Mtikila aahidi kuendelea kuishambulia Chadema
MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amesema ataendelea kusambaza nyaraka zinazohusu kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo la Tarime, Chacha Wangwe na hatima ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuwa haogopi kukamatwa na polisi.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo machachari imekuja baada ya kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Liberatus Barlow kusema mapema wiki hii kuwa jeshi lake litamkamata mchungaji huyo wa kanisa la Wokovu Kamili na kumchukulia hatua za kisheria kwa kuendelea kusambaza waraka unaoihusisha Chadma na kifo cha Wangwe, akieleza kuwa waraka huo ni wa uchochezi.
Lakini pia Mch. Mtikila ameeleza hayo siku moja baada kunusurika kupigwa jiwe wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni, tukio hilo likitokea siku chache baada ya kiongozi huyo kutunguliwa na jiwe kwenye mkutano mwingine baada ya kuituhumu Chadema kumuua mbunge huyo wa Tarime.
Shambulio la kwanza lilisababisha Mtikila akimbizwe hospitalini na kushonwa nyuzi saba baada ya jiwe alilorushiwa kumchana kisogoni.
Lakini jana, 'mtumishi huyo wa Mungu' alionekana kutoyumbishwa na kauli hiyo ya DCI wala matukio yanayotokea kwenye wilaya ambayo mapigano baina ya koo hulipuka mara kwa mara.
"Nitaendelea kusambaza nyaraka hizi hadi nifikie lengo langu la kusambaza nakala milioni moja kwa watu wasiopungua milioni 10," Mtikila aliwaambia waandishi wa habari jana.
Mtikila, ambaye aliwahi kutumikia kifungo cha mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kusema kuwa viongozi wa CCM walimuua katibu wa zamani wa CCM, Horace Kolimba, alisema haogopi kukamatwa na polisi kwa kuwa tayari ameshakamatwa mara kadhaa na kushitakiwa.
Kiongozi huyo wa DP alimtaka Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba kutopoteza muda wake kwa kuunda tume kwenda Tarime kumchunguza yeye (Mtikila) kama anaendelea na kusambaza waraka huo kwa kuwa ni wazi kwamba hatakoma.
"Hakuna atakayenizuia kusambaza waraka huu, na sasa ninasambaza waraka mwingine, huu unaoeleza 'Taarifa ya DP na Mwisho wa Chadema' ambao nitasambaza nyumba kwa nyumba kwa kutoa nakala za kutosha, nitasambaza mikoa yote pamoja na hapa Tarime," alieleza Mtikila, ambaye pia ni kiongozi wa taasisi ya Liberty Desk, ambayo shughuli zake hivi sasa zimefifia.
Akizungumzia uzoefu wake wa mapambano na vyombo vya dola, Mtikila alisema ameshawahi kukamatwa mara 29 tofauti na kuwekwa ndani ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi za aina mbalimbali, kitu kinachomfanya asiogope kukamatwa tena kwa kuwa polisi hawana jipya.
Mtikila alisema ameamua kutoa kauli hiyo baada ya kuamini kuwa polisi wana mpango wa kumziba mdomo katika kampeni zake na yeye hatakubali na badala yake ataendelea kusambaza waraka huo.
"Imefika mahali tunafungwa mdomo tusizungumze mambo ya nchi yetu," alisema. "Wamekufa akina Sokoine kwa ajali nilizungumza, amekufa Horrace Kolimba pia nilizungumza na kupiga kelele kwa vile tuliamini wameuawa. Naomba DCI atambue kuwa mimi ni mtu mwenye msimamo nitaendelea kueleza."
Alifafanua kuwa namna pekee ya itakayomzuia asiendelee kusambaza waraka huo ni wahusika kutoa waraka mbadala utakaoeleza sababu za kifo cha Wangwe vinginevyo, ataendelea kuusambaza waraka huo hadi jamii ijue ukweli.
"Sasa ninasaka fedha zaidi ili niweze kuongeza nakala ambazo pia nitasambaza tena," alisisitiza.
Kamanda huyo alisema tayari ofisi ya DCI imeunda tume ambayo itaenda wilayani Tarime kwa ajili ya kumchunguza Mtikila kwa kitendo chake cha kusambaza waraka huo unaoeleza kuwa ana ushahidi unaojitosheleza kwamba CHADEMA ilimuua Wangwe.
Katika kampeni zake Mchungaji Mtikila amemtaka Spika wa Bunge, Samwel Sitta kutopuuza ombi la mke mdogo wa marehemu Wangwe, Mariam Wangwe, ambaye aliomba Bunge kuunda tume kuchunguza kifo cha mume wake.
Alisema kama Bunge liliunda tume kuchunguza mambo mengine, halina budi pia kuunda tume ya kuchunguza kifo cha Wangwe kwa vile ni mwakilishi wa wananchi.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment