Saturday, May 3, 2008

Msiwaguse Masihi wa Mungu?? (Lugha ya kujilinda??)


Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.Zaburi 105:15

Nimekuwa nikiamini sana andiko la kuwa ukiujua ukweli utakuweka huru, tunaishi katika zama ambazo biblia imetushauri tuwe wajanja kama nyoka na wapole kama ua, tunaishi katika zama ambazo ama kwa hakika aina nyingi za uovu zinapatikana katika makanisa yetu, watu ambao tulitegemea wangekuwa msaada wa kuongoza watu hasa wafikie kulijua andiko ndio wanakuwa wakwanza kupindisha maandiko kwa manufaa binafsi, nilishtuka nilipokuwa ninaabudu kanisa moja kuna mtu akasimama na kusema ‘’hata mtumishi wa Mungu akikosea hutakiwi kumfanya lolote lile kwani ni mpakwa mafuta wa Mungu na ya kuwa hata Miriam na Haruni waliadhibiwa kwa sababu walimng’ong’a na kumlaumu mtumishi wa Mungu Mussa kwa sababu alioa mkushi’’

Lakini ikumbukwe makosa ya mtumishi huyu anayetetewa ni dhahiri, na huyu aliyesimama hapa kumtetea si ya kuwa anapaswa alaumiwe bali nae ni upungufu wa kutoelewa maandiko na kutomruhusu Roho wa Mungu atawale au ni mmoja wa wale wanaonufaika na kile anachonufaika mchungaji. Kwa kisingizio cha andiko la kuwa msimguse masihi wa Mungu , na kutolea mfano Musa, na Daudi watumishi wengi wa Mungu wamefanya mambo ya ajabu makanisani kama vile makanisa ni yao na wala si ya Yesu, kuna watu wamefukuzwa makanisani, wametengwa, wameathiriwa kisaikolojia, wametishiwa watakufa! Kwa sababu wameuliza, wamekosoa,wako wachungaji waliolala na waumini wao, wasiulizwe eti! wako ambao utendaji wao wa udhihirisho wa Roho ni wa ajabu sio wa Roho wa Mungu bali roho za ajabu ajabu, wako walio na wanaowachagulia waumini wao mke au mme wengine ndoa zinavunjika na kwa kweli wanaishi katika huathiriwa wa ndoa kama Bahati Bukuku anavyoimba nyingi zimevunjika!! Wako waliofanya utapeli wa mali za kanisa na kuzifanya zao, wako waliozuia vijana wao wasioane kisa mchungaji hampendi kijana au binti na wala sio kumuuliza Mungu, viko vituko vingi ambavyo vikiandikwa nafasi haitoshi wala muda haupo, lakini katika makanisa ambayo yalikosa demokrasia ya Mungu walikuwa Roman Catholic (siyo sasa) hapo zamani lakini hali hii inajirudia kwa mlango tena hasa kwenye makanisa ya kilokole, ambapo wale wachungaji wa kiroho wanaowaongoza waliojazwa Roho wanaogopa maswali pengine ya kiroho, wanaogopa changamoto, wanaogopa kuonywa maana ni wakubwa kuliko Petro aliyeonywa na Paulo, wanaogopa kuna wachungaji wamewaumiza mno waumini wao kisa ‘’Msimguse masihi wa Mungu’’



Baada ya yule mtumishi wa Mungu ambaye ni msomi kutetea machafu aliyofanya mchungaji nikapata wakati mzuri wa kuujua ukweli, sio kuwa nina mlaumu aliyemtetea mchungaji kwa kwenda kinyume na maandiko labda hajui, japo kutokujua kiMungu bado adhabu yake ni kuangamia, kwani anasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.WAKATI mwafrika mlokole anasema msiwaguse masihi wa Mungu mtangamizwa na kuadhibiwa, wazungu wabaguzi wa rangi nao wanasema kwa Miriam na Haruni waliadhibiwa kwa sababu tu Musa alikuwa mpakwa mafuta wa Mungu lakini Musa naye aliadhibiwa kwa sababu hakuiona kaanani,kwa hiyo wazungu wasiwaoe watu weusi!!. kumbuka siri ya kwa nini Musa hakuingia kaanani bado kila mtu anatoa sababu zake.

Kuna haja ya kujua maandiko, tumeipunguza biblia na kuona ni kitabu cha kusoma wakati fulani tu, tena kwa mazoea, wala si kwa kusoma kwa lengo la siku hiyo au wakati huo unaposoma kuhakikisha Mungu anaongeza kitu. Kuna hatari sana ya kizazi hiki kuishi kwa maandiko yale yale na tafsiri ile ile uliyoipata miaka 10(sio makosa), iliyopita!! Andiko la Mungu ni hai linafanya kazi kila siku chini ya uongozi wa Roho, unapata tafsiri mpya nzuri zinazomjenga na kumtengeza mtu kulingana na hitaji lake, mstari mmoja unaweza ukawa na maana nyingi lakini zote zenye lengo la kulinda utakatifu wa Mungu.huku tafsiri za zamani zikiwa tayari tunazifanyia kazi na kuziishia maana raha ya neno ni kuishi kama lisemavyo na sio kama ulivyokariri!

Kama kuna mwalimu ambaye aliulizwa maswali mengi basi hakuna kama Yesu, aliulizwa mpaka maswali ambayo wachungaji wengi leo aidha wanayakwepa au kukataa achilia mbali kuwa wanaulizwa na waumini wao, Yesu aliulizwa hata na wasiokuwa wanampenda!!

Nilianza kujiuliza maswali mengi na moja ni ‘kinga’ waliyonayo wachungaji mbona Mungu hana upendeleo?? Kwani hii imekuwa katiba ya kuwa watu fulani viongozi wa Tanzania hata wakifanya makosa wana kinga hawawezi kushtakiwa mpaka kinga hiyo iondolewe, huku mataifa mengine mtu yeyote akifanya kosa anashtakiwa! ‘’Petro akafumbua kinywa chake akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo’’Matendo 10:34. Ninaamini maneno ya Mungu huwa hayana walakini wala matatizo ila watu kwa akili zao na manufaa yao wamegeuza maneno mengine kuendana na wao wanavyotaka, wako wanaosema pombe sio dhambi, wako wanaoweza kuoa wake wengi wakisema mbona fulani na fulani walifanya hivyo, wako wanaofanya vituko vingi sana hili hali kila mmoja ameweka viwango vyake na wala si viwango vya Mungu. Huwa nawaambia watu fikiria Yesu amekuja na akakaa siku mbili tu labda ikulu halafu akasema atafanya ziara kila nyumba na makanisa! watu wengine hawatakuwa tayari kumkaribisha! Wengine watafanya shauri auawe tena, kwani atakuja kuwaaribia dili zao na biashara zao, wengi watahaha kama watu Fulani ambao huwa wanahaha pale rais anaposema anaenda kuwatembelea, nakumbuka zamani nilipokuwa shule ya msingi tulikuwa tunapaka matofali rangi nyeupe au kwa majivu pale afisa elimu anapokuja kututembelea , usiulize kama mkuu wa wilaya anakuja kutembelea au rais !! siku mbili hamuingii darasani!Andiko hili la zaburi 105:15 linajieleza na kujifunua kwa namna nyingi.


Waalimu au waabudu wa andiko hili wameshindwa kutofautisha kati ya wapakwa mafuta wa agano la kale na wale wa wa agano jipya , wakati wapakwa mafuta wa agano la kale walikuwa ni mmoja mmoja (Isaiah 61:1; 1 Samuel 26:9-11; 2 Samuel 22:51; 2 Chronicles 6:42), Agano jipya linasemaje, je siku hizi watu fulani ndio wana upako kuliko wengine? ‘’Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo’’ 1petro 2:5, Nani anaambiwa hapa kuwa wamejengwa kuwa nyumba ya Roho? Je si tunaambiwa tena kuwa miili yetu ni hekalu la Roho mtakatifu?? Je ili andiko linawabagua kati ya wachungaji na wasio wachungaji? Tena biblia inathibitisha kuwa Yesu ndiye mzaliwa wa kwanza tena ndiye Kuhani mkuu nasi tu makuhani ‘’Bali ninvi ni mzao mteuli. Ukuhani wa kifalme, taifa takatifu.watu wa-milki va Mungu mpate kutangaza fadhili zake yeye alivewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu’’ 1 petro 2:9. nani anaambiwa hapa? Je Roho mtakatifu alishuka kwa watu wachache tu ambao ni wachungaji? Nani amesema kuwa agano jipya wachungaji wana upako zaidi ya waumini.

Dhana hii imesababisha wachungaji wengi kuwaonea waumini wao, kujikweza na baadae kuanguka machoni pa Mungu, japo wanakuwa na majina yaliyo hai lakini tayari wengi wao wamepotea na wataenda kuzimu, MAKANISA YAMEJAA WAUMINI ‘’DORMANT’’ WAUMINI WALIOMEZESHWA SUMU KUWA MCHUNGAJI PEKEE NDIYE MWENYE UPAKO, makanisa mengi yana waumini wasiomtumikia Mungu, wasioweza kuomba, kuombea wagonjwa, wasioeneza injili ya Mungu, wasiofanya chochote kwani mawazo yao yamedumaa, na wachungaji wengi wanafurahia hali hii, kuwa na mshirika miaka kumi kanisani asiyeweza kufanya lolote wala hutaki akue kiroho kwani ataondoka, sadaka atapata wapi?? Akifungua tawi anaogopa kwani moto wake wa kiroho anaweza akavuta waumini wake, ndiyo tumebaki na kanisa lisilokua lenye watu wanaosema wameokoka wengi kwa fasheni, waumini ambao wako kama kondoo wasioweza kuuliza lolote kwani wanaogopa kumuumiza mpakwa mafuta wa Mungu,waumini waliotayari kuambiwa Yesu anakuja tarehe 30 na waende kumpokea porini, huku walokole wengi wakiwalaumu hao wengine wamesahau kuwa hata katika makanisa yao wako hivyo hivyo ila viwango vya ujinga wa kiroho vimetofautiana najiuliza hivi Tanzania tungekuwa na akina Kulola mia moja tungekuwa wapi? Achilia mbali kuwa hata yeye mwenyewe ameshindwa kumtoa kama yeye!.Makanisa yamejaa ukabila, ubaguzi, wenye hela ndio wanatawala makanisa achilia mbali kama pia ni watenda dhambi ili mradi sadaka ije.


Au hakuna ushaidi wa kupakwa mafuta kwa watu wote wa agano jipya?? ‘’Basi yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo na kututia mafuta ni Mungu’’2 korinto 1:21, Biblia inazidi kuthibitisha kuwa sisi wote tuko sawa ‘’Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja,kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja’’ 1 korinto 12:13. Enyi wachungaji, manabii, wainjilisti, walimu, n.k kujiona kuwa mna upako zaidi si kwenda kinyume na Mungu?, na je si ndio sababu ya kudumaza waumini wengi kiroho??, mmeiua dhana ya kuwa sisi sote ni viungo na kila kimoja kinamanufaa yake mwilini, na tunategemeana je watumishi wa Mungu hawategemei viungo vingine ndani ya kanisa?? Kama wachungaji hamtegemei viungo vingine basi wengi mna KASORO, maana viungo vingine viliwekwa viwakune, viwaogeshe, viwasugue, viwakumbushe, viwaonye,viwasafishe, viwape chakula(hiki mnakipenda sana), je kuna haki ya mtumishi wa Mungu fulani kujiona ana haki sana(kiungo yeye ni bora sana kuliko vingine??) kuliko waumini wengine?? Hata kama anafanya makosa? Ni kinyume na neno la Mungu Rumi 12;4-6 inasema Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Andiko linamalizia kusema kila mmoja ana karama yake kanisani!! MUNGU HANA WAFUASI WAKUBWA WALA MAALUM. Halafu wengine sio maalum

Sio kuwa kutoa pepo na miujiza ndiyo hamna kasoro wala hamwezi kuulizwa pale tunapokuwa na wasiwasi, 1 Yohana 4:1 inasema tuzijaribu kila Roho, hata kama jana nilikuona ukitoa pepo kwa jina la Yesu, lakini leo nina wasiwasi kwa nini nisiulize?? Mbona Sauli alikuwa mpakwa mafuta wa Mungu na baadae akapotea njia?, na pia sijuia ni lini na wakati gani umewafuata wamataifa kwa hiyo umeshakatwa nywele kama Samson? .” A. A. Allen alikuwa mlevi ambaye miujiza ilitokea kwenye mkutano wake,, Jimmy Swaggart mnunuaji wanawake wanaojiuza, Jim Bakker mwizi na mzinzi, Larry Lea alikuwa mwongo, and Robert Tilton tapeli.sijawasema watanzania, wala mataifa mengine hao ni wamarekani tu, miujiza ilitendeka katika mikutano yao, siwahukumu wala kuwasema vibaya . Wengine wanapoanguka ni wakati mazuri wa wale mliosimama kujua ni kwa nini, wengine hawakukubali maonyo, hawakutaka kusikia kwani wana upako!!, naamini pengine wasomao na wakajigundua kuwa wamekosea ni wakati mzuri wa kujirudi kwani naamini nina Roho wa Mungu, lakini nachelea usije ukawa ni mmoja wa walioanguka na hawajui kuwa wameanguka! Pale unapoona wewe ni mtakatifu huku ukidharau viungo vingine visikuulize wewe nani na jinsi unavyotenda utumishi wako ndio mwanzo wa maangamizi, wangapi agano la kale walikataa maonyo ya manabii na wakaangamia na upako wao?? Watumishi wengi wamejiinua kamwe hawaishi maisha aliyoishi Yesu sisemi Yesu aje mbagala au msasani sisemi Yesu apande daladala kama wewe, Roho yuleyule wa Yesu ndiye huyuhuyu wa sasa, habadiliki wala hana fasheni YEYE ni Mwanzo na Mwisho. Hana wakati andiko hili cha ajabu limetawala sana miaka ya tisini kuwa usimguse masihi wa Mungu hata kama anafanya ya kishetani na yasiyotambulika mbinguni.Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.Zaburi 105:15

Nilitegemea andiko hili wale walioenda shule za biblia wangetusaidia tatizo wengi tuna mawazo wanaotakiwa kwenda shule za biblia ni wale wachungaji tu!! Ni muhimu kwa wote na ikiwezekana shule zisogezwe karibu sana na walipo watu kila kanisa lifanye hivi, kuna makanisa kama winners Chapel(siabudu huko), wao bible school ni kwa kila mtu wala sio wachungaji tu, tumeushusha ulokole na kuonekana ni dini na ina matabaka ndani yake, sijui kama kuna mchungaji jasiri anayeweza kusema nimefungua makanisa mengi sana, kuna mwingine akifungua matawi mawili basi ndiyo mahubiri ya miaka 20!

Lakini Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.Zaburi 105:15 ina maana gani hasa kimaandiko na kitafsiri?? Kiebrania hili andiko linasomeka hivi ‘’ naga` mashiyach nabiy' ra`a`, na matamshi yake ni naw-gah' maw-shee'-akh naw-bee' raw-ah' wakati biblia tunazosoma zimetafiriwa moja kwa moja toka kiingereza ambacho kinasema ‘’Touch Not Mine Anointed’. Msiwaguse- Naga(naw-gah’) tafsiri sahihi ni piga, angusha, na siyo gusa au touch, hili ni tatizo la sehemu nyingi katika biblia ambayo haina maana kuwa biblia ina mapungufu hapana, iko palepale na iko sahihi, Jamani Mungu ni mwema wala akili zake hazichunguziki unafikiri alikuwa hajui kuwa matatizo ya tafsiri yatatokea tunaye mwalimu wa ajabu –ROHO anatufundisha na kutufunulia siri nzito. kwa maneno na tafsiri sahihi.Naga ni piga, ndugu usimpige wala kumuumiza mtumishi yeyote wa Mungu yaani anayesema ameokoka anayeishi maisha matakatifu, maana kufanya hivyo ni kugusa mboni ya jicho la Mungu. Nimeona watu wengi waliowapiga wachungaji waliosimama kiroho wakifa ghafla maana wanatimiza andiko, na hii sitoi mfano huu ili kuwapa upendeleo wachungaji kwani wako wanaokaa magotini na kumtafuta Mungu na ndipo wanapokuwa na nguvu, hii haimzuii mtu yeyote kumtafuta Mungu na akawa na upako zaidi ya mchungaji wake(ila hatuna vipimo vya upako ila tuna tofauti ya karama), lakini pia hatoi kibali kuwa kwa sababu unakaa magotini mwa Mungu basi uwadharau wengine na kuwaona hawana thamani kwa Mungu.

Tumeona maana ya neno gusa asili yake ni NAGA ikimaanisha kupiga na sio kuuliza maswali, kukosoa, kuonya kama wengi wa wachungaji wasivyopenda iwe.

Daudi aliposema msiguse masihi wa Mungu alisema sentensi hiyo 1 samwel 26:3-11, akiwa na kisu askari mmoja akamwambia muue Sauli Daudi akasema msiguse masihi wa Mungu akimaanisha kumpiga kumdhuru kimwili, mstari wa 17-24 Daudi anamwambia Sauli Mungu alikutia mikononi mwangu lakini sijakugusa hakuwa na maana kumgusa mwili, kumbuka alikata kipande cha vazi la Sauli, tena anamlaumu Abneri mlinzi wa Sauli kuwa anafaa auawe kwa sababu ameshindwa kumlinda mfalme.

Yule muameleki alirudi na kumuambia Daudi kuwa nimemuua mpakwa mafuta wa Mungu 2 Samwel 1: 13-16. Biblia inaonyesha wazi neno hili lilimaanisha kumuumiza kimwili


Sasa swali je Kwa nini Musa baada ya kumuoa mkushi ndugu zake Miriam na Haruni waliadhibiwa kwa sababu ya kumlaumu??

Kweli Haruni na Miriam walifanya makosa ambayo wengi huwa wanafanya, Hesabu 12:1, biblia inasema Miriam na Haroni walimnung’unikia Musa kwa sababu ya mwanamke mkushi aliyekuwa ameoa, kwa sababu ameoa mkushi. Tafsiri zingine potofu za kiingereza zinasema kuwa mwanamke wa kiethiopia, hapa uwe mwangalifu, mkushi ni kizazi cha kushi, kumbuka Nuhu alikuwa na watoto watatu Shemu Hamu na Yafeti,Mwanzo 10:6.inaeleza watoto wa Hamu walikuwa Kushi, Mizraimu na Puti na kanaani, Nuhu na wanawe walikuwa weupe hii haina shaka, watoto wao walikuwa bila shaka weupe, Mizraimu maana yake ni misri, kumbuka wamisri wote walikuwa weupe wala hakukuwa na kizazi cheusi zaidi ya weusi waliokuwa watumwa tena wakifanya kazi wakiwa na minyororo, kwa hiyo hatutarajii huyu mke wa Musa alitoka Kushi ya Ethiopia wala hakuna andiko linalosema Musa alienda Ethiopia, huyu Mkushi sasa alitoka wapi?? Kipindi cha biblia kulikuwa na kushi mbili ya Afrika ambayo ni Ethiopia ya sasa, kulikuwa na kushi nyingine Mashariki mwa Mesopotamia ambayo kuna wakati ilikuwa ni milki ya wababiloni hawa nao pia hawakuwa weusi.Sasa mke wa Musa anatoka wapi?? Musa hakwenda Ethiopia , Unakumbuka Musa alikimbilia Midiani baada ya kumuua mmisri?? Alipofika Midian akapewa mke Reuel jina hili likiwa na maana ya rafiki wa Mungu. wengine wanadai labda ndiye huyu.

Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. Akamzalia Zimrani, Na Yokshani, Na Medani, Na Midiani, Na Ishbaki, na Sua. Mwanzo 251-2: Wakati kuna uwezekano mkubwa kuwa huyu mke wake hakuwa na rangi sawa na akina Miriam alikuwa mweusi pengine sio kama mimi, lakini bado kuna maswali mengi katika hili.Haitatusadia sana kujua alitoka wapi lakini tunaona matokeo na aina ya adhabu ya Mungu kwa Miriam, ‘’Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama yu mwenye ukoma’’Hesabu 12: 10.Miriam na Haruni waliringia ngozi yao, na Mungu akawapa adhabu za ngozi!! Walikuwa wabaguzi Mungu aliposema wasio watu wamataifa mengine hakumaanisha kwa sababu ya rangi bali kwa sababu ya imani yao, ndio maana tunaona Ruthu pamoja na kuwa mmataifa lakini kwa sababu alikuwa anamuamini Mungu wa Naomi akaolewa na Ruth na kizazi cha Yesu kimetokea hapo, yaani katika moja ya bibi zake Yesu mmoja alikuwa sio mwisrael akimaanisha Yesu alikuja na akitayarishwa na Mungu kwa watu wote duniani! Lingine Miriam na Haruni hawakujua pamoja na rangi tofauti ya Mkushi huyo lakini alikuwa ni wa taifa lao chanzo ni Ibrahimu.Walokole wangapi tunabaguana kwa sababu ya hali zetu, mali, makabila makanisa, historia n.k kumbe sisi wote wa Mungu?

Kwa hiyo, Musa hakufanya kosa lolote ni ujinga wa Miriam na Haruni wala sio kisingizio eti kwa sababu Musa alifanya makosa basi mchungaji wa leo naye anafanya kosa akitoa kisingizio cha Musa. MUSA HAKUFANYA KOSA. Wala hakuwa huko mliko nyie kwa kusingizia mna kinga ya Mungu.Wakati Mussa anawaombea msamaha Haruni na Miriam na wakatakaswa leo tuna wachungaji wengi wanalaani waumini wao na wachungaji wa makanisa jirani, bila kujua hao ni Israel hivyo wanajilaani wenyewe!!


Matendo ya mitume inaeleza wazi jinsi watumishi walivyoonyana, walivyokaripiana na bado wakapendana.

Yesu anasemaje?? Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye Mamlaka juu Yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; Bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.Luka 22:25-27. Hali ya kutafsiri maneno ya Mungu ili yatupe manufaa yaetu binafsi ndiyo yamelifikisha kanisa la Mungu hapa lilipo. Tuna makanisa ambayo hayana sura ya Mungu aliye mmoja, mwenye tabia moja. Wachungaji nimethibitisha jinsi ambavyo wengi wenu msivyokuwa na maisha ya mvuto, mmewakwaza wengi na wamepotea na hawataki kurudi mmewarudisha watu nyuma, hamjatengeza familia ya Mungu ambayo mnaweza mkaka chini mkaulizana, mkaonyana kwa upendo wa undugu, kila mmoja anajiona sahihi huku kunawezekano hakuna hata mmoja sahihi!.

Yesu aliulizwa nani wewe usiulizwe, Yesu alijibu wala hakumtisha mtu alijibu kimaandiko watu wakafurahi Yesu angewajibu kwa vitisho na mikwara ‘’unanijua wewe utaniona nitakupeleka motoni’’ Yesu angeweka visasi nani angepona, wale waliomuuliza maswali hata tunayoyaona ya kijinga leo ndio wale waliookoka na kutangaza injili yake kwa Nguvu.Tuamke sasa tumeshapoteza sura ya Mungu hatuna waberoya leo kwani wanaogopa kuwa wakiuliza maswali wataambiwa utakufa.

Kuna maswali mengi ya kuuliza imani yetu tunaweza tukayatatua kwa upendo wa kukaa chini kujadili,hili litasababisha mlipuko wa watu kupenda kusoma biblia, kujiamini, kila mtu atajiona ni wakili wa siri za Mungu, kila mtu atakuwa macho akikosea anaonywa kwa hekima sio naupole kama biblia inavyosema.ikumbukwe waolokole wengi hawasomi biblia. YESU ALICHANA PAZIA LA HEKALU. Wote tu sawa mbele za Mungu Jehovah

WAUMINI;’Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Nina nena hayo niwafedheheshe’’,1 korinto 15:34.

Kuna mambo ambayo hayahitaji Roho akufunulie unaona kabisa kwa akili hakipo, uliza ueleweshwe, usinung’unike yasije yakakupata kama ya Miriam inawezekana mchungaji yuko sahihi, na wewe hujui, lakini kumbuka lolote afanyalo mchungaji wako lazima liwepo kibiblia na Roho atakugusa, huu mchezo wa kusema nimefunuliwa na Mungu jambo fulani, lazima lithibitishwe kibiblia , ndio uhusiano na kipimo cha biblia ,Roho na mafunuo, ukiona mchungaji wako anashindwa kukujibu, anakwepa, anakuzuia, matatizo tena siyo mchungaji ni wewe!! hama haraka unapoteza muda utaishia kuuondoa na kupoteza utakatifu wako kwa manung’uniko tafuta mchungaji atakayekulea kitakatifu atakaye kukuza wokovu wako, hata ufikie kumtumikia Mungu popote pale na kwa namna yoyote ile, fikiria ni mlokole wa miaka 5 huwezi kufanya lolote.Sisemi tuwe wachungaji maana kuna walio na kansa ya mawazo wanadhani kumtumikia Mungu ni uchungaji tu, hii yote ili ulindwe na andiko kuwa’’ usiguswe’’ hata ukikosea! Na ili kujiweka sawa na kujiimarisha wachungaji wengi wameweka wapelelezi ndani ya waumini wao! Wamekuwa kama serikali za dunia hii, hao wapelelezi wako tayari kusema lolote kulinda maslahi ya wachungaji, na wengi malipo yao ni kupewa uzee wa kanisa au ushemasi hata kama hawajafikia ubora ambao biblia inaousema!

WACHUNGAJI NA WATUMISHI MLIO KWENYE MAMLAKA:’’kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.tLakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo Efeso 4:12-16.

Wote tuko sawa wote tuna upako wote tunauwezo wa kufanya lolote lile la kiMungu tukielewa na kufundishwa wote tuna Roho, Mungu mmoja, Roho mmoja, ubatizo mmoja, mbingu moja, tuko ndani ya MWILI MMOJA.Hakuna kinga kwa mchungaji mwovu.
Niko tayari kukosolewa na kufundishwa pale ambapo nakala hii imeelezwa visivyo.


Mbarikiwe

Mr. Kalenge



2 comments:

Maranatha said...

Enough to be called the sermon of the day! Bro Kelenge you have exhausted almost everything pertaining to the so called miungu watu hapa duniani.

Umenifanya nimkumbuke mtumishi mmoja toka Iringa zama hizo za IPYA alitamka wazi pasipo woga kanisani akasema: Kama wengine wanasema ni wapakwa mafuta, je sisi je tuliosalia (raia) tumepakwa maji?? Kwa wasiokuwa na masikio ya kuelewa walidhani anasengenya lakini alikuwa dhahiri kwani wachungaji wengi, tena wengi wamechukua nafasi ya miungu hapa duniani. Kule tuliko toka ndo huko tunakurudia. Nalitoka kwa Papa,ambako yeye Papa ni mkuu wa kanisa, mwakilishi wa Mungu duniani na vilevile ni mkuu wa serikali yake. Hiki ndicho kinachoonekana kulikumba kanisa la Mungu tusipokuwa makini.

Bwana atusaidie ili kutokuyarudia yale tuliyoyakataa na kufanywa watumwa kwa namna nyingine. Neno lasema "Mwana akiwaweka huru, mnakuwa huru kwelikweli" Uhuru wetu usiwe wa kuonesha ujasiri kwa kusema na kuwarudi "panzi" makanisani, bali na tuvae uso gumegume na kusimama katika haki ya Mungu kusema iliyo kweli toka moyoni, ila pia nachelea kusema HEKIMA na MAONGOZI ya ROHO MT. ni ya muhimu sana kabla ya kuchukua uamuzi wa kumuonya huyo aitwaye mtumishi wa Mungu!
Amina!

Anonymous said...

Amen mpendwa Maranatha, Mungu ashukuriwe anayetupa nguvu na uwezo wa kuyatambua haya, napenda tuwe kanisa la mfano TANZANIA na dunia nzima, .Tuanze sisi na tutakuwa na ujasiri wa kuwanyoshea wengine vidole.tuombeane safari siyo tambarare hii!!!!!!

Be blessed

Kalenge