Wachungaji zaidi ya 300 na wazee wa Kanisa la Pentecoste Tanzania (KLPT), wanakutana jijini Dar es Salaam kuzungumzia masuala mbalimbali yanayoitikisa nchi kwa sasa, yakiwemo mauaji ya maalbino na ufisadi. Mambo mengine yatakayojadiliwa katika mkutano huo ulioanza jana na ambao umepangwa kumalizika Jumapili ijayo, ni ugonjwa wa ukimwi, afya ya uzazi na kufanya tathmini ya shughuli za kanisa hilo kwa mwaka uliopita na kupanga mikakati mipya kwa ajili ya mwaka ujao. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa KLPT, Fanuel Shekihiyo, alisema kuwa mkutano huo ambao unawakutanisha pamoja wachungaji na wazee wa kanisa hilo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, utaongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Philemon Tibanenson. Alisema ajenda za mauji ya maalbino, ufisadi, afya ya uzazi na ugonjwa wa ukimwi zitajadiliwa kwa kina wakati wa mkutano huo kwa sababu mambo hayo kwa sasa yanaitingisha nchi na kuwafanya wananchi waishi kwa hofu. Alisema wao wakiwa kama viongozi wa kiroho wameona wana wajibu wa kuyajadili masuala hayo yanayoenda kinyume cha mafundisho ya Mungu, ili kuwaongoza wanadamu katika mambo mema, baada ya mkutano huo kanisa hilo litatoa tamko juu ya masuala hayo. Kilio cha mauaji dhidi ya watu wa jamii ya albino kilichoelezwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam wakati wa maandamano ya kupinga vitendo hivyo, vimeendelea kutikisa taifa baada ya watu wasiojulikana juzi kumkata miguu akiwa hai mwanafunzi albino na kisha kutokomea nayo. Mwanafunzi huyo wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Shilela, kata ya Segese, Kahama mkoani Shinyanga, Esther Charles (9), alifariki dunia baada kukatwa miguu na kunyofolewa nywele za utosini na kisogoni na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia juzi na kutoweka na viungo hivyo. Tukio hilo la kusikitisha linafanya idadi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) waliouawa nchini kutokana na imani za kishirikina kufikia 29 na kuibua upya hofu miongoni mwa jamii.
SOURCE: Nipashe
No comments:
Post a Comment