BWANA YESU ASIFIWE!
(hili ni somo nililolituma kwa wale waliojiunga na Mailing lists)
KUZIJENGA KUTA ZILIZOBOMOKA NA KUSIMAMA MAHALI PALIPOBOMOKA TANZANIA-2
• Ni muhimu na lazima kuanza kuombea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Tanzania.
Katika somo nililotuma mara ya mwisho, Roho Mtakatifu alikuwa anatuhizima sote tudumu katika kuomba toba kwa ajili ya taifa letu la Tanzania, Bwana Yesu asifiwe kwa ajili ya watu wote ambao tayari wamechukua hatua kuanza kufanya hivyo, wale walionitaarifu pia na wale ambao hawajanitaarifu, awape nguvu zaidi. Katika somo hili la leo, nataka niweke ndani yako wito (“mzigo”) wa kuanza kuombea uchaguzi mkuu wa viongozi wa Serikali wa Tanzania, utakaofanyika mwishoni mwa mwaka 2010. Katika mazoea yetu, huo mwaka 2010 waonekana kuwa mbali sana kutoka sasa, lakini nafikiri hii ni picha ya kimwili tuu, kwa sisi tumwaminio Bwana, kipindi hicho kii karibu nasi kuliko ionekanavyo katika mwili. Ninaamini unafahamu kuwa, shetani akitaka kuweka watu wake kwenye uchaguzi huo, basi yeye hataanza jitahada zake ikifika hiyo 2010, yeye huanza mapema sana, labda kwa sababu Biblia inasema “Kwa kuwa anajua anao wakati mchache”. Na sisi watu tuliookoka tunatakiwa kuanza kufanya hivyo mapema, mapema kumzidi hata “adui” yetu. Hii ndio sifa ya walinzi bora, wale tuliojifunza katika sehemu ya kwanza ya somo hili. Baba Mungu anapenda aanze kufanya kazi yake mapema, lakini kumbuka siku zote kuwa Baba Mungu mara nyingi anatusubiri tufanye kitu (tuombe) ndio na yeye atusaidie. Tukikaa kimya bila kuomba, tunaweza kupata viongozi wasio-mpango wa Baba Mungu na hasara zake zikatupata wote. Neno la Baba Mungu linatuagiza katika kitabu cha 2 Timotheo 2:1-3: “1Basi, kwanza kabisa, naagiza kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zitolewe kwa ajili ya watu wote: 2kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani, tukimcha Baba Mungu na kuwa wenye heshima kwa kila njia. 3Jambo hili ni jema na linampendeza Baba Mungu Mwokozi wetu “ Neno hili ni wakati wake sasa kwa sisi wote kuliweka katika matendo kwa ajili ya nchi yetu ya Tanzania. Kwa wale ambao hupata nafasi ya kufuatilia vikao vya bunge la Tanzania, wanaweza kuelewa ni kitu gain kitatokea kama Baba Mungu asipoweka watu wake kule ndani ya bunge. Vivyo hivyo kwa sehemu nyingine za madaraka katika nchi yetu. Kama wote tujuavyo, Baba Mungu akitaka kufanya kitu mahali, huwatumia watu wake aliowaweka hapo mahali, na shetani vilevile, akitaka kufanya maovu yake mahali, huwatumia watu wake walio mahali hapo. Kwa hiyo ni muhimu na msingi sana tumwombe Bwana Baba Mungu ili awaweke watu wake katika sehemu mbalimbali za uongozi katika nchi hii. Tumwombe atupe rais anayemjua, makamu wake, waziri mkuu, mawaziri wote na manaibu wao, wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji, lakini pia wakuu wa mikoa, wilaya na maeneo mengine yote. Ni imani yangu kuwa kama Kanisa tukijipanga vizuri na kuanza kuomba, basi Baba Mungu atakaa upande wetu na atatupa viongozi watakatuongoza kwa kufuata Neno la Baba Mungu. Tatizo au kosa ambalo tumekuwa tukilifanya ni kwamba huwa tunasubiri hadi ule mwaka wa uchaguzi ndiyo tunaanza kuombea uchaguzi huo. Sisemi kuwa Baba Mungu hatajibu kabisa, lakini ni vizuri zaidi kuanza kuomba mapema iwezekanavyo. Maana naamini michakato hii ya uchaguzi imeshaanza ‘kimyakimya’ ndani ya wanasiasa na vyama vyao hata sasa. Ninaamini kuwa kila chama kimeshaanza kuweka umakini mkubwa kwenye uchaguzi wa 2010, kulizidi kanisa. Inatupasa mimi na wewe, na vikundi vyetu vya maombi pamoja na waombaji wengine, tuanze kumwomba Baba Mungu ili kuanzia katika ngazi ya chama, aanze kuwainua na kuwaweka watu kwa ajili ya kugombea nafasi katika uchaguzi wa 2010. Tena tumwombe Baba Baba Mungu ili awaondoe/kuwazuia watu wote ambao shetani kwa hila zake atajaribu kuwaingiza katika harakati zote za uongozi wa nchi hii. Ni muhimu sana kuombea jambo hili kwani viongozi wa serikali wana athari kubwa (nzuri au mbaya) katika taifa wanaloongoza. Ikumbukwe pia kuwa, maamuzi ambayo viongozi wanayafanya yanatuhusu sisi kanisa la Mungu pia, yanagusa hata namna kazi ya Mungu Baba inavyofanyika katika nchi hii. Tukipewa viongozi wamjuao Bwana Mungu, basi itakuwa ni rahisi zaidi kwa taifa la Tanzania kupokea Baraka nyingi sana ambazo Mungu ametuahidi (sisi kama Tanzania) Ni wakati muafaka sasa, sote tuamke na kushika zamu zetu kuanza kuomba kwa ajili ya uchaguzi wa 2010, tumwombe Mungu Baba atupe viongozi; wanaomjua yeye sana (Ayubu 22:21), wenye hofu ya Mungu na wacha Mungu, watakoongoza hii nchi kwa kufuata Neno la Mungu, watakapenda kutenda haki n,k kama Roho atakavyokuongoza. Unapokuwa kwenye maombi likumbuke hili, unapokuwa kwenye vikundi vya maombi kanisani au popote usisite kuwashirikisha wengine jukumu hili. Ninaamini kuwa Roho Mtakatifu ataendelea kusema na wewe juu ya jambo hili na Yeye pia atakusaidia kufanya sehemu yako katika kuhakikisha kuwa mapenzi ya Mungu yanatimia katika uchaguzi wa 2010 na katika mambo mengine yote katika nchi hii.
(**Kupokea masomo mengine kupitia email yako, jiunge na mailing lists kwa kutembelea www.lema.or.tz)
Tuendelee kuombeana daima.
Katika Utumishi wa Kristo,
Frank Lema. Arusha.
No comments:
Post a Comment