UMUHIMU WA KANISA KATIKA SIASA NCHINI TANZANIA
Ndugu wana-Kanisa la Tanzania, na wana-blog wote wa SAYUNI Amani, Upendo,na Furaha atoavyo Yesu Kristo viongezwe kwenu wote daima.
(*** Hii ni makala ambayo nimeipeleka katika gazeti la Kikristo hapa Tanzania la Nyakati na pia nimeona vyema kuileta hapa katika mlima huu wa Sayuni)
Nimeguswa siku hii ya leo kusema kidogo yale Mungu aliyoyaweka katika moyo wangu kuhusu uhusiano katika ya Kanisa na siasa ya nchi hii. Nimesikia watu wengi wakitoa mawazo yao, na mimi sipo hapa kuwaponda bali natoa na mimi kile Mungu alichoweka ndani ya moyo wangu. Ni maombi yangu pia kuwa nitakachokisema hapa kitakuwa cha kuujenga mwili wa Yesu na si kuuharibu.
Ninajua watu wengi mno wamekuwa WAKISISITIZA kuwa kanisa haliruhusiwi kabisa kuchangamana/kujihusisha/kuhusika katika siasa, lakini mimi ninaamini kabisa kuwa kanisa lina sehemu yake kubwa mno katika siasa.
Ninachoamini moyoni mwangu ni kwamba kanisa lina mchango mkubwa sana katika mwelekeo wa siasa za nchi ikiwemo Tanzania. Naomba tukubaliane kwanza kwamba hali ya kisiasa ya nchi yoyote iwe mbaya au nzuri inawaathiri watu wa nchi ile wote, kanisa likiwa mmojawapo.Hali ya kisiasa ikiwa mbaya katika nchi wote tunafahamu ni nini matokeo yake,na tunajua kuwa athari zake zitalipata na kanisa pia,kama tulivyoona yaliyotokea kwa wenzetu wa Kenya.
Kutokana na hali hiyo niliyoeleza, ina maana kuwa sisi kama Kanisa tusipofanya sehemu yetu katika kushughulikia hali ya kisiasa ya nchi yetu,tutakuwa tunajiwekea makaa ya mawe vichwani mwetu au kukata tawi tulilokalia.
Kwanza kabisa,Ndugu zangu,ninachofahamu mimi ni kuwa Serikali ya nchi hii(na yoyote) inatakiwa kufanya shughuli zake kwa kufuata ushauri wa karibu sana kutoka kwa Kanisa,yaani kwa kuliangalia kanisa namna linavyofanya mambo yake,kanisa likiwa kama mwakilishi wa Mungu hapa duniani.Twaweza kuliona hili tukiangalia kwa undani safari ya wana wa Israeli kule jangwani kuelekea Kanani.Tuangalie pale walipofika katika mto Jordan.(Yoshua3 hadi 4).Tuangalie Yosh3:3;”Wakawaamuru watu wote wakisema,mtakapoliona sanduku la agano la BWANA, Mungu wenu, na makuhani walawi wakilichukua,ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata” Ninaamini kuwa wengi tunafahamu kuwa sanduku la agano ndani yake kulikuwa na ‘ushuhuda’ yaani Neno la Mungu,kwahiyo kwa sasa maana yake na Neno la Mungu.Halafu wale makuhani walawi kwa sasa ndio watumishi wa Mungu (kanisa),na Roho Mtakatifu ameweka ndani yangu yale maji ya mto Yordani kuwa tafsiri ya Hali muhimu inapopitia nchi yeyote,na kwasasa tukizungumza kuhusu hali ya kisiasa.Tukiutafsiri huo mstari hapo juu ina maanisha kuwa, watanzania(wakiwemo viongozi wa serikali) wanaambiwa kuwa “Mtakapolisikia/Kuliona Neno la Mungu, na Kanisa/watumishi wa Mungu wakilibeba (kulihubiri),ndipo ninyi mtakalifuata hilo Neno wanalolisema kuhusu siasa/uongozi” Na ukiusoma mstari wa Nne kipengele “b” kinasema kuwa “Kwa maana hamjapita njia hii bado”. Ninapenda kusisitiza kuwa inatulazimu sasa kanisa tuifute kabisa ile dhana ya kuiona siasa kama dhambi,kwani inatupeleka sisi wenyewe pabaya.Kanisa linawajibika katika siasa katika njia mbalimbali, si lazima watumishi wote tuhamie kwenye siasa,hapana. Ukiendelea kusoma kitabu hicho cha Joshua sura ya 3 na 4 zote,utaona kuwa wale makuhani waliobeba sanduku la agano walipotia miguu yao katika mto Yordani yale maji,tena mengi ya ule mto yalisimama na wale makuhani waliendelea kusimama pale ndani ya kingo za mto hadi wana wa Israel wakavuka WOTE,Ndipo Yoshua katika Yos 4 anawaamuru kuondoka.Hii ni ishara ya KUHITAJIKA KWA MAOMBI KUELEKEZWA KWA VIONGOZI NA WANASIASA.Maana yake,WOTE tuliookoka tunatakiwa kusimama katika mto Yordani(Yaani kuombea hali ya siasa ya nchi hii) mpaka hapo taifa letu litakapovuka kwa kufanikiwa katika eneo hili la siasa.Nawashauri sana ndugu zangu katika Kristo tuifanye kwa bidii njia hii moja ya kanisa kushiriki katika siasa(kuomba).Haifai kabisa sisi wapendwa kuanza kuwalaumu mafisadi na viongozi wabovu wakati tulikuwa hatuwaombei,it’s not fair,na tusipobadilika tunaweza kujuta siku moja(Ewe Mungu epusha hili)
Njia nyingine (ya pili) ya kanisa/watumishi/waliokoka kuhusika na siasa ni sisi wenyewe kuonesha mfano mzuri wa uongozi unafaa kuigwa na serikali,hiyo ni njia muhimu sana ndio maana kwenye Yoshua3:3 Mungu aliagiza taifa la Israel lifuate Neno la Mungu linalohubiriwa na Makuhani,yaani kanisa.Sisi kama kanisa tunatakiwa tuweke mfano bora,iweje tulaumu kuwa kiongozi amekaa madarakani muda mrefu sana kama kanisani tunao viongozi kama hao pia? Nakumbuka mtumishi mmoja aliwahi kuwauliza watu mahali kama ni watu wangapi makanisa yao yana miradi?Wengi sana walinyoosha mikono.Halafu akauliza, wangapi wameridhishwa na jinsi miradi hiyo inavyoendeshwa?Asilimia kubwa walionyesha kutokuridhishwa kabisa.Sasa ndugu zangu, kama sisi kanisa tutashindwa kuendesha mradi wa shs laki tano, itakuwaje tumlaumu kiongozi aliyeshindwa kutunza mabilioni ya serikali?Je hakuiga kanisani huyu?.Tumeilaumu serikali kuwa haiwajali vijana ipasavyo, je kanisa tunajali vijana, hebu tuangalie namna kanisa linavyoutunza UKWATA na vikundi vingine vya vijana mashuleni na hata makanisani,asilimia ngapi ya bajeti inawalenga vijana? Je serikali haijaiga kwetu? Hatujachelewa sana, we still have time ,let’s make the most of it, tubadilike sasa,tuoneshe mfano bora kwa wanasiasa.
Njia nyingine sasa ni hii ya UONGOZI,Nasisitiza kabisa UONGOZI, watu wamepinga sana watumishi wa Mungu kuingia katika uongozi wa kisiasa, mngejua mimi namwomba Mungu atupe viongozi waliookoka WOTE,Hakuna raha kama hiyo.Tatizo ni kwamba kanisa limejijengea mawazo kuwa siasa ni dhambi,au hata kama si dhambi, sisi watumishi wa Mungu haturuhusiwi kugusa siasa kabisa,ni rahisi kuhisi pia kuwa watu hawa huwa hawawaombei viongozi pia.Mimi ninaamini kuwa wapo watu wengi MNO katika hii nchi ambao Mungu amewapaka mafuta kuwa viongozi,ndiyo maana tukisoma habari za karama 1Wakorintho 12:28:Na Mungu akaweka wengine KATIKA KANISA,wa kwanza mitume.....manabii wa tatu waalimu kisha miujiza,kisha karama za kuponya wagonjwa,masaidiano na MAONGOZI na aina za lugha” Angalieni ndugu zangu Biblia imesema katika Kanisa kuna karama zote hizo,Tena Biblia za kiingereza (AMP) imewaita Administrators,yaani watawala/wasimamizi(viongozi)
Ni kweli kuwa si kila mtumishi amepewa kuwa kiongozi,na pia si wote wamepakwa mafuta ya uongozi wa serikali,wengine ni viongozi wa makanisa na huduma.Sina shaka kabisa kuwa wote tunafahamu Mfalme Daudi alipakwa mafuta kuiongoza Israel tena kwa miaka 40 kama mfalme,kiongozi wa nchi ile,tena tunajua kuwa Mungu alikuwa naye karibu sana akimwongoza namna ya kuiongoza ile nchi,hata katika vita alimwambia nini cha kufanya na wakashinda,na pia mwanawe Solomoni namna alivyomwomba Mungu naye akampa hekima kwa ajili ya kuwaongoza watu wake.Hebu mkumbukeni nabii Musa namna Mungu alivyomteremshia hekiama ya kuwaamua watu wake kupitia kwa mkwe wake Yethro kwenye Kutoka 18:13-26,Hebu mkumbukeni mfalme Yehoshafati wa 2Mambo ya Nyakati20 alichofanya.Alikuwa mfalme,wakavamiwa na adui,akenda kumwabudu Mungu,kisha akamwomba,Mungu akasema naye na kisha Mungu akawapigania taifa zima, hebu mkumbukeni mfalme Hezekia kwenye 2Walme18&19,walitishiwa kuvamiwa,tena kwa barua na ujumbe wa watu maalumu kutoka kwa Senakerib,yeye Hezekiah akawahi kumwonesha Mungu,na Mungu akawapigania na kuwaokoa.
Ninawasihi wale watumishi ambao wanajua Mungu amewapaka mafuta kuongoza nchi hii,wajifanye tayari kushika nafasi hizo.Ninaomba tena kanisa tubadilishe kabisa mtazamo huo,mnafahamu ndugu zangu,Kwa sababu kanisa limekuwa likiona kuwa halina uhusiano na siasa,limekuwa likiwalea wakristo,vijana katika namna ambayo haiwaandai kuwa viongozi wa nchi hii,matokeo yake wale vijana wakikua wanapewa uongozi,lakini kwa sababu kanisa halijawaandaa kuwa viongozi,wanafanya mambo wanayoyafanya halafu walezi wao (kanisa) wanajiunga kuwalaumu,wote si tunafahamu ni viongozi wengi ambao hawaongozi vizuri sasa ni wakristo,na hata kwenye sherehe zetu huwa tunawaalika?
Naamini wengi wetu tumewahi kusikia tetesi za kuhusishwa kwa viongozi wetu na mambo ambayo hayampendezi Mungu,je tungekuwa na viongozi waliookoka haya yangepitia wapi?Nadhani mnaamini kuwa kitendo cha kuvunjwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi yetu na Israel kimetuletea mabaya sana, je tungekuwa na viongozi waliookoka yangetufika haya?Hebu angalieni ile hekima Mungu aliyompa Mfalme Solomoni akaitumia kuamua kesi ya wanawake wale katika 1Wafalme3:16-28, je tungekuwa na viongozi waliookoka katika nchi yetu, ndugu zangu mikataba feki ingepitia wapi,huku tuna viongozi waliokoka na kanisa linawaombea mchana na usiku???Habari ya kuiingiza nchi kwenye IOC ingepitia wapi TUKISHIKA ZAMU ZETU?Jambo la Mahakama ya kadhi lingeanzia wapi?
Narudia kusema tena kuwa mimi simlaumu mtu,maana na mimi mwenyewe nipo ndani ya kanisa,lakini naweka changamoto hii kwa kanisa na wachungaji,wainjilisti na maaskofu wetu,tubadilike sasa,tushike zamu zetu katika siasa,Tuwaombee viongozi na wanasiasa,tuoneshe mfano bora na tuingie katika uongozi wa serikali(kama Mungu amekuita kwa ajili hiyo).Tukiendelea kukaa pembeni na kutazama,shetani atakuja saa tumelala,atawavuruga viongozi na watafanya mambo ambayo yatakuja kutudhuru sisi wenyewe kanisa.Tusikubali kukaa pembeni halafu tumwachie ibilisi aje na kupanda mbegu zake mbaya kwa wanasiasa.Si mnakumbuka kitu ambacho Mordekai alimwonya Nabii Esta kwenye Esta 4:12-14. Nasisitiza pia kanisa litie mkazo katika malezi ya vijana kuanzia ngazi ya chini,kuwalea kwa namna ambayo itawaandaa kuwa viongozi wazuri huko baadaye.
Kwa mfano tusipokuwa na vijana waliookoka wanaosomea sheria, je shetani hatawatumia wengine kutunga na kupitisha sheria ambazo ni kinyume na mapenzi ya Mungu katika nchi hii? Tusipokuwa na vijana waliookoka wanaosomea udaktari tutaweza kuwapata madaktari kama wale wakunga waliokuwa wakiwasaidia wanawake wa ki-Israel kujifungua wakati wa kuzaliwa Nabii Musa?
Lakini njia nyingine ya kanisa kuhusika katika siasa ni sisi watumishi wa Mungu KUWASHAURI viongozi.Ni wajibu wetu sisi kama watu tuliojazwa Roho Mtakatifu wa Mungu,watu tuliopewa kusema na kusikia kutoka kwa Mungu,kuwashauri viongozi wa serikali kile ambacho Mungu anatuambia sisi watumishi wa Mungu.Hiyo ni sehemu yetu na sisi na haifai kuikwepa kabisa.Natumaini wote tunajua kuwa kuongoza serikali si kazi rahisi hata kidogo,ni kazi nzito,hivyo kwa mfano kikitokea kitu kizito/kigumu hapa Tanzania ni lazima sisi makuhani tukae katika zamu zetu,twende kwa Mungu tukamuulize hapa tufanye nini? Atakachosema tuje kuwaambia viongozi wetu,hii ni muhimu.Hebu kumbukeni wakati ule wa Farao wa Misri na Yusufu,wakati Mungu alipomwonesha Yusufu miaka saba ya njaa iliyokuwa mbele ya taifa la Misri (Mwanzo 41:1-57),kisha akamwambia na kitu cha kufanya,(akamwambia waweke akiba kwa miaka saba),kisha Yusufu akamshauri Farao cha kufanya,na Farao akaamua kumteua kuwa waziri mkuu. Naona kama tungekuwa tumeshika zamu zetu vizuri,Mungu angesema nasi kuhusu ule ukame wa mwaka 2006 mapema kabla haujatokea,halafu angetuambia tujiandae vipi kuukabili,na nina uhakika kabisa UFISADI WA RICHMOND USINGETUPATA WATANZANIA,maana tungekuwa tumeshaandaliwa na Mungu mapema. Nawatia moyo tuifanye hii zamu yetu.
Ni wazi kabisa kuwa hali ya kisiasa ya Tanzania inashikiliwa na waombaji,nami nichukue nafasi hii kuwatia moyo katika Jina la Yesu,tukazaneni kutubu na kuomba kwa ajili ya eneo la siasa ,uchumi, amani na mambo mengine kwa ajili ya nchi yetu, Mungu aliyetuumba atatulipa kwa wakati tusipozimia roho.
Kwa moyo wangu wa dhati namrudishia Mungu atawalaye bila mwisho utukufu wote,wote kabisa.
Mungu awajaze nguvu zake kwa kusudi lake.
Frank Lema
www.lema.or.tz
savedlema@yahoo.com
Arusha.
1 comment:
Ubarikiwe mtumishi umenena vyema na sawa.Tatizo ni kuwa hao watakaoingia kwenye siasa hawatakiwi kucompromise na wenzao wanaoenda kinyume na uadilifu.Problem je utapita wapi bila kutoa rushwa ili uwe kiongozi???naamini na na nakubali uliyosema.NADHANI NJIA NZURI NI KUPIGA VITA VYA MBALI VITA VITAKATIFU, KUSEMA KUKARIPIA KUONYA BILA KUOGOPA MAPAK PALE VIONGOZI WA SERIKALI NA VYAMA WATAKAPOFIKIA HATUA YA KULIOGOPA KANISA THEN KUTOKA HAPO TUTA KUWA NA AMANI VIONGOZI WETU AU KANISA KUJITOSA MOJA KWA MOJA KWENYE SIASA KIASI CHA KUCHUKUA HATA UONGOZI WA NCHI, HII NI STRATEGY YA KUFIKI APALE UNAPOSEMA.WACHUNGAJI MAASKOFU WAAMKE SASA.ni maoni yangu na nitapublish kuunga mkono hoja yako na ikipidi LEMA tuanze wenyewe.nashangaa wanaojiita walokole wanashindwa nguvu na kanisa la katoliki angalau huwa wanasema.
Kalenge-Canada
Post a Comment