Wednesday, April 30, 2008

Unamfahamu "Njia Nyembamba"?

Nikiwa katika kuwatembelea wanasayuni waliohitaji huduma ya maombezi na ushauri wa kiroho kutoka katika mlima huu wa Mungu maeneo ya posta mpya,nikasikia sauti kama ya mtu aliyae nyikani.Mahubiri yake yalikuwa yamejaa nguvu ya Mungu na neema ya YESU KRISTO ya ajabu akiwasihi watu wote wenye kusumbuka na mateso waje kwa YESU ili awape pumziko. (Mathayo 11:28).Ndipo nilipoamua kusimamisha gari na kujisogeza karibu yake, alipomaliza kuhubiri nikamwendea kwa karibu na kumsalimia kasha nikajitambulisha kwake na kutaka kujua mawili matatu kutoka kwake.

Wengi tummzoea kwa jina la “Njia Nyembamba”.Amekuwa akihubiri maeneo ya posta mpya, mnazi mmoja na kwenye mikusanyiko ya watu kwa miaka mingi sasa.Nakumbuka nimeanza kumwona akihubiri miaka ile ya mwishoni mwa themanini huku akiwa anatembea kwenye kamba yake aliyoifunga kwenye miti iliyo na umbali wa kama mita 8 au 12 hivi na urefu wa kama futi 10 hadi 14 hivi huku akiwaambia watu wamfuate YESU kwani yeye ndio njia,kweli na uzima na kuwa njia ya kwenda mbinguni ni nyembamba na imesonga sana.Mazungumzo yetu yalikuwa kama ifuatavyo:-

Mtade: Bwana asifiwe Mwinjilisti Njia Nyembamba..!
Njia Nyembamba: Amen mpendwa..karibu sana.
Mtade: Ahsante sana mtumishi.
Njia Nyembamba: Ndio kijana, karibu sana ..na ..(akiwa anajifuta jasho na leso yake huku akinitazama usoni)
Mtade: Mimi naitwa ndugu Mtade,kutoka mlima wa sayuni,nimevutiwa sana na mahubiri yako na ningependa kuongea na wewe mawili matatu ili kukufahamu zaidi
Njia Nyembamba:Oohh…karibu sana ila sijajua vizuri kama mlima Sayuni ni nini hasa?
Mtade: Ndio mwinjilisti, mlima sayuni ni mtandao wa computer ulioenea dunia nzima unaowaunganisha wakristo wote wanaoliitia jina la Bwana ili kufundishana,kupashana habari,kurekebishana,kutiana moyo, kushuhudiana, kumtukuza Mungu na kuifanya kazi ya Mungu kwa pamoja kupitia mtandao wa computer, kuombeana mahitaji mbalimbali na mengine yanayofanana na hayo.
Njia Nyembamba:Ooh ..that is wonderful,nimefurahi sana kukutana na wewe ndugu Mtade.Mimi jina langu halisi ni Mch.Lucas Paulo Nchimbi ila wengi wananifahamu kwa jina la Njia Nyembamba.
Mtade:Nashukuru kujua hilo Mch.Lucas…sijui umeanza huduma hii ya kuwaleta watu kwa YESU lini..?
Njia Nyembamba: Mimi nimeokoka mwaka 1980 pale kanisani TAG Temeke(kwa sasa ni eagt temeke) kwa Mch. Masalu.Na mwaka 1988 mwezi wa 9 nilianza kazi ya kuhubiri injili.
Mtade: Unaweza kutuelezea maisha yako kabla ya kazi hii ya kuhubiri injili.
Njia Nyembamba: Kwanza mimi ni mwanajeshi mstaafu wa jeshi la wananchi wa Tanzania.Nimetumikia jeshi kuanzia mwaka 1970 hadi mwaka 1987 mwezi april nikastaafu ili kumtumikia Mungu.
Mtade: Nini kilitokea hadi ukaokoka?
Njia Nyembamba: Ndg Mtade..kuna dada mmoja alikuwa ameokoka alikuwa anasali kanisani pale temeke miaka ile na alinikaribisha jumapili moja.Nilisali mahali pale na usiku ulipofika wakati nimelala nyumbani kwangu niliona mbingu zimefunguka na mwanga mkali mweupe ukanimulika na nikasikia sauti ikiniambia niokoke na nibaki mahali pale kanisani.Kwa asili mimi nilikuwa mkristo wa dhehebu la katholiki lakini ile sauti ilijaa utisho wa ajabu.Hivyo tangu siku ile nikaokoka na kuamua kusali pale temeke.
Mtade: Kwa hivi sasa unasali kanisa gani …bado upo pale?
Njia Nyembamba: Hapana, pale niliwekewa mikono rasmi na wachungaji ya utumishi huu..na hivyo nikaamua kuingia shambani na kuanza kuwahubiria watu.Kwa sasa nimeanzisha huduma inayoitwa Kanisa la Yesu ulimwenguni la njia Nyembamba ambalo lipo huko kigamboni ambayo ndio base station yangu.Mwaka 1988 nilianzia pale Shauri moyo ambapo baadaye alikuwa Mtume Maboya kwani kuna mama mmoja nilikuwa naye pale, alinikuta lakini baadaye akafanya hila akanipindua na kulipeleka kanisa kwa Mtume Maboya.
Kwa wakati huo nilikuwa na washirika wapatao 160 ambapo kati yao watoto walikuwa 100 na watu wazima walikuwa 60.
Pia kipindi hicho nilikuwa na matawi mengine mawili maeneo ya buguruni shule na kidongo chekundu kuanzia mwaka 1988 hadi 1994.Lakini nako pia mambo yakawa yaleyale,kwani nilinyang’anywa makanisa yote hayo.
Baada ya muda Mungu amenipatia eneo jingine kigamboni na hapo nimeanza na washirika watoto wadogo 10 na watu wazima 6.
Mtade: Aisee ni historia nzuri ya kusikitisha na kufariji pia.Mch.Lucas umeo au unao watoto?
Njia Nyembamba: Hapana, sijaoa hadi sasa na wala sina motto.
Mtade:Nini maono ya huduma yako kwa siku za baadaye?
Njia Nyembamba: Kwa kweli pamoja na huduma hii ya uinjilisti na uchungaji pia natumika kwa roho ya unabii.Nakumbuka kipindi kile kabla Rais Kabila wa kongo (Iliyokuwa Zaire) hajauwawa Mungu alinionyesha mambo yatakayoipata nchi hiyo na kwa kulithibitisha hili kuna nabii mwingine anaitwa Rafael Simbamanga naye alionyeshwa the same,Mungu akatuambia twende DRC kuongea na Rais Kabila na kumpelekea ujumbe wa Mungu.Lakini tulikutana na upinzani pale ubalozini kwani walitunyima visa.Hivyo tulishindwa kwenda na matokeo yake DRC vita kali ililipuka na Rais Kabila akauwawa na….(Nikamkatisha)
Mtade: Nazani huo ushuhuda kuna siku nitakuja tena unielezee kwa kirefu ila kwa sasa naomba kujua nini maono ya huduma yako hii ya sasa.
Njia Nyembamba: Ahh..kwa kweli ndg.Mtade maono ya huduma yetu kwa sasa ni kuwa tunataka kuanzisha kituo cha kulelea vichaa na watoto wanoishi katika mazingira magumu.Mungu amenipa huo mzigo wa kutaka kuwakusanya hawa vichaa wote walioko mjini na kuwatunza pale kwenye kituo chetu kigamboni.Maana nao ni watu na wanastahili elimu bora,chakula bora,malazi bora na matibabu ili wapone warudi katika hali zao za kawaida kama watu wengine.Kuna kipindi niliwahi kumwombea kichaa mmoja mwenye uhusiano na waziri mmoja wa serikali ya sasa.Na Mungu aliponya siku hiyo.Ngoja nikuonyeshe picha za tukio hilo (anatoa picha nyingi za kijana huyo aliyekuwa kichaa na jinsi alivyomwombea na kuponywa).Kwa hiyo kama nilivyosema tunataka pamoja na kuwahubiria watu tuwe tunawapa na huduma hawa ndugu zetu vichaa na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.Tatizo kubwa linalotukamisha ni pesa.Hatuna funds za kutosha kutimiza malengo yetu mengi mazuri tuliyojiwekea.Ningependa kuchukua fursa hii kukuomba ndg Mtade kama kuna watu unawafahamu wanaoweza kutusaidia kifedha itakuwa jambo jema sana.
Mtade: Usijali mtumishi wa Mungu..sisi wanasayuni tutakutangaza duniani kote maana ndio wajibu wetu na Mungu kwa wakati wake atatenda kitu.
Njia Nyembamba: Asante sana san asana kwa hilo mtumishi wa Mungu.
Mtade: Asante nawe pia…naomba nikuage then nitakutafuta week ijayo kwa mazungumzo zaidi.Mungu akubariki sana.
Kwa atakaye penda kuwasiliana au kwa maelezo zaidi kuhusu Mch. Lucas Paulo Nchimbi (Njia Nyembamba) anaweza kuwasiliana na sayuni.

Mungu awabariki sana.

1 comment:

Maranatha said...

Aiseehh Mtade Mungu akubariki ka hii story ya huyu mtumishi njia Nyembamba! Niliwahi sikia stori zake zamani sana kupitia mchungaji wangu ila sikujua kama yupo hai na wapi. Sasa kwa habari hii walao umenifungua kujua kwamba bado yupo na anaendelea kumtetea YESU! Ila sijajua kama bado anaendelea kuitumia ile style yake kaiacha!!?? Nimeupnda sana huo ubunifu wake maana huitaji kupiga panda ili watu wasogee karibu, kwani ni wangapi wenye uwezo wa kutembea juu ya kamba kwa ujasiri kama wake??

Ubarikiwe sana Mch. Njia Nyembamba!!!