Bwana Yesu asifiwe!
Ndugu wapenzi wote wa Mlima Sayuni, tunawaletea mafundisho mazuri ya Neno la Mungu yaliyofundishwa na mtumishi wa Mungu, Mwalimu Christopher Mwakasege. Somo hili lenye sehemu 11 linaitwa "MAMBO YA KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYAUAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA" Tunaamini kuwa hili somo litakuwa ni baraka kubwa kwa wote, na hasa kwa wale ambao hawajoa au kuolewa na wana mpango huo. Mungu akubariki, wataarifu na wengine pia.
Utangulizi
Ukifungua kitabu cha Yoeli.3:14 kinasema, “Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya Bwana i karibu”. Huyu ndugu, mtumishi wa Mungu, aliyekuwa anaitwa Yoeli, Mungu alimpa nafasi ya kuona mambo ambayo yamekuwa yanafanyika tangu kuumbwa kwa ulimwengu, mpaka hapo Yesu atakaporudi tena. Anasema, ameona makutano makubwa, makutano makubwa, katika bonde la kukata maneno.
Tafsiri nyingine ya bonde la kukata maneno maana yake ni bonde la kufanyia maamuzi. Kukata maneno ni kufanya maamuzi. Sasa, bonde la kukata maneno, kwa tafsiri ya haraka ni dunia hii, wakati huu, mwanadamu anapoishi duniani.
Kwa sababu kabla hujazaliwa huna uwezo wa kuamua. Biblia inasema Mungu alimwambia Yeremia, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, kabla hujatoka tumboni nalikutakasa” (Yeremia 1:5). Kabla hajawekwa tumboni mwa mama yake, Mungu alimjua Yeremia, ambayo inamaanisha Yeremia alikuweko, lakini alifananaje sijui! Lakini maandiko yananiambia ya kwamba alikuwepo na Mungu alimjua. Alipokuwa tumboni Mungu alimtakasa, maana yake alimtenga kwa ajili ya utumishi na wito wake.
Lakini Yeremia hakuwa na uwezo wa kuamua. Kabla ya kuzaliwa huwezi kuamua, baada ya kufa huwezi kuamua kitu chochote. Ndio maana tunatamani kila mtu lazima aokoke, aamue anataka kuishi maisha ya namna gani baada ya kufa, maamuzi hayo unayafanya kabla hujafa. Baada ya kufa hakuna mahali pa kufanyia maamuzi hayo tena!
Kwa hiyo kipindi hiki, ambacho mwanadamu anaishi ndicho kipindi cha kukata maneno. Bonde la kukata maneno ni dunia hii. Makutano makubwa; maana yake aliona watu wengi sana wamekaa katika bonde ambalo wanatakiwa kufanya maamuzi.
Katika dunia hii, (Kama ulikuwa hujafahamu afadhali ufahamu), ya kwamba kati ya jambo muhimu sana ambalo utawajibika nalo mwenyewe ni kufanya maamuzi. Na yako maamuzi ambayo unahitaji kuwa mwangalifu sana unapotaka kuyachukua, kwa sababu yatasababisha mabadiliko ya maisha yako kabisa.
Kwa mfano maamuzi ya kuokoka, kwa mfano maamuzi ya kumtumikia Mungu, yanabadilisha kabisa maisha yako, ndio maana Yesu anasema, mtu kabla hajamfuata, akae chini, ahesabu gharama; kuna gharama katika kumfuata Yesu, na kuna gharama katika kumtumikia Yesu. Maisha yako yanabadilika kabisa! Huwa saa nyingine mimi na mke wangu tunatamani kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine, lakini haiwezekani, (watumishi wa Mungu wataelewa kitu ninacho elezea hapa), ukiishafanya maamuzi ya kusema unataka kumtumikia Mungu, maisha yako hayawezi kuwa ya kawaida tena, sio maamuzi madogo hayo.
Kuna maamuzi ya masomo, watu wanafanya mchezo wanapotaka kufanya maamuzi ya masomo, usifanye mchezo, ni maamuzi muhimu. Kuna maamuzi ya marafiki, unataka kuwa na marafiki wakina nani. Maamuzi haya yanaweza yakakubadilishia kabisa maisha yako. Lakini pia kuna maamuzi ya unachotaka kufanya maishani mwako ni nini. Mwingine atajitetea na atasema, Mungu anajua, - sawa Mungu anajua, lakini anahitaji maamuzi yako!
Wengine wanasubiri wakiishamaliza sekondari, au wakiishamaliza chuo kikuu, ndipo waamue wanataka kufanya nini. Ukiishafika chuo kikuu ndipo unataka kuamua cha kufanya maishani, utakuwa umechelewa. Kwa sababu, kama unataka kuamua kufanya kitu ambacho hukusomea, mambo yanawezayakawa magumu kwako, labda iwe ni Mungu anakupitisha hapo kwenye eneo hilo jipya.
Lakini pia kuna masuala ya kuamua kuoa au kuolewa, katika somo hili tutaangalia somo linalosema, “Mambo ya kutafakari kabla ya kufanya uamuzi ya kuoa au kuolewa”. Wengine mnaosoma somo hili ni vijana ambao umri wa kufikia kuolewa bado, lakini huu ni muda muafaka wa kukufikirisha jambo hili. Wengine wanaosoma somo hili wana karibia - karibia kuoa au kuolewa; au wameshaingia kwenye ndoa tayari. Halafu wanajikuta ya kwamba, afadhali wangekuwa wamejiuliza na kutafakari yaliyomo humu mapema zaidi.
Kwa muda ambao Mungu ametupa wa kuwahudumia watu mbalimbali katika miaka ya utumishi ambayo Mungu ametupa, kati ya jambo ambalo limesababisha maisha ya watu wengi yakawa mabaya au yakawa mazuri, yakawa magumu au yakawa marahisi, ni suala la kuoa au kuolewa.
Saa nyingine huwa ninawaambia vijana, Kama kijana anataka kuoa au kuolewa na ana haraka sana ya kutaka kuoa au kuolewa, basi asije kwangu kwa ushauri! Kama unataka kuoa au kuolewa, na una haraka sana ya kufanya hivyo tafadhali usije. Kwa sababu mambo niliyoyaona kwenye ndoa mbalimbali yananifanya hata mtu akija kwa ushauri wa kutaka kuoa au kuolewa, nimpitishe kwenye maswali magumu sana yatakayomfanya atafakari sana na kuomba kabla ya kuamua kuoa au kuolewa.
Nia niliyonayo ni ili nijue kama kweli amefikia mahali ambapo anajua kitu anachotaka kufanya. Maana wengi wanafikiri ni jambo rahisi. Mungu wangu aweze kukusaidia kuona ili usilichukuie jambo hili kwamba ni jambo jepesi, maana linabadilisha kabisa maisha yako.
Hii ni sehemu ya utangulizi wa somo hili lililofundishwa na Mwalimu wa Neno la Mungu, ndugu Christopher Mwakasege. Tutaendelea kuwaletea sehemu zinazofuata.
Tunawapenda,
-Sayuni.
No comments:
Post a Comment