Tuesday, July 15, 2008

Mtikila na milioni 3 za Rostam Aziz

Mchungaji wa Kanisa la Wokovu Kamili, Christopher Mtikila, amesema atamfungulia kesi mahakamani Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz. Alidai mashitaka hayo yatakuwa ni pamoja na ya kughushi saini katika stakabadhi ya malipo anayodai alilipwa kama mkopo na si sadaka au mchango wa Kanisa kama inavyodaiwa. Wakati Mtikila akiyasema hayo, suala la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kutangaza kutotambua mchango alioutoa Rostam alipoalikwa kwenye uzinduzi wa kwaya, limeleta changamoto mpya baada ya baadhi ya taasisi za dini kutaka zipewe namba ya mbunge huyo ili zimwalike azichangie fedha.
Mmoja wa Wainjilisti kutoka Huduma ya Biblia ni Jibu kutoka Morogoro, Damian Ndimbo aliomba apewe namba ya simu ya Rostam kwa lengo la kumpigia na kumwomba aipatie msaada wa kifedha taasisi yake. “….Mbunge Rostam Aziz kuchangia kanisa yupo sahihi, kwani kanisa limesababisha hayo yote na kama mna namba yake mnitumie aje asaidie na huduma yetu,” alisema Ndimbo kwa njia ya simu. Aliongeza, “Wakristo wenye fedha wako wengi lakini hawachangii kanisani wala kusaidia, kazi yao ni kuchangia mambo ya ajabu kama pombe, lakini huyu Rostam amejitolea, tunaomba namba yake atusaidie na sisi huku Morogoro.” Mtikila, akizungumza na na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, aliibua masuala ya uraia na kusema kuwa miongoni mwa kesi atakazofungua ni pamoja na kuhoji uraia wa mbunge huyo. Mtikila, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), alisisitiza jana kuwa Sh milioni tatu alizopokea kutoka kwa Rostam zilikuwa za mkopo na kwamba atamrudishia. “Mimi nitazirudisha hizo fedha na akizikataa ina maana nizitafune, na mimi nina meno 32 kama binadamu wengine nitazitafuna,” alisema. Akirejea kwenye Biblia, Mtikila alisema huo ulikuwa mkopo kama ambavyo Mungu alivyomtumia Farao kugharamia maandalizi ya Musa na kwamba na yeye aliutumia katika maandalizi ya kuwashtaki waliofilisi nchi na kuwafanyia utafiti. Alisema alipochukua mkopo yeye ndiye aliyesisitiza asainishwe akiwa na uhakika wa kuurudisha, kwa kuwa mkopo ni kama biashara hivyo hauna dhambi na unachukuliwa kwa mtu yeyote ili mradi masharti yasiwe mabaya. Mtikila alisema kila stakabadhi halali ya malipo inatakiwa iwe na jina kamili la mlipwaji, maelezo sahihi ya sababu za malipo, tarehe ya malipo, saini ya mlipaji na mlipwaji na namba na mhasibu hawezi kugonga mhuri kama stakabadhi hiyo haina namba kwa kuwa itakuwa ni malipo hewa. “Na huyu aliyesaini stakabadhi hii aanze kutroti kwenda Keko”. Alidai Rostam ametumia stakabadhi hiyo kwa ajili ya kujisafisha kwa kuitumia KKKT na kwamba yote aliyofanya ni halali. Alisema hata makanisa ambayo mbunge huyo anadai kuwa alishayachangia tangu awali, yalipokea fedha hizo za sadaka kabla ya Rostam hajatuhumiwa kuhusika na masuala ya Richmond na EPA. Pia alimtaka mbunge huyo naye kwenda mahakamani kama anaona anaonewa au kuchafuliwa kufuatia kauli zinazotolewa dhidi yake kuhusu mwaliko wake na kauli zake alizozitoa hivi karibuni katika KKKT, Usharika wa Kinondoni
Source: Habari leo;Globalpublishers

No comments: