhaifu tuko kimya kazi kuandaa matamasha na kuwaita viongozi wa serikali wazindue albamu na kugawa tuzo! Tumemwachia kazi hii Mtikila!!

Tusiangamie kwa kukosa maarifa yaliyo katika uwezo wetu kuyafanya tunayafanya,tuna mamlaka,tuna Mungu,tuna Roho tuna elimu,tuna mdomo tuna la kusema,hatujachelewa bado,kumbe kweli mmomonyoko wa maadili,maisha ya taabu ya wananchi kanisa limechangia.Hivi ndio Nionavyo mimi INAWEZEKANA AMKENI!!

‘’Lakini nawasihi, ndugu,mchukuliane na neno hili lenye maonyo maana nimewaandikia kwa maneno machache’’ Waebrania 13:22

Nakala hii pia niliitoa gazeti la nyakati toleo la 335 May 2007, edited to suit now.

Kalenge-Canada
Imanimartini2222@gmail.com

5 comments:

Maranatha said...

Hakika kwa kila jambo hapa duniani kuna sababu juu yake. Je uongozi wa nchi yetu Tanzania tuwaachie MAFISADI NA WALA RUSHWA, Tuko wapi watu wa Mungu, Je hata kuikosoa serikali kwa uwazi tumeshindwa, au tuna nidhamu ya woga? Hebu na tujiulize ndani ya mioyo yetu kwa dhamiri safi na ukiona si sahihi hebu na tuchukue hatua! Yuko wapi Samuel wa leo mwenye ujasiri wa kumkosoa Sauli kwa kufanya asiyoagizwa? Nani atasimama katika zamu ili kukemea uozo unaondelea serikalini na kwa wanasiasa wanaocheza mchezo mchafu hata hadharani?

Si kwamba watumishi wetu haayaoni haya, katu! Bali kuna namna fulani ya woga miongoni mwetu au haiyumkini kuna namna fulani ya UBIA!

Anonymous said...

Ndg wapendwa! Mara nyingi watu wanashindwa kuwa na ujasiri kwa kuchelea kuchanganya dini vs siasa. Wanaona kwamba mambo ya kisiasa au ya nchi yanaweza kutatuliwa kwa kupiga magoti na kuomba/kukemea na sio kujionyesha physically. Mara nyingine baadhi ya makanisa hutishiwa kufungiwa na serikali (kumbuka lile la Kakobe). Jingine ambalo siamini kama lina nguvu sana ni kuwa inawezekana mafisadi husaidia mara kwa mara kwenye kutoa michango ya ujenzi wa makanisa. Niambie kama mchungaji atakuwa na ubavu wa kukemea uovu wowote! Cha kutia moyo ni kwamba kale kanidhamu ka woga ka wadanganyika, sory watanzania, kanazidi kupungua siku hadi siku. Ila kazi bado kubwa sana ya kuifanya nchi hii kukaa kwenye mstari ulionyooka katika kuelekea kwenye maendeleo ya uhakika, utashanga mwaka 2010 mafisadi wanashinda tena uchaguzi tusipokufumbua macho. Mungu awabariki.

Anonymous said...

Ni kweli kabisa mtumishi, Ni mambo ambayo huwa yananiuma sana pale ninaopoona viongozi wa makanisa ya Kiroho hawana sauti kabisa hasa katika mambo ya kiserikali. Kwa ukweli sisi tuliookoka ndo ilitakiwa tuwe na sauti kuliko Dini zingine, hasa ukizingatia idadi ya watu waliookoka inakua kwa kasi kubwa sana nchini kwa miaka hii ya karibuni. Mara kwa mara nimekutana na watu wa Mungu mbalimbali na wengi wao (hasa wachungaji vijana wasio na uongozi wowote katika makanisa yetu)mara nyingi wamekuwa wakielezea hisia zao kuhusiana na mambo yanavyoendeshwa serikalini huku watumishi wa Mungu tukiwa kimya kabisa tumefumbwa vinywa kabisa.

Inawezekana kabisa yumkini tuna nidhamu ya woga kwa Serikali.

Anonymous said...

Ni kweli wakati wa kuamka kutoka katika usingizi wa kiroho umewadia kama neno la Mungu linavyosema ktk amka uangaze maana nuru imekuzukia, na nuru inapoangaza ni wazi kwamba giza halina nafasi tena. Tumesahau wajibu wetu kama kanisa kwamba tumepewa mamlaka ya kuteka na kutawala, maadamu hili tumelifahamu ni jukumu letu kupambana na kuhakikisha Tanzania inakuwa huru katika misingi ya Kimungu.

Anonymous said...

Shalom. Mungu amekasirika sana kwa sababu ya Kanisa la Tanzania limeacha njia yake na kuacha wajibu wake kama nuru na chumvi ya dunia! Badala yake limekuwa likitegemea zaidi misaada toka kwa viongozi wa kisiasa kuliko Mungu! Giza na uozo linaigubika Tanzania bila kubagua Kanisa! Sivyo ilivyokuwa Gosheni kwenye makazi ya waebrania wakati Musa amesimama kidete kupigania uhuru wa watu wake! Mtumishi wa Mungu, omba amani kwa ajili ya nafsi yako, familia yako na nchi ya Tanzania ukiutubia uovu unaofanywa! Mwenye masikio na asikie Roho aongea na masalia ya waliokombolewa na Yesu Kristo!