Monday, July 14, 2008

KIZUNGUMKUTI BAINA YA ROSTAM AZIZ (MB) NA K.K.K.T.

Haya maoni nimeyapata kwa mtu fulani nami nimeona niyaweke hapa kuhusu sakata la Rostam Azizi (mb) na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T.). Japo ni marefu lakini huyu mtu ana ujumbe mzito ndani yake.
Mh. Rostam Aziz akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Kempsinki Jijini Dar.

Kama mtanzania awaye yeyote, nimezopekea taarifa za KKT vs Rostam kwa mtazamo wangu pia. Najua kila mtu anamtazamo wake wa kuwaz na kufikiri jinsi ya hali halisi ya mambo yalivyo.Kila kukicha neno fisadi ni neno la kawaida kabisa na tumekuwa wepesi kufuatilia habari zake usiku na mchana, sina shaka mchango wa vyombo vya habari katujuvya swala hili umetukuka. Sitashangaa pia kuona hata wasanii mbalimbali kuiliimbia hili kukubaliana kuwa awa ni adui wa taifa letu na binadamu mwingine yeyote hapa duniani.

Niliposoma habari ya Rostam kwenda kanisani kama mgeni rasmi sikushtushwa na Kusikia hivyo, hila nilishtushwa na ujasiri, shutuma zikikulemea unaweza pata magonjwa ya moyo,na simanzi nzito. Nakumbuka pale ambapo tulipokuwa watoto na tunamwimbia mtoto aliyekojoa ‘’kikojozi kakojoa na nguo kaitia moto’’ tunamalizia kindumbwendumbwe chalia..Zamani ulikuwa unazungushwa mtaani huku mzazi au mlezi wako akihakikisha unazomewa hili usirudie tena. Naona hawa mafisadi wako hivyo! Lakini kinyume na mtoto kikojozi ambaye anatembea na aidha godoro lilolowa mkojo au nguo zake. Mafisadi hawana alama yoyote ya kutuonyesha kuwa ni mafisadi..Nikitafakari kwa kina swala la KKT, ufisadi na mafisadi serikali na wananchi.Adhabu wanayopata tunaowaita mafisadi haitoshi na haiwastahili, kwa sababu na sisi hatustahili kuwahukumu jinsi inavyowastahili wahukumiwe.

KKT wanaelewa vyema tabia mbaya ya baadhi ya watanzania kujichukulia hatua mkononi ya kuchoma vibaka au wezi huku mitaani mwetu. Sio siri watanzania wengi wasio na hatia wamepoteza maisha yao. Serikali, makanisa , asasi mbali mbali za kijamii zimepiga kelele kuhusu swala hili.Na kwasababu ni tabia iliyojengeka kwa kufikiri polisi hawafanyi kazi vizuri basi wananchi ikiwemo KKT sasa inachukua hatua mkononi.Sio siri, KKT kutoa tamko la kumkataa Rostam kwa kisingizio wako mbele kwenye vita juu ya ufisadi, kwa kumuita mtu fisadi mimi siliungi mkono. walilofanya KKT inaonyesha kuwa wanaunga mkono swala la watu wote wanaoshukiwa wezi wapewe adhabu bila kuwasikiliza. Kwa namna hii,KKT wamekuwa mahakimu, waendesha mashtaka na mashahidi, ila hawajajiweka nafasi ya mtuhumiwa!, wala kuangalia upande wa pili kuwa ni kanisa.

Mtego mkubwa kuliko yote ni pale ambapo KKT inataka ituaminishe kuwa wote wanaoalikwa katika sherehe zao zinazofanana na zile wanakuwa ni watakatifu au hawana madoa yoyote yale. Na pia sitaki kuamini kuwa wote waliowahi kualikwa na watakaoalikwa basi watakuwa watakatifu!. Na kwa namna hii kikanisa tunapata picha ya ajabu ambayo hata Mungu anatushangaa kona dhambi fulani ni kubwa na nyingine ndogo.Tunapofikia kuona mwongo afadhali kuliko muuaji tunahalalisha mambo yasiyofaa kanisani.Kwani vipimo na viwango vya dhambi havipatikani katika biblia ambayo KKT wanayoitumia hakuna dhambi kubwa wala ndogo.Kwa uongo wa shetani kwa Adamu na Eva mpaka leo tunakufa!..Ili kuthibitisha kuwa dhambi zote ni sawa hakuna msahafu unaoeleza adhabu tofauti kwa dhambi tofauti.Ilichofanya KKT ni kuhalalisha dhambi zingine, ili mradi kila mmoja kama aonavyo, ndipo pale watu wanaoamini ndoa za jinsia mmoja kwao wataona ni sawa. KKT wao dhambi kubwa ya kumfukuza mtu ni ufisadi. Nasubiri kwa hamu kuona nani ataalikwa na KKT ambapo lenzi zao zitawaonyesha kuwa huyo mtakatifu.

Siamini ninaposikia kuwa kumbe haikuwa mara ya kwanza kwa Rostam Aziz kualikwa katika kanisa hilohilo.Tunataka tujue 2005 wakati Rostam anachangia ujenzi hakuwa fisadi?? (kama mnavyomuita). Na je fedha zilipokelewa ? na je leo mkitambua kuwa fedha zilikuwa za kifisadi ilikuthibitisha mnachukizwa na ufisadi basi kanisa libomolewe! Maana kama hela yake ilinunua sementi, mchanga au maji tusemeje?. Na lisiishie kubomolewa kanisa la KKT kinondoni bali makanisa yote ambayo misingi yake na fedha zake zilitoka kwa wenye dhambi.Maana sitaki kuamini kuwa wanaotoa fedha zisizo halali ni Rostam pekee! Ndipo pale katika tamko la KKT sijaona wakisema watarudisha fedha! Inabidi kuweka mashine kwenye chombo cha sadaka ambacho kitazikataa hela zisizo halali!

Tamko la kanisa linachanganya zaidi pale linapoamua kupinga ujio wa Rostam kwa sababu ya presha za wananchi juu ya ufisadi.Hii kwa KKT ni udhaifu, ni udhaifu wa ajabu kutoa maamuzi kwa sababu ya presha ya watu fulani wenye malengo mazuri ila bila mbinu nzuri juu ya ufisadi. vikitokea vikundi vya watu fulani vikawapa presha KKKT wapitishe ndoa za mashoga watakubali?. Je haikutosha kusema Rostam hatujafurahishwa na aliyoyazungumza, bila kuondoa dhana ya kuwa kanisa ni la kila mtu.Maana tunavyomwona sisi Rostam sivyo Mungu anayomwona! Kanisa inabidi lijifunze jinsi ya kujibu bila kuondoa dhana nzima ya ukristo.

Paulo mtume alikuwa muuaji! Daudi alizaa na mke wa mtu cha ajabu mtoto wa nje ndiye aliyejenga hekalu, Rahabu alikuwa kahaba ! akamzaa Boazi(Mathayo 1:5) ambapo tunapata ukoo wa Yesu!.Msingi mkubwa wa Yesu ni kuwafanya watu watoke katika hali zao za dhambi, kwa sababu wote tumefanya dhambi na tumeshindwa kuishinda dhambi tufikie hatua ya kuishinda dhambi(Ufunuo 12:11). Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi,kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema(Rumi 6:14).Na kwa sababu mpango wa Mungu hataki mtu apotee, Yesu hakusita kukutana na Zakayo mtoza ushuru maana huyu alikuwa fisadi mwingine wa kipindi hicho.Zakayo kwa kukutana na Yesu alishawishika kurudisha mara nne ya mali alizozifisadi, na zingine akawagawia maskini(Luka 19).Lakini cha ajabu Yesu alipohuzunishwa na mambo ya biashara mahekaluni hakusubiri vyama vya upinzani, wala asasi mbalimbali yeye mwenyewe aliingia na kuwafukuza wote waliofanya biashara ndani ya hekalu! Hapa ndipo tunapomwona Yesu katika upeo wa kitofauti.Hakumbagua mtu kutokana na hali zao.Ilipofika swala la kodi aliwaeleza ya Mungu mpeni Mungu ya kaisari mpe kaisari!.Katika dhana nzima hii ya Yesu na mpango wake naona kanisa liko mbali kabisa!.Kwa hiyo tamko la kanisa lilitakiwa kutokukiuka misingi ya kanisa lakini bila kuondoa vita ya ufisadi.Hapa ndipo KKT walitakiwa wakae chini na kuwaza sana.Tukiuliza ni viongozi wangapi wa KKT ambao kwa nyazfa zao walienda kwa watuhumiwa wa ufisadi angalau kuwahubiria injili.Je kumualika kwenye sherehe kama hiyo pengine kungetoa nafasi kama hiyo?.Paulo anasema ni muhimu kuchangamana na watu fulani ili kuwapata hao watu!.Kuwatenga na kutoa matamko makalikamwe hakutoi nafasi ya watu hao kubadilika.Je Rostam hapaswi kuhubiriwa?

Nachanganyikiwa zaidi pale ninapofikiri kumuita Rostam aje kuzungumza kwenye hafla ya kikristo mlitaka aongee nini??Marko? Luka?Mathayo?? Basi angeandaliwa hotuba ili aisome!Kwa maana nyingine asingesema aliyosema bado angeandamwa na watu kuwa hajasema lolote!.Pia angekaa kimya angekuwa mnafiki wa nafsi yake,watu wamekualika na kila siku unaandikwa kwenye vyombo vya habari bado ukae kimya kama hamna kitu kinachoendelea!.Yeye kisaikolojia anaumizwa na hali hii iwe kweli au si kweli. Au waliomualika ni wanafiki hawamjui Rostam??.Rostam hajawa mbaya kiasi hicho. Watanzania wengi wanataka mtu aseme ndio wafurahi!.Alilosema Rostam kama mimi ningesema amefikia pazuri(mtazamo wa kikanisa).Pale aliposema watoto wake anataka walelewe kwenye misingi mizuri ya dini hapa ni ‘’ushindi’’ wa kikanisa swala je wataenda wapi? Sio siri kiroho zaidi Roho ya Rostam ingeweza kuokolewa kama mpaka ana uwezo wa kufika kanisani lakini mmepoteza na kumrejesha sio rahisi. Yesu anasema adhabu yake ni kufungiwa jiwe shingoni atupwe baharini(Mt 18:6). Hivi mlitaka Rostam aseme nini??

Tuna nchi dhaifu kwa sababu makanisa na misikiti yetu ni dhaifu,familia ni dhaifu,kwa sababu tuna akina baba na akina mama dhaifu.Dhana nzima ya dini haifuatwi.wengi yuko dini fulani kwa sababu wazazi walikuwa dini hiyo au mazoea.Hii imepelekea kuwa na wasanii makanisani kuwa na mafisadi wa imani.Kufungisha ndoa za wajawazito, kuingia na nguo zisizo na heshima makanisani, kufanyiana fitina na kupigana makanisani,utapeli kupindisha maneno ya Mungu, hawa wote sio bora kuliko Rostam.Wale walio kwenye ile orodha ya mafisadi wamo makanisani na misikitini mwao, wengine ni vongozi makanisani! Kwa hiyo hao wote wafukuzwe! Hapa naona KKT iko mtegoni..Nilifikiri katika tamko lao watasema kuanzia sasa hakuna kwaya yoyote inayozindua albamu kumualika mtu yeyote kama mgeni rasmi. Hili siliongelei kwa sasa ila nafikiri ni wakati mzuri kwa watu wajiitao wakristo kufikiria swala la kumualika mtu mwenye hela ili atoe pesa za michango.KKT wangeanzia hapo.Maana kama hivyo basi hamna imani na kama haana imani hamumpendezi Mungu!.Amelaaniwa amtegemeaye mwanadamu!!.Nafikiri mkiomba tu kwa imani kanda zitauzika.Hili nalo linathibitisha makanisa yetu mengi ni taasisi za kibiashara na watu kukusanyikia ili wajuane maana kama uko kanisani na huna mpango wa kwenda mbinguni nachelea kusema a ni kupoteza muda na kufuga wezi ,mafisadi hawa wote wametoka makanisani na misikitini.

Kwa sababu ni KKT wametoa tamko hili,afadhali kidogo maana angekuwa ni askofu mkuu wa KKT ingekuwa hatari, naamini anabusara zake na nimjuavyo ni mlokole mzuri. Kwa wadhifa wake anakutana na viongozi wengi, siku anasimikwa walikuwapo viongozi wengi wa serikali wenye tuhuma za ufisadi. Je waliusimika ufisadi? , je asihudhurie wala kuchangamana na hao watu maana kwa kufanya hivi kunamfanya naye kuwa mmoja wa mafisadi? Si kweli. Je angekuwa raisi amehudhuria?KKT ingetoa tamko kama hilo? Mbona naye yumo katika ile orodha ya mafisadi?

Watanzania wengi tunafurahi sana kusikia na kununua habari kuhusu mafisadi. Gazeti ambalo haliandiki habari za mafisadi yanaonekana wasaliti na yale yaandikayo wanaonekana mashujaa, yote yanaweza kuwa sawa kutegemea na nini sisi tunataka, Je nikijua huyu mtu fisadi basi inatosha?? Nikimzuia asiseme popote pale huku wanakula hela walizoiba nimetatua tatizo ? Magazeti hayaandiki habari za kifisadi kama udaku, tatizo wengi wanachukulia habari hizi za ufisadi kama udaku.ukishajua fulani fisadi basi moyo wako unasuuzika! Nadhani kazi ya vyombo vya habari na baadhi ya wapinzani ni kueleza tatizo na kulitatua.Tangu habari za ufisadi zimeanza mpaka leo hatua gani zimechukuliwa? Je Rostam angekuwa jela hao wanakwaya wa amkeni wangempata wapi?. Tatizo ni mamlaka tulizo nazo nani anahusika? akina nani wako TAKUKURU wakristo na waislamu, akina nani mapolisi? Wakristo na waislamu! Mawaziri na wabunge hawa makanisa yao yapo mwezini? Hapana. Sasa tatizo liko wapi?

Nadhani wote tumekutana na mbwa wanaobweka sana, ukitishia unataka kuokota jiwe anakimbia ni kama sisi tulio wengi.Ni hodari sana kusema ufisadi hatuchukui hatua yoyote.Kuna msomi mmoja yeye anataka Rostam akusanye waandishi wa habari awaambie anavyohusika kwenye ufisadi!akikusanya waandishi wa habari na akasema basi mioyo yetu itaridhika kabisa!eti ajibu tuhuma huu mamlaka zilizowekwa kisheria kuweka usalama wa raia na watu wao zipo!.Ukiona nchi ambayo wasomi, wapinzani makanisa hayana chochote cha kufanya isipokuwa kusema ujue nchi hiyo bado sana ukombozi kupatikana, kuna watu wanasema mpaka mitume wote warudi labda tutabadilika.

Wasomi,makanisa,misikiti waliunga mkono CCM na ikashinda kwa asilimia kubwa.Vyama vya siasa vinaongezeka na vinajulikana wiki moja kabla ya uchaguzi ,ukiona watu wanawapokea kwa vigelegele watuhumiwa wa ufisadi huku wengine wakiwatetea, ukiona makanisa yako kimya hayasemi lolote juu ya ufisadi au la wanasema wakati wengine wameshasema! ujue jamii hii ina tatizo.Mapinduzi ya kifikra yanapaswa yafanywe na mtu mmoja mmoja kasha yahamie katika ngazi ya jamii na baadae kufikia hatua jukumu la mwanandamu duniani.Kuzungumza swala la ufisadi bila kuchukua hatua yoyote ni kupoteza muda.

Kila mmoja kwa nafasi yake likiwamo kanisa linapaswa lijiulize mara mbili jinsi tunavyowachagua viongozi wetu kuanzia ngazi ya mjumbe wa nyumba kumi kumi mpaka taifa, sio hapo tu makazini mashuleni, kila mahali viongozi wetu tunawapataje?.KKKT wananichekesha pale wanaposema taratibu hazikufuatwa na kwamba wao ni wakubwa zaidi kiasi kusema waliomualika ni kikundi cha watu fulani.Viongozi wengi makanisani ni miungu watu, hawakosolewei wala hawashauriki. Wanapeana uzee wa kanisa, ushemasi, uaskofu kulingana na fedha za mtu, kazi ya mtu na urafiki na mtu na siyo mtu huyo ana uwezo gani wa kuongoza watuki-Mungu.Si tunakurupuka leo na kutaka mtu fulani ajiuzulu wakati hatujalelewa katika tamaduni hizo, kuanzia ngazi ya familia na kanisa.

Muda umefika wa kubadilisha mifumo yetu,tujiulize je mafisadi wanapaswa wakamatwe na nani? Na je wakikamatwa mahakama zetu zina uwezo wa kuwahukumu? Na je wakienda gerezani hawatatoroswa kwenda nje ya nchi?.Mwakyembe aliposema Rostam na wengine wengi wanahusika , TAKUKURU,polisi na usalama wa taifa walitakiwa wachukue hatua haraka na tungeona matokeo.Tukishaona hivi tujue tunapaswa kuifumua mifumo yote kuanzia ngazi ya rais mpaka balozi wa nyumba kumi kumi.Mapinduzi hayaleti demokrasia , demokrasia inaleta mapinduzi.Tukishafanya mapinduzi kama mifumo bado mibaya bado hatujafanya kitu, Kenya mashahidi wa hili.Ni wakati mzuri wa kupigia kelele swala la katiba, tume za uchaguzi na misingi mingine mingi.. Hili linawezekana kwa sababu tunauwezo wa kupiga kura. Kama tuko tayari tupige kura si kwa kusema fulani nimchanga katika uongozi , maana hata Nyerere hakuwahi kuwa rais kabla ya kuwa rais, tunaangalia uwezo wa mtu,je alifanya nini siku za nyuma na atatufanyia nini.Hapa ndipo ninashawishika kusema hata vyama vyetu vingi vya upinzani bado ni visaliti . Natamani ruzuku isiwepo ili tupate viongozi waliojitoa na kuuza sera zao tutazinunua kwa michango yetu, huu utaratibu wa fedha kutoka serikalini ni kunyong’onyesha upinzani! ama sivyo watu wa aina ya Odinga na Tsavangirai tutawasikia tu.

Maaskofu wa makanisa kaeni chini nendeni kwa rais mkamuulize mafisadi wanachukuliwa hatua gani na mumpe muda, maana mafisadi hawa ni kaka na dada zetu, ni wajomba zetu, watoto wetu, waumini wenu wanacheza nao,hata nyie mnakula nao, Kama vithibitisho vyenu viko sahihi kwa nini hawafunguliwi mashtaka?.Mkishindwa kupata majibu inabidi mkubali hata kuandamana ili haki itendeke.Kumsimamisha Mchungaji siyo kutatua tatizo! Na si kikanisa tena hii ni siasa kanisani.Nachelea siku moja KKT kufanya maamuzi kuwaridhisha watu mtafika pabaya! Mtoto aliyekuwa anacheza nyumba ya jirani akarudi analia sio unampiga mtoto na kumwambia kwa nini ulienda kucheza kwa jirani,labda kama ulimkataza asiende ,sidhani kama KKT imewaambia waumini wake wawakwepe mafisadi na kwa namna hiimakanisania hawatabaki watu!

Tunaishi katika criminalised society(jamii ambayo wengi wao wanamakosa ya jinai)) ambapo ufisadi wanafanya watu wengi, pengine asilimia 40 ya watanzania sio waaminifu katika maeneo yao ya kazi,katika mali za serikali na jamii, wengine hawajajulikana , wengine wakati huu bado wanaiba mabilini ya shilingi!. Na hiyo asilimia wengi wao wasomi na wana uwezo.Wengi wa hawa hawana mpango na siasa wala kinachoendela nchini maana wanakula wanavaa na wana magari. Katika hawa wengi hawapigi kura. Kulalamika kuwa raisi hatufai kwa maneno mengine japo inauma kusema ni kujitukana wenyewe. Tunawezo wa kuchagua tumtakaye.Kama unalalamikia uongozi na hukupiga kura nao ni ufisadi mwingine afadhali anayelalamika alipiga kura, hata kama kwa macho masikio na utashi wake alimchagua asiyefaa! Dhana ya kikristo ya kuheshimu mamlaka inaanzia hapa, kuwa wanaotuongoza ndio tuliowachagua. La si hivyo basi lawama zote wanachi wanapaswa kuzibeba! KKKT wakiwemo hapa. Na hapa sio siri katika wapiga kelele za ufisadi wengi sio wakweli ili mradi siku ziende. Ukiwaambia haya sasa maandamano ya kupinga ufisadi wengi hawajitokezi, lakini ndio wa kwanza kongelea juu ya ufisadi.

Watanzania wengi sio wapole kama inavyojulikana, ila kinachoonekana ni kuwa hakuna matatizo sana ya kuwaua watu(there is no critical problem).Nauli zikipanda wataongea siku mbili lakini watalipa, vitu vikipanda watafanya hivyo hivyo, mali asili zinaondoka, kilimo hamna anayefuatilia. Ikitokea asilimia 70 ya wananchi wanashindwa kusafiri,kula na matibabu kwa sababu gharama ya maisha imepanda,ikifikia mpaka mfagizi kariakoo ni mchina.Wengi ndio wataamka na kushtuka lakini tutakuwa tumechelewa.Kipindi hicho mwenye nguvu ataishi, hata kama tutawapeleka mafisadi gerezani lakini tayari mali asili zetu zitakuwa zimeondoka.Upole wetu na kutojali mambo yetu kipindi hiki kutaangamiza vizazi vijavyo.Hapa uzalendo hauhitaji elimu.

Furaha yangu ni kuona wanaotuhumiwa na ufisadi wanachukuliwa hatua na kuthibitishwa kuwa ndio halafu wapate adhabu sawia na makosa yao.Furaha yangu ni kuona makanisa yanachukua hatua nzito juu ya mafisadi kwa kuangalia kiini cha tatizo.KKT inapaswa ijue kuwa watanzania wengi wako kama wale wayahudi waliosema ona Yesu anakula na Zakayo mwenye dhambi, itambue kama ambavyo wale wayahudi hawakuwa na uwezo wa kumfanya lolote Zakayo, ndivyo ilivyo watanzania wengi wanaishia kusema tu. Lakini KKT wakati wanamzogoa Rostam(kama Zakayo) walipaswa wachukue nafasi kama ya Yesu, watimize wajibu a kikanisa na sio walivyofanya.Niko tayari kukosolewa pale nilipoandika kinyume,Mungu ibariki Tanzania.

MdauUDSM

No comments: