Tuesday, July 8, 2008

Rostam Aziz ajisafisha kanisani

**Asema watu wanachukiana na kuombeana vifo Adai wanazushiana uchawi, anapakaziwa fisadi **Aomba kanisa litumike kurejesha taifa katika mstariDar es Salaam,

MBUNGE wa Igunga, Bw. Rostam Aziz amesema taifa liko katika wakati mgumu kisiasa na kijamii na ameomba watu watumie makanisa kulirejesha katika mstari ulio sahihi.
Bw. Rostam ametoa mwito huo leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi na kuweka wakfu albamu ya kwaya ya Amkeni ya Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kinondoni, iliyofanyika katika viwanja vya kanisa hilo ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz akionyesha kanda za video, kaseti na dvd za kwaya ya Amkeni ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kinondoni wakati wa hafla ya uwekaji wakfu katika kanisa hilo, Dar es Salaam leo. Kulia ni Mwenyekiti wa maandalizi ya hafla hiyo, Justine Mugangala
Amesema waumini wa dini hawamtuhumu mtu, hawamshutumu, hawapendi wenye wivu na wenye chuki bali wanapenda haki, na kwamba licha ya kashfa za ufisadi anazozushiwa, wamepuuza hilo na wamejenga imani kwake.
“Nawashukuru kwa kuamua kunialika kuwa mgeni rasmi… ni ishara kwamba mmeamua kupuuza maneno na upuuzi wa vijiweni. Nafurahi kuwa miongoni mwenu…. hamtuhumu, hamshutumu, hampendi wenye wivu na wenye chuki, mnapenda haki. Ninao watoto watatu na nataka niwalee katika misingi hii,” alisema Rostam huku akishangiliwa na umati wa watu waliofurika katika hafla hiyo.
Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz akizungumza na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kinondoni wakati wa hafla ya uwekaji wakfu katika video, kaseti na dvd ya kwaya ya Amkeni ya kanisa hilo, Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mchungaji wa kanisa hilo, Joseph Masege na kulia ni Mwenyekiti wa maandalizi ya hafla hiyo, Justine Mugangala
Rostam alisema watu wanachukiana mpaka kufikia hatua ya kuzushiana uchawi na kuombeana vifo. “Tutumie makanisa kukemea vitu hivi ili kurejesha taifa katika mstari ulio sahihi,” alisema.
Rostam alisema licha ya matatizo ya kisiasa, kuna matatizo ya kijamii ambayo alisema ni ndoa kuvunjika kila kukicha, watoto wa mitaani kuongezeka, madanguro na dawa za kulevya kukithiri, mambo ambayo yanasababishwa na mmomonyoko wa maadili.
Katika hafla hiyo ya kuweka wakfu kanda za video, kaseti na dvd, Mbunge huyo alitoa mchango wa sh. milioni 5 kuchangia seti za vyombo vya muziki kwa kwaya ya Amkeni pamoja na jenereta yenye thamani ya sh. milioni 2.6. Hiyo ni albamu ya kwanza ya kwaya ya Amkeni iliyodumu kwa miaka 24 sasa.
Mwaka 2005, Rostam pia alishiriki katika harambee ya ujenzi wa jengo la Kanisa la KKKT Kinondoni ambalo kwa sasa linatumika kama Chuo Kikuu cha Tumaini.
Waimbaji wa kwaya ya Amkeni ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kinondoni wakitumbuiza wakati wa hafla ya uwekaji wakfu katika kanda zao za video, kaseti na dvd, leo jijini Dar es Salaam . Mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz aliyeichangia kwaya hiyo sh. milioni 5 na kuahidi kuinunulia jenereta yenye thamani ya sh. milioni 2.6.

No comments: