Monday, July 14, 2008

WANAMAOMBI KUTAKA KULIOMBEA BUNGE KUFUKUZA NGUVU ZA GIZA (UCHAWI)

Kamati ya Umoja wa Makanisa ya Kikristo nchini, imemuandikia barua Spika wa Bunge, Bw. Samwel Sitta, ikimuomba awaruhusu waende Dodoma kulizunguka Bunge kwa ajili ya maombi na kusisitiza kwamba hawaamini taarifa iliyotolewa na Polisi kwamba unga uliopatikana ndani ya jengo hilo haukuwa na uchawi.

Kadhalika, Kamati hiyo imewashauri mawaziri na wabunge wenye hirizi kuzisalimisha kwao kabla ya kuanza maombi kwani wanaweza kuumbuka.

Pia Kamati hiyo imesema hatua ya Naibu Spika kufunga mjadala kuhusu `unga wa uchawi` haiwakatishi tamaa kufanya maombi hayo. Kamati hiyo imesema taarifa ya polisi imewachanganya na sio sahihi kwa sababu dola haiamini mambo ya uchawi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamti hiyo, Askofu Isack Kalenge alisema uchunguzi huo wa Polisi, Mkemia Mkuu, Bunge na Usalama wa Taifa ni batili kwa kuwa vyombo hivyo ambavyo viko chini ya serikali, havina uwezo wa kutambua uchawi.

Askofu Kalenge, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Pentekoste International, alisema wanaamini kuwa bado uchawi upo bungeni na wabunge wengi wanateswa na nguvu hizo za giza.

``Uchawi ni jambo la kiroho, haliwezi kupimwa kwa kamera wala uchunguzi wa Mkemia Mkuu, tunaamini tatizo la uchawi bungeni halijapatiwa ufumbuzi, tunakwenda Dodoma kulimaliza tatizo hilo ili lisitokee tena,``alisema. Akizungumza katika mkutano huo, Mchungaji Wilbert Ngowi alisema kamati hiyo haiwezi kufumbia macho taarifa hizo, kwa vile zimeliaibisha Taifa.

``Umefika wakati sasa kanisa liseme yale ambayo lilikuwa linayafumbia macho na lifanye mambo ambayo yalikuwa hayafanyiki, japokuwa hatua hii inaweza kutafsiriwa kwamba tunachanganya dini na siasa, lakini si vibaya.

Kuanzia sasa tumeamua kuchanganya dini na siasa kwa sababu maandiko matakatifu yanasema kufanya hivyo sio dhambi,``alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mchungaji Christopher Mtikila alisema iwapo watapata ushirikiano wa Spika wataenda bungeni wiki ijayo. Akifafanua, kiongozi huyo alisema wamemuomba Spika awape kibali cha kuingia bungeni kuwaombea wabunge na `kuharibu` nguvu za giza zilizojaa humo. Mchungaji Mtikila alisema kabla hawajatia mguu Dodoma, wanawataka Wabunge, mawaziri na yoyote ambaye anatembea na hirizi aisalimishe kabla hawajaanza maombi.

``Ni matarajio ya Kamati kwamba wabunge wazalendo, hususan wale ambao hawatembei na hirizi vibindoni, watafurahia kazi hii njema ya watumishi wa Mungu yenye lengo la kuwaponya,``alisema. Kiongozi huyo alisema iwapo watakataliwa kufanya mambo hayo, watalizunguka jengo la Bunge hilo na kurusha `makombora ya sala` na kuahidi kwamba hakuna mwanga wala hirizi itakayosalimika.

Aliahidi kuwa wabunge na mawaziri, ambao ni wapenda uchawi, wataumbuka vibaya kutokana na sala hizo. Alisema tayari waumini mbalimbali wameshaanza kufunga kwa ajili ya kujiandaa na sala hiyo. Alisema hawatarajii upinzani kutoka kwa Bw. Sitta kwa sababu hivi karibuni Spika huyo alinukuliwa akiwataka viongozi wa dini, kuliombea Bunge kutokana na kuwa katika wakati mgumu.

``Sisi tumeamua kwenda kuliombea Bunge kama alivyosema, ila sisi tutaenda na mamlaka makubwa, ambayo yatasambaratisha kila roho chafu. Sisi wenye macho ya kiroho tumejua kwamba pale ndani pametundikwa kila aina ya uchawi, lakini hakuna hata mmoja ambao utasalimika,``alisema.

Sorce: Nipashe, 14.07.2008

2 comments:

Unknown said...

kwakweli ni jambo la muhimu kuliombea bunge hasa kwenda mule bungeni hata iwe nje iwapo watakataliwa wasambalatishe nguvu za giza!! aliyefikiria ili namshukuru ni mungu anataka kujidhihirisha kwa utukufu wake. Niko mbali sijui kama limefanyiwa kazi hapa naona habari hii ni ya tarehe 14 Julai!! je limefanyiwa kazi!! Kama bado nawaombeni watumishi wa mungu mfanye Hima kutokomeza uchawi Bungeni!! Wanataka serikali ibaki mikononi mwa wachawi!!! Pinga vita uchawi

Unknown said...

kwakweli ni jambo la muhimu kuliombea bunge hasa kwenda mule bungeni hata iwe nje iwapo watakataliwa wasambalatishe nguvu za giza!! aliyefikiria ili namshukuru ni mungu anataka kujidhihirisha kwa utukufu wake. Niko mbali sijui kama limefanyiwa kazi hapa naona habari hii ni ya tarehe 14 Julai!! je limefanyiwa kazi!! Kama bado nawaombeni watumishi wa mungu mfanye Hima kutokomeza uchawi Bungeni!! Wanataka serikali ibaki mikononi mwa wachawi!!! Pinga vita uchawi