Saturday, July 12, 2008

Wasabato wenye imani kali na safari ya ulaya

WAUMINI 17 wa dhehebu la Wadiventista Wasabato Masalia, kutoka mikoa mbalimbali nchini, akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka (16) na wanawake wawili wameweka kambi kando ya Uwanja vya Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa lengo la kusubiri usafiri kwenda nchi za nje kuhubiri Injili bila kuwa na nyaraka zozote za kusafiria.
Waandishi wa gazeti hili jana walifika eneo hilo la Uwanja wa Ndege majira ya saa 4:30 asubuhi na kuwaona waumini hao wakiwa wamepiga kambi wakiwa na mizigo yao.
Mwananchi lilipofika katika eneo hilo, waumini hao walianza kuwafokea kuwa wanakiuka haki zao za msingi kwa kuanza kuwapiga picha bila idhini yao.
Kutokana na mtafaruku huo, waandishi wa Mwananchi waliwaomba radhi na kuwaelewesha kwamba, lengo lao halikuwa baya, bali walitaka kuandika habari na kuchapisha picha zao ili jamii ielewe walichokuwa wakifanya katika eneo hilo.
Baada ya mazungumzo hayo, hatimaye waumini hao walikubali kuzungumza na Mwananchi, lakini wanawake waliokuwa miongoni mwa kundi hilo waliondoka. Walipoulizwa wale wanawake wameenda wapi, walijibu kuwa hawatakiwi kuelewa.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti waumini hao walisema, wapo katika viwanja hivyo kwa muda wa siku tano sasa wakisubiri usafiri kwenda nchi za nje kuhubiri neno la Mungu.
Kusekwa Daudi, ambaye ni mmoja wa waumini waliopiga kambi katika viwanja hivyo, alisema lengo lao ni kusafiri na kwenda nchi za nje ambazo wameelekezwa na Mungu waende wakaeneze Injili kama neno la Mungu linavyosema, enendeni ulimwenguni mkaihubiri Injili.
''Tupo hapa kwa maelekezo ya Mungu, tunasubiri usafiri kwenda kuhubiri Neno la Mungu, mimi naenda Iran, Mungu kanituma huko,'' alisema Daudi.
Daudi alifafanua kuwa, Mungu kawapanga watu wawili wawili kila sehemu na kwamba, tiketi zao na viza ni Biblia, hivyo hawana wasiwasi wa kuondoka eneo hilo.'' Tutaondoka hapa tulipo, hatuna chakula, lakini Mungu atatupa,'' alisema.
Naye Daniel Masinde (16) ambaye alimaliza elimu ya msingi mwaka jana katika shule ya Bunda na kudai kufaulu kujiunga na sekondari, alisema hakutaka kuendelea na masomo hayo kwani aliamua kumtumikia Mungu kwanza na mambo mengine yatafuata baadaye.
''Nilifaulu, lakini sioni umuhimu wa elimu, kwanza nimtumikie Mungu, mimi amenituma kwenda Ufaransa na muda wowote nitaondoka kuanzia sasa,'' alisema Masinde.
Aliendelea kudai kuwa, amewaacha wazazi wake mkoani Mara kwani Biblia inaeleza kuwa mtu asipoacha vyote na kumfuata Mungu amepotea.
Mtoto huyo ambaye alionekana akiongea kwa ujasiri na kujiamini zaidi, alisoma mistari katika Biblia na kutolea maelezo ikiwa ni pamoja na Bahari ya Hindi itakuwa damu siku ya uchungu.
Mtoto huyo alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na lugha atakayotumia wakati akieneza Injili huko Ufaransa wakati hajui Kifaransa, alisema Mungu atamjaza Roho Mtakatifu ili kuweza kuongea lugha yoyote ile.
''Suala la lugha halina shida kabisa, Mungu atanijaza Roho Mtakatifu nitaongea tu lugha yeyote,'' alisema Masinde.
Mwingine aliyejulikana kwa jina la Kibunda Masige alisema kuwa, Kristo atawakatia tiketi za ndege wataondoka muda wowote kuanzia sasa (wakati wa mahojiano jana).
Awali, waumini hao walieleza kuwa maamuzi ya kwenda kuhubiri Neno la Mungu katika nchi za nje yalitolewa katika Mkutano Mkuu wa dhehebu hilo uliofanyika Mwanza Aprili mwaka huu ambapo walifikia maamuzi hayo.
Walifafanua kuwa katika msafara wao hawana kiongozi wao wala mkuu wa msafara, kwani kiongozi wa msafara wao ni Mungu.
Waumini hao walipoulizwa kuhusu sehemu wanapolalala, walijibu kuwa Mungu ndiye anajua wanapolala hata wao hawaelewi.
Waumini hao wamedai kuwa wale ambao wanakwenda nchi za jirani ambazo hazihitaji ndege, wameshafika huko, lakini wao wanakwenda nchi za mbali ndio maana wanasubiri usafiri Dar es Salaam.
Waumini hao wa dhehebu la Waadiventista Wasabato, walianza kuingia Dar es Salaam mmoja baada ya mwingine kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ikiwemo Mwanza, Shinyanga na Kigoma Jumamosi wiki iliyopita.
Badaa ya kufika uwanjani hapo walikaa ndani ya Uwanja wa Ndege kwa siku mbili na baadaye uongozi uliwafukuza ndipo walipoamua kwenda pembeni ya baa ya Night Park jirani na uwanja huo na kuweka kambi eneo hilo.
Kwa upande wake, Afisa Usalama wa Uwanja wa Ndege, Julius Muungwana, alithibitisha kuwepo kwa kundi la waumini hao katika maeneo ya viwanja hivyo kwa muda wa siku mbili na kueleza kwamba waliwafukuza.
''Ni kweli kundi la watu hao lilifika katika viwanja hivi, sheria zetu haziruhusu mtu kukaa katika maeneo haya bila kazi yoyote, hivyo tuliwafukuza, lakini sasa hatuelewi nini kinaendelea juu yao,'' alisema Muungwana.
Hivi karibuni kundi jingine la waumini hao lilipiga kambi porini mkoani Mbeya likisubiri siku ya kurudi kwa Yesu. Waumini hao walidaiwa kuuza vitu vyao wakisubiri mwisho wa dunia kwa maelezo kwamba, Yesu asingeshuka mijini ambako kumejaa maovu ndiyo maana wakawa wanamsubiri porini.
Hata hivyo, baada ya muda waumini hao waliondoka porini bila Yesu kushuka.
Source: mwanachi

No comments: