Sunday, March 16, 2008

Wakristo muwathamini wafanyakazi wa ndani -Bartomayo hakuwa kipofu

Nawasalimu wote kwa jina la Bwana Yesu!, Serikali hivi karibuni imetoa tamko au agizo la kupandisha mishahara kwa watumishi wa ndani na sekta zingine binafsi.Agizo hili limekuja huku kukiwa na malalamiko mengi sana ya miaka mingi juu ya jinsi gani ndugu hawa wanavyotendewa na moja ya watu wanaowaonea,kuwatukana,kuwafanyisha kazi ngumu,kuwalipa kidogo au kutowalipa kabisa na wengi wa hawa waoneaji ni wakristo, nimetumia neno la wakristo kwa maana ya wale waliojitangaza na kuonekana katika jamii ni wafuasi wa Yesu,pengine kwa lugha yangu ili niwatofautishe na wakristo jina basi hawa watu niwaite waliozaliwa mara ya pili au walokole au waongofu. Mambo na jinsi wanayochukuliwa wafanyakazi wa ndani walokole wengi limewashinda mimi nikiwa na ushahidi niliouona kwa macho yangu achilia mbali kusimuliwa.’’Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu na vyumba vyake kwa udhalimu.Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira wala hampi mshahara wake’’Yeremia 22:13.

Hivi tunafikiri tukitoa pepo na kuhubiri injili na kufanya mambo yote yawapasayo watauwa huku nyumba zetu tukifanya uonevu mkubwa tutapona hukumu? ‘’Nami nitawakaribieni ili kuhukumu nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi,wazinzi,waapao uongo;Na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa,kwa ajili ya mshahara wake’’ Malaki 3:5.Aibu gani hii kuwekwa kundi moja na wachawi na wazinzi, hebu fukiri mchungaji,askofu mshirika? Hivi tunasubiri serikali itueleze kuwa tupandishe mishahara kwa hesabu za serikali huyu mtu inabidi alipwe 65,000 akikatwa kama anaishi kwako itabaki 20,500, wangapi walikuwa wanatoa hiyo? Au je hata hii inatosha? Kama wewe kazini unalipwa NSSF je huyu? Kwa sababu masikini? Kuna mtumishi mmoja alikuwa anasema kwa kutamba , eti namsaidia kwa sababu ana shida! Fikiria huyu mchungaji!

Hivi Farao anatushinda? ‘’Nami nitakulipa mshahara wako’’ Kutoka 2:9, Au Labani aliyeongeza mshahara angalau mara kumi kwa yakobo katika kipindi chote cha ukaaji wake Mwanzo 31:41,Mwanzo 30:28.? .Je leo wakiambiwa nao waanze kufanya kazi kwa kudai masaa ya ziada!

Akina baba tunaweza kujitetea kuwa akina mama ndio wanahusika na wafanya kazi wa ndani, kama,Utetezi uleule wa Adamu baada ya Eva kula tunda, hivi alivyojitetea alipona?.

Nchi zilizoendelea mfanyakazi wa ndani unaogopa kumuajiri kwa sababu ni gharama! Mchango wa wafanyakazi wa ndani ni mkubwa sana katika ujenzi wa familia,kanisa na taifa, ndio sehemu ambayo hali zetu za uchumi na baraka zitakuwa imara endapo unamjali kama binadamu.Imefikia hatua mtu aliyeokoka kuamini kuwa mfanyakazi wa ndani hawezi kuolewa au kuoa msomi!,kuvaa nguo nzuri hata kula pamoja kama ndugu.Tunadanganya watu kuwa hawa ni sehemu ya familia huku hatutekelezi mambo ya muhimu kwao.Namshukuru alinifungua mapema!

Ikumbukwe kuwa, thamani ya mtu haipo katika kuwa na magari,nyumba elimu na mali nyingi, thamani ya mtu iko katika kuonyesha upendo kwa watu wengine pamoja na kuwajali,Wazungu wana tabia ya kupenda wanyama hata kuwalipia bima za matibabu, sembuse kumpenda mwanadamu mwenzao.Mbele za Mungu tuko sawa kabisa, Yesu alitupenda pasipo sababu yoyote iliyomvutia yeye atupende hata akafa kwa ajili yetu. Wakristo tuwe na tabia ya kuwaangalia watu KAMA MUNGU ANAVYOWAANGALIA.Hawa ni watu ambao wengine walileta hata ukombozi kwa mataifa yao na wakuu wao(Ester).Hili wazo langu halitetei kuwa wanaweza kuwa wengi wao wanamatatizo.lakini kabla ya kutupa lawama lazima tuangalie tumewajibika kwa kiasi gani.Kuwajibika huku ni pamoja na kuwaza kuwa ataishi maisha gani baadae kwani hatazeekea kwako!.Usije ukajitetea kipato kidogo, kwanza kama tunaamini sisi sio maskini matendo yetu yaeleze kwani ndio imani.Pili kama unakipato kidogo utaishi kulingana nacho na upendo utuonyesha kulingana na hali yako.

Hivi karibuni kumezuka watanzania watumishi wa ndani kufanya vitu vya kikatili kwa watoto wa mabosi wao, sio lengo la waraka huu kuwatetea, ila ni kuangalia tatizo ni nini?? Huyuhuyu mama anayelalamika housegirl ni mkatili, ndie aliyemchukua kijijini kwa ahadi za kumsomesha, ndiye anayemtenga na hamfanyi huyu mtu kuwa sehemu ya familia, ndiye huyuhuyu hampi mshahara, ndiye huyuhuyu anayemkaripia usiku na mchana wala hakuna alama ya upendo.Hivi hawa watumishi wa ndani wangekuwa nyumbani kwa kwa baba na mama je wangefanya ukatili huo, jibu ni hapana, sasa ni kitu gani kinawafanya wawe makatili?? Kuna jambo ambalo kabla ya kuanza kutoa vibanzi na kuwalaumu tujiangalie tunavyowachukula hawa watu katika jamii.Tunawachulia kama ni watu wa chini, waliodharaulika, hawana akili hawana mbele wala nyuma.Kuna siku nilijiuliza ni kwa nini maaskari wengi wa magetini ni wakali sana, kumbe wengi wanajihisi inferior na wanajidharau kwa sababu jamii inamuona hivyo, hivyo ukali wake ni kukueleza hata ‘’mimi niko’’ .Huyu mfnyakazi wa ndani kisaikolojia akiishaona ametengwa roho ya ukatili inaingia(TUSIMPE NAFASI SHETANI).
Lakini kwa walokole ni sehemu nyingine ya kujadili kwa upana sana kiasi ambacho wengi ulokole wao ni wa makanisani sio wanavyoonyesha na kuwatendea watu hawa wa ndani.Pia hata kujadili swala lenyewe ni uthibitisho tosha kuwa tumeweka matabaka katika jamii!!!

Naomba mlokole aniambie kama kweli ni nani aliyekuwa anampa mshahara mzuri mfanyakazi wake wa ndani kiasi kikubwa angalau sio kama hiki(maana mshahara wa serikali ni sh.elfu sitini ukikata makato kama ilivyoelekeza net pay unayotakiwa umlipe ni kama 23,000), kama ulishtuka baada ya serikali kutangaza wapandishiwe mishahara,basi macho ya kiroho huna,tena inabidi mtubu.Walokole tuwe wa kwanza na kuwaza mbali sana nje ya upeo wa serikali, maana tuna macho ya kiroho.

Ni walokole wangapi wanaosema nina mfanyakazi wa ndani, naye ni sehemu ya familia, je kama sehemu ya familia umemfikira huyu mtu baada ya miaka mitano ijayo atakuwa wapi?? Kama huna wema wa kufanya hivyo na kuwaza mazuri kwa mtu anayeishi na kuwatunza watoto wako, anakupikia kila siku, je Mungu wetu ansema nini, najua mawazo ninayowawazia ni mawazo ya amani.

Hili pengine ni gumu kulipokea, kama walokole wameweka matabaka, basi hakuna mbingu, Yesu alikaa na watu wa kila aina na kamwe hakumbagua mtua.Wanafunzi wa Yesu walikuwa wanapita njia aliyokuwa anakaa Bartomayo na bado hakuna aliyewaza kumbeba wala kumpeleka kwa Yesu, mbaya zaidi hata siku ambayo Yesu alipita , wakati anaita wakamnyamazisha, akae kimya.KIPOFU HAPA HAKUWA BARTAMAYO WALIKUWA WAFUASI WA YESU, YESU ALIKUJA KWA WATU WA AINA ILE HIYO NDIYO MISHENI YAKE KUBWA!! Watumishi na walikole wengi wamesema Bartomayo alikuwa kipofu kuna mengi hatuyaoni maisha ya kila siku ili yatupe ubora ule ambao Mungu anautaka, hatuyaoni sisi ndio vipofu!! Bartamayo hana shida anaupofu wa mwili.UPOFU WA KIROHO NI MBAYA ZAIDI.

Serikali inaweza na itawabana wale wote wsiotekeleza hili,mlokole haupaswi kufuatiliwa.’’Mambo yale yaliyo mbali na yale yaendayo chini sana ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?’’Mhubiri 7:24.

Hivi ndio nionavyo
Kalenge

No comments: