Tanzania inatarajia kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) wakati wowote katika siku zijazo baada ya serikali kuweka bayana azma hiyo jana. Azma hiyo ya serikali iliwekwa bayana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi, alipozungumza na Nipashe jana, ikiwa ni wiki chache tangu Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe, aliambie Bunge kwamba, hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na jumuiya hiyo. Balozi Iddi alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC, unatarajiwa kuanza wakati wowote na kwamba, hatua ya mwanzo ya mchakato huo, viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano watakutana na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa ajili ya kupata msimamo wa pamoja kuhusu suala hilo. Naibu Waziri huyo alisema hayo alipoulizwa na Nipashe kama mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC umeshaanza au la tangu Waziri Membe atoe kauli hiyo bungeni, mjini Dodoma, Agosti 22, mwaka huu. ``Bado hatujaanza mchakato. Kuna kikao tunachotaka kwanza kufanya kwa ajili ya kushauriana na wenzetu wa Zanzibar ili tuwe na msimamo mmoja kuhusu hilo. Ilikuwa tuanze sasa, lakini Mheshimiwa Waziri (Membe) hayupo na Bunge linatarajiwa kuanza,`` alisema Balozi Iddi. Alisema mchakato kwa Tanzania kujiunga na OIC ni mrefu, ambao unatarajiwa pia kulishirikisha Baraza la Mawaziri kufikia maamuzi. Balozi Iddi alisema hatua nyingine ya mchakato, ambayo serikali inatarajia kuichukua, ni kutoa elimu kwa umma ili kuwaondoa uoga wote walioonyesha hofu iwapo Tanzania itajiunga na jumuiya hiyo. ``Hao wanaopinga, ni waoga tu, hawajaeleweshwa kwani haina maana Tanzania itakuwa nchi ya Kiislamu. Zipo nchi kama vile Uganda zimejiunga na OIC, lakini hazijabadilika kuwa nchi za Kiislamu. Tutawaelewesha wakati ukifika, tunavyo vyombo vya kuelimisha hilo,`` alisema Balozi Iddi. Agosti 22, mwaka huu Waziri Membe wakati akifunga mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema hakuna madhara yoyote kwa Tanzania kujiunga na IOC. Waziri Membe alisema serikali mwaka huu, ilifanya kikao na Baraza la Wawakilishi kuhusu suala hilo na kugundua kuwa nchi 21 zimejiunga na jumuiya hiyo. Alisema kati ya nchi hizo, zimo pia nchi za Wakristo ambazo zimejiunga na hazijapata madhara yoyote. ``Tumeshakusanya takwimu za nje na kuona hakuna madhara yoyote ya kujiunga na IOC, bora tu kufuata taratibu,`` alisisitiza Waziri Membe. Alisema suala hilo lilileta utata awali kwa sababu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, marehemu Ahmed Hassan Diria, alipeleka ombi la Zanzibar kujiunga kwenye jumuiya hiyo bila kuishirikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, alisema suala hilo limefanyiwa kazi na serikali na kuona kuwa hakuna madhara kujiunga na IOC. Siku chache baada ya Waziri Membe kutoa kauli hiyo bungeni, viongozi wa makanisa na baadhi ya wasomi, akiwamo Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Dk. Methodius Kilaini, walipinga vikali kauli hiyo ya serikali. Wengine waliopinga suala hilo, ni Askofu Stefano Msangi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT Tanzania, Dk. Alex Malasusa, Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi. Hata hivyo, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mnyamani, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mohammed Iddi, amekuwa akijitokeza kuwapinga maaskofu kuhusu kauli zao za kupinga suala hilo.
SOURCE: Nipashe
No comments:
Post a Comment