Thursday, April 17, 2008

Mwinjilisti ablino akimbilia polisi kujiokoa asiuawe

POLISI mkoani Shinyanga linashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutaka kumuua Mwinjilisti wa Kanisa la AIC, wilayani Bukombe ambaye ni albino, Wilson Maduhu (55).
Watuhumiwa ni Paul Suka (72) na Joyce Edward (27), wote wakazi wa Kijiji cha Lulembela na wanaendelea kuhojiwa kujihusiana na tukio hilo.
Tukio hilo linadaiwa kutokea kati ya Aprili 6 na 8, mwaka huu saa 4:00 usiku Kijiji cha Ibambula, wilayani Bukombe.
Inadaiwa kuwa, Aprili 6 watu wasiofahamika walifika nyumbani kwa mwinjilisti huyo, kuanza kugonga mlango na kusababisha bawaba moja kuvunjika na kwamba, familia iliposhtuka watuhumiwa walikimbia.
Pia, inadaiwa usiku wa Aprili 8, watu hao walifika tena nyumbani kwa Marco Luchapa, wakidhani Maduhu alikuwa amelala huko ambako inadaiwa kuwa, walibomoa dirisha la chumba kimoja cha mbele wakimtafuta kwa lengo la kumuua, lakini alikwenda kulala kwa Petro Nhilimbe.
Kufuatia hali hiyo, Maduhu baada ya kuona maisha yake yako hatarini, aliamua kutoa taarifa za tukio hilo Kituo cha Polisi Ushirombo na walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa kutokana na ushirikiano wa wasamaria wema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Shaibu Ibrahim licha ya kuthibiisha kutokea kwa tukio hilo, alisema upelelezi ukibainisha watuhumiwa kuhusika watafikishwa mahakamani.
Ibrahim alitoa wito kwa wananchi kuepukana na mila potovu za ushirikina dhidi ya jamii ya albino na kuwataka kutoa taarifa polisi pale watakapoona mienendo yeyote wanayotilia mashaka
Source: Mwananchi

No comments: