Thursday, July 10, 2008

Kanisa la KKKT lamkana Rostam Aziz

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limesema taratibu zilikiukwa katika kumwalika Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM) kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu ya kwaya ya Usharika wa Kinondoni, Dar es Salaam Jumapili iliyopita. Taarifa ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) ambako Usharika huo upo, imesema kanisa hilo halitambui usafi wake. Katika hafla hiyo, Rostam ambaye si Mkristo, alichangia Sh milioni tano kwa ajili ya ununuzi wa seti za muziki za kwaya hiyo na jenereta yenye thamani ya Sh milioni 2.6. Taarifa hiyo inawaomba radhi waumini wake ambao huenda walikwazwa na taarifa za ugeni na matamshi ya Rostam katika Usharika wa Kinondoni, ambako alinukuliwa akiipongeza KKKT kwa kutambua usafi wake. Katibu Mkuu wa KKKT wa Dayosisi hiyo, Balozi Richard Mariki amesema katika taarifa hiyo jana kuwa katika tukio lililomhusisha Rostam, taratibu za kuwaalika wageni kwenye shughuli za kanisa hazikufuatwa na kanisa limesikitishwa na matamshi yake. “Rostam alialikwa na kikundi ambacho hakikuwa na mamlaka ya kumwalika". Alisema kutokana na ukiukwaji wa taratibu hizo, madai yaliyonukuliwa katika vyombo vya habari kwamba ugeni wa Rostam katika usharika wa Kinondoni na tafsiri ya kuwapo kwake kuwa kanisa linatambua usafi wake, si sahihi na ni madai potofu. “Msimamo wa kanisa hauruhusu usharika zake zitumike kama majukwaa ya siasa kujisafisha au kuwasafisha watuhumiwa wa ufisadi,” ilisema taarifa hiyo ya KKKT ambayo imetolewa na Halmashauri Kuu ya DMP. Katibu mkuu huyo alisema KKKT imekuwa mstari wa mbele katika kupinga na kukemea ufisadi na linaunga mkono juhudi za kutokomeza uovu. Mariki alisema kanisa litachukua tahadhari kuhakikisha kwamba jambo kama hilo halitokei tena na kusisitiza kuwa jukumu la kanisa ni kuokoa roho za watu na si kukumbatia aliodai kuwa ni “mafisadi na wala rushwa”. “DMP inapenda kuwaomba radhi waumini wote wa DMP, KKKT na wale wote wenye mapenzi mema kwa nchi yetu ambao kwa namna moja ama nyingine wamekwazwa na tukio hilo,” alisema Mariki katika taarifa hiyo. Kwa mujibu wa Mariki, juzi Halmashauri ya DMP ilifanya kikao cha dharura ambacho kilijadili taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali Jumatatu kuhusu Rostam kulipongeza kanisa hilo kwa kutambua usafi wake, licha ya mlolongo wa tuhuma na kashfa zinazoelekezwa dhidi yake. Taarifa hiyo ilieleza kuwa kama kanisa kuna taratibu za kualika wageni kwenye shughuli mbalimbali za kanisa kuanzia ngazi ya mtaa, usharika, jimbo na ofisi ya Dayosisi. Mwishoni mwa wiki iliyopita Rostam alialikwa na kwaya ya Amkeni ya Usharika wa Kinondoni kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi ambako alisema taifa liko katika wakati mgumu katika siasa na jamii na akawaomba watu watumie makanisa kulirejesha katika mstari sahihi. Alisema waumini wa dini hawamtuhumu mtu, hawamshutumu, hawapendi wenye wivu na wenye chuki, bali wanapenda haki na hivyo ni vizuri wakaitumia fursa hiyo kuliombea taifa. “Nawashukuru kwa kunialika kuwa mgeni rasmi leo hii…ni ishara kwamba mmeamua kupuuza vijimaneno na upuuzi wa vijiweni,” alisema Rostam. Haikuwa mara ya kwanza kwa Rostam kushiriki na kuchangia katika Usharika huo, kwani mwaka 2005 alichangia ujenzi wa jengo la kanisa hilo ambalo sasa linatumika kama sehemu ya Chuo Kikuu cha Tumaini.
***************************************************************

Maswali ni mengi sana kuliko majibu katika sakata hili la Rostam Aziz.

1.Hivi ni kweli imethibitishwa kisheria au kiroho kuwa Rostam Aziz fisadi?

2.Kwa nini KKKT wasirudishe sadaka hizo za Rostam Aziz na jenereta lake alilolitoa?

3.Hivi kama akialikwa mwanasiasa mwingine anayetuhumiwa kwa ufisadi KKKT bado wanaweza kutoa tamko la namna hii?(Tunajua wapo wengi wanaotuhumiwa kwa ufisaidi --epa,meremeta,tangold,kiwira,richmond n.k)

4.Hivi dhambi ya kuishupalia ni hii tu ya ufisadi?

5.mbona kuna wazinizi,walevi,wachawi,wezi na wauwaji wanaoalikwa makanisani na hata ndani ya KKKT na huwa wanatoa michango mingi sana na huwa inapokelewa kwa vifijo na nderemo.Kwa nini KKKT wasirudishe hizo nazo?

6.KKKT wamethibitisha vipi kama Rostam Aziz ni Fisadi?

7.Nani anayetakiwa kuingia kanisani? Je ni watakatifu pekee au pamoja na wenye dhambi?

8.Ni matamko mangapi ya wanasiasa yamewahi kutolewa kanisani na KKKT ika react kama hivi?

Kwa kweli maswali ni mengi sana ya kujiuliza hapa...nahisi majibu ni machache sana katika maswali haya...Nadhani imefika wakati sasa kwa makanisa kuangalia upya utaratibu wa kuwaalika wanasiasa na matajiri makanisani hata kama ni hawajampa YESU maisha yao kwa kisingizio cha changizo na kupokea mapesa...hivi hakuna wageni rasmi waliokoka wanaomjua Mungu?

Hivi kumkaribisha mlevi,mzinzi na kahaba katika madhabahu ya Mungu na kumwacha akitoa hutuba yake ni sawa kweli mbele za Mungu?Tumeshuhudia wafanyabiashara au wanasiasa wakipandishwa madhabahuni na kutoa hotuba zao mara nyingi...

Siungu mkono ufisadi ila ninasema kuwa lazima tufike kipindi tuwe tunapima mambo kabla ya kukurupuka na kutoa matamko ili kuufurahisha umma bila kujali kuwa hatutendi haki mbele za MUNGU wetu..


Mbarikiwe....

2 comments:

Anonymous said...

Mtade tuko pamoja,inafact natarajia kuandika nakala kupinga tamko la KKKT, kanisa kimekuwa siasa sasa!!!! wanafuata mambo ambayo watu wanawashauri.Yesu angefuata ushauri wa watu asingeenda kwa Zakayo waka asingeongea na mwanamke pale kisimani.

Je 2005 wakati Rostam anachangia jengo la kanisa kwa nini walizipokea hizo fedha, au hakuwa fisadi muda huo.

Na je mtu watakaye mualika atakuwa mtakatifu ???, je wana lenses kama za Mungu??

N je wanamyonyeshea kidole Rostam angekuwa amefungwa jela kwa kosa la ufisadi wangempata wapi??

N kanisa halioni kufanya hivi ni kutetea wale watu wanaowachoma moto vibaka, wanaojichukulia sheria mkononi.

NI NANI ALIYEENDA KANISANI ALIKUWA MTAKATIFU KAMA SI YESU KUTUOKOA??

Yaani hatutakiwi kukaa kimya ama sivyo theme nzima ya maana ya kanisa itapotea kwa wengi.

Lazarus Mbilinyi said...

Ni kweli viongozi wa KKKT wanahitaji busara na hekima ya Roho mtakatifu vinginevyo wanavyofanya ni kama kunasa kwenye mtego ambao shetani ameutega.
Nakubaliana na ndugu hapo juu.